Watatu wa familia moja wakutwa wameuawa Dodoma, mama yao ajeruhiwa

Dodoma. Watu watatu wameuawa, huku mama mwenye nyumba akijeruhiwa na watu wasiojulikana katika Mtaa wa Segubwawani, Kata Nala jijini Dodoma.

Waliouawa ni watoto wawili wa familia moja ambao miili yao imekutwa imeungua motor, huku mfanyakazi wa ndani akikutwa na majeraha kichwani.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Anania Amo akizungumza na Mwananchi usiku wa jana Jumatatu Septemba 16, 2024 amesema watu watatu walikutwa wamefariki dunia.

Amesema mmoja ambaye ni mama mwenye nyumba alikutwa amejeruhiwa na amepelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

“Huyo aliyewahishwa hospitali anaonekana ana jeraha kichwani na watatu tuliendelea kuangalia hali ya majeraha waliyoyapata kabla hawajafariki. Hawa wawili (watoto), walikutwa wameungua isipokuwa mmoja ndiyo amejeruhiwa hajaunguzwa,” amesema.

Amesema hakuna jirani aliyesikia kelele, bali mtoto aliyetumwa kwenda katika familia hiyo ndio alirudisha habari kuwa hakupata ushirikiano.

“Majirani waliposogea katika nyumba hiyo, mtoto wa miaka sita ambaye alikuwa katika nyumba hiyo, lakini hajajeruhiwa ndiye alipiga kelele akiomba kufunguliwa maana milango ilikuwa imefungwa. Ndio baadaye waligundua  kuna mauaji yamefanyika,” amesema.

Tukio hilo ni mwendelezo wa matukio ya mauaji mkoani Dodoma ambayo yamekuwa wakitokea katika siku za hivi karibuni. Mengine yamekuwa wakihusishwa na visasi.

Mwenyekiti wa Mtaa Segubwawani, Kata ya Nala, Jeremia Molima amesema alipewa taarifa ya tukio hilo saa 9.45 alasiri na alipofika eneo hilo alikuta watu wanaingia ndani na kutoka nje.

“Lakini nikawaomba watu wasiingie ndani kwa sababu tunasubiri askari wafike. Baada ya kufika nilikuta watoto wawili wameungua kwa moto, halafu kuna dada wa kazi amelala kifudifudi amekufa, anaonekana kichwa chake kimeshambuliwa kwa sababu kwenye sakafu damu imeganda,” amesema.

Amesema walimkuta mama mwenye nyumba akiwa hai, lakini ameshambuliwa:”Yeye alikuwa akitamka kuwa anajihisi maumivu, anaomba akalale.”

Amesema walichokifanya ni kumuita bodaboda kwa ajili ya kumuwahisha kat

Zahanati ya Nala kwa ajili ya huduma ya kwanza na wakati huo huo wakiwasiliana na polisi kata ambaye aliwaeleza yuko njiani akielekea eneo la tukio.

Molima anasema baba wa familia aliyemfahamu kama Robert Mugema ni Mwalimu mkoani Singida, hivyo katika nyumba hiyo walikuwa wakiishi mama, watoto wake watatu na mfanyakazi wa ndani.

Amesema Septemba 14, 2024 walikuwa na sherehe ya mtoto aliyemaliza darasa la saba (mmoja kati ya aliyeuawa), hivyo baba wa familia hiyo alifika katika sherehe ya kumpongeza mtoto wao na haikufahamika wakati tukio linatokea kama alikuwa amesharejea katika kituo chake cha kazi ama la.

“Inaelekea watu waliwavamia, wakawapiga hadi kufa, lakini hawa watoto wawili walioungua ndio tunashindwa kupata majibu ya haraka,” amesema.

Amesema wamekuta hakuna dalili ya moto kuwaka muda wa karibuni na hivyo wanahisi tukio hilo lilifanyika usiku.

Alipoulizwa walijuaje kuhusu mauaji hayo, Molima amesema Jumamosi walipokuwa na sherehe ya mtoto wao kumaliza darasa la saba (mmoja wa marehemu), walikwenda kuazima redio kwa jirani kwa ajili ya sherehe.

Amesema leo, mwenye redio alimtuma mtoto mdogo kwenda kuifuata,  lakini alipofika alikuta milango yote imefungwa, pamepoa na hakuna mtu anayeitika.

“Alirudi nyumbani kuwaeleza hali hiyo, ndipo majirani wakaenda. Lakini ndani ya nyumba kulikuwa na mtoto mdogo, (ambaye hakuguswa), baada ya kuita kwa muda ndipo mtoto aliitika ambaye alikuwa akisema anaogopa kufungua mlango,” amesema.

Amesema walipofungua wenyewe kwa nje na kuingia ndani na kukutana na mauaji hayo.

Molima amesema wamekuta nguo zimevurugwa ziko chini, lakini kuna televisheni iko ukutani na haijaguswa kwa lolote.

Kwa upande wake, Diwani wa Nala, Herman Masila amesema miili ya watoto wawili ilikutwa chumbani kwao ikiwa imechomwa moto, huku mwili wa mfanyakazi wa ndani na mama aliyejeruhiwa ukiwa sebuleni.

“Tukio ni kubwa sana hili, tunashindwa kuelewa ilikuwaje. Hii inaonekana ni tukio la usiku kwa sababu lingekuwa limetokea jana, ingekuwa ni leo wangekutana na moto bado unawake,” amesema.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

Related Posts