Badala yake, Waziri Mkuu Keir Starmer ameahidi “kuvunja magenge” yanayofaidika na wahamiaji wanaovuka ujia wa bahari wa English Channel kutoka kaskazini mwa Ufaransa, ambao mara nyingi hukumbwa na madhila.
Waziri wa Mambo ya Ndani Yvette Cooper amesema hadi dola milioni 99 za mpango huo sasa zitawekezwa katika vifaa vya uchunguzi wa siri ili kuimarisha ukusanyaji wa ushahidi kwa ajili ya kuwashitaki viongozi wa magenge hayo.
Soma pia:Mpango wa Sunak wakuwapeleka wahamiaji Rwanda wafanikiwa
Pia zitatumika kuwalipa wafanyakazi wa usalama wa mpakani na wachunguzi zaidi ya 100 waliobobea katika Shirika la Kitaifa linalofuatilia Uhalifu, kama sehemu ya mbinu jumuishi zaidi miongoni mwa wasimamizi wa sheria katika kushughulikia suala hilo.
Cooper amesema “Teknolojia ya hali ya juu na uwezo thabiti wa kijasusi utatuwezesha kutumia kila zana ili kukomesha biashara hii mbaya.”
Serikali ya Uingereza inasema inataka kukabiliana na tatizo la uhamiaji ikishirikiana na majirani zake wa karibu barani Ulaya kuzuia wahamiaji zaidi kuhatarisha maisha yao kwa kutumia boti dhaifu.
Soma pia:UN : Mfumo wa hifadhi ya wakimbizi wa Rwanda haujitoshelezi
Tayari imeongeza idadi ya maafisa wa Uingereza walioko kwenye polisi ya kimataifa, Europol kusaidia juhudi za Ulaya kuvunja mitandao iliyopo ya kusafirisha watu.
Starmer alikuwa mjini Roma siku ya Jumatatu kuangazia juhudi za Italia za kupunguza uhamiaji usio wa kawaida, ikiwa ni pamoja na mipango ya kuendesha vituo vya wahamiaji vinavyoendeshwa na Italia nchini Albania.
Siku ya Jumapili, watu wanane walikufa wakati meli iliyokuwa imefurika watu ilipozama katika pwani ya Ufaransa wakati ikijaribu kuvuka njia ya meli yenye shughuli nyingi, chini ya wiki mbili baada ya watu wengine wasiopungua 12 kupoteza maisha.
Cooper mnamo mwezi Julai aliuita mpango wa wahamiaji ulioandaliwa na chama cha Conservatives’ kuwa ni “ufujaji wa kushtusha zaidi wa fedha za walipa kodi ambao hajawahi kushuhudia”.
Aliliambia Bunge kwamba kiasi pauni milioni 700 zilitumika katika mpango huo na serikali iliyokuwa imepanga kutumia zaidi ya pauni bilioni 10.