Uingereza yathibitisha kuwazuia wahamiaji – DW – 01.05.2024

Haya yanajiri huku mmoja akiripotiwa kujipeleka kwa hiari Rwanda kutoka Uingereza. 

Kamata kamata ya wahamiaji inajiri wiki moja baada ya wabunge kumaliza mvutano uliokuwepo bungeni na kupitisha sheria hiyo baada ya kutangaza kuwa Rwanda ni nchi salama.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, aliapa kuwazuia wahamiaji kuingia Ulaya kupitia njia za baharini, na wiki iliyopita aliahidi kuanza kuwakamata watu kabla ya kuwahamisha rasmi Rwanda ndani ya wiki 10 na 12 zijazo.

Soma pia:Mpango wa Uingereza kuwahamishia wakimbizi Rwanda kugharimu pauni milioni 300

Ripoti za maafisa wa utekelezaji wa uhamiaji kuwazuia watu waliopangiwa safari za ndege ziliibuka mapema wiki hii. Siku ya Jumatano, wizara ya mambo ya ndani ilithibitisha kuwa kuna “operesheni ya kamata kamata kitaifa” inaendelea.

Aidha wizara hiyo ilitoa video zilizowaonyesha maafisa wa utekelezaji wa uhamiaji wakiwatoa watu majumbani mwao, kuwafunga pingu na kisha kuwaingiza katika magari ya polisi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza James Cleverly amesema wanafanya kazi kwa kasi kuwaondoa wale wote wasio na haki ya kuishi nchini humo.

Soma pia:UN yaitaka Uingereza kufirikia upya sheria yake ya uhamiaji

Mbunge mmoja wa Uingereza siku ya Jumanne alifichua kuwa serikali inatarajia kuwafukuza wahamiaji 5,700 hadi Rwanda mwaka huu, baada ya wizara ya mambo ya ndani kuthibitisha kwamba Kigali “kimsingi” ilikubali kupokea idadi hiyo.

Wahamiaji wahofia usalama wao 

Migranten im Ärmelkanal vermisst
Picha: Gareth Fuller/PA/AP/picture alliance

Watafuta hifadhi wameanza kutoroka Uingereza kuelekea katika mji unaokua kwa kasi wa Dublin nchini Ireland na wanasema maisha chini ya turubai ni bora na salama kuliko hatari ya kupelekwa Rwanda.

“Nilikuja Dublin jana kutoka Uingereza. Kwa hivyo leo nimeomba hifadhi hapa. Na sasa sijui niende wapi, nifanye nini, hakuna malazi, hakuna chochote, lakini naweza kuhisi niko salama. Natokea Afghanistan huko kuna Taliban, nilikuja hapa kujisikia salama. Na kama watatupeleka Rwanda, siwezi kujisikia salama huko.”

Hata hivyo sio wote wanahofia kwamba Rwanda sio salama, hapo jana mtu mmoja aliyeshindwa kupata hifadhi Uingereza amesafiri kwenda Rwanda chini ya mpango wa hiari.

Naibu Msemaji Mkuu wa Serikali ya Rwanda, Alain Mukuralinda, amesema mtu huyo, ambaye uraia wake haukufichuliwa, amepokelewa na wanamuhudumia, na baada ya siku chache wanatarajia kwamba atawaambia kuhusu matakwa yake iwapo anataka kubakia Rwanda au kwenda nchi nyengine.

Rwanda, ambayo ni makazi ya watu milioni 13 katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika, inadai kuwa moja ya nchi tulivu zaidi barani humo na imejizolea sifa kwa miundombinu yake ya kisasa.

Soma pia: UN yaitaka Uingereza kuachana na mpango wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda

Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yanamshutumu Rais Paul Kagame kwa kutawala katika mazingira ya hofu, kukandamiza upinzani na uhuru wa kujieleza.

 

 

Related Posts