Ukiingia mtandaoni ni rahisi kuuliza kiasi cha umbali kutoka Dar es Saalam kwenda mikoa mbalimbali ya nchi yetu.
Sio umbali wa mikoani pekee, mtandao unaweza kukusaidia kujua hata umbali kwenda nchi jirani.
Hata hivyo, umewahi kujiuliza ndani ya Dar es Salaam umbali huo unaanza kuhesabiwa eneo gani?
Je, tunaanza kuhesabu kuanzia Kiluvya eneo linalopakana na Pwani katika njia kuu ya Morogoro iendayo mikoa mingi ya nchi yetu na hata nchi nyingi jirani?
Swali hilo jibu lake ni hapana. Ukweli ni kuwa umbali wa Dar es Salaam na maeneo nengine unapimwa kuanzia ulipo Mnara wa Saa.
Naam! Ni Mnara wa Saa ulio kwenye makutano ya mitaa ya Samora na Nkrumah, huku ukiwa na historia ya kipekee zaidi ya kuwa “ zero point ya Jiji la Dar es Salaam.
Kwa wasiojua kimombo, ‘zero point ‘ tunamaanisha eneo la kuanzia kupima umbali. Na pengine unaweza kusema ndio katikati ya jiji. Kwa maneno mengine, hapo ndipo kilipo kitovu cha jiji hili kubwa zaidi nchini.
Mnara huo ulizinduliwa na aliyekuwa mume wa Malkia Elizabeth, Prince Philip, Desemba 10, 1961.
Hata hivyo, zipo simulizi nyingine zinazoeleza kuwa ‘zero point’ya Dar es Salaam ni pale lilipo sanamu la askari kwenye makutano ya Mtaa wa Samora na Azikiwe ambao zamani ulijulikana kwa jina la Maktaba.
Sanamu hiyo inamuonyesha askari wa asili ya Kiafrika akiwa ameshika silaha kukumbukia ushiriki katika Vita ya Kwanza ya Dunia.
Wanahistoria na wenyeji wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Abdallah Tambaza na Sheikh Mohammed Said kwa nyakati tofauti walisema, mnara huo ni moja ya alama zilizoweka wakati wa Uhuru wa Tanganyika.
Wanasema mnara huo ulizinduliwa siku moja baada ya Uhuru, Desemba 9,1961 na mume huyo wa Malikia aliyekuja nchini kuwapa Watanganyika Uhuru akiwa sambamba na Mwalimu Julius Nyerere.
“Siku hiyo ndipo Manispaa ya Dar es Salaam ilifanywa kuwa jiji, kabla ya hapo nchi nzima hakukuwa na jiji, miji mikubwa ilikuwa ni Dar es Salaam na Tanga, maeneo mengine yalikuwa ni halmashauri ndogo ndogo,” anasema Alhaj Tambaza.
Anasema, siku ya Desemba 10, 1961 ndiyo Meya wa kwanza wa Jiji la Dar es Salaam, Sheikh Kaluta Amri Abeid alipoapishwa pale.
“Ilikuwa ni sherehe kubwa, paliwekwa majukwaa pale, Meya akala kiapo na Tanganyika ikapata jiji la kwanza.
“Kabla ya kuwekwa mnara wa saa, ilikuwa ni eneo la roud about (makutano) ambapo hadi sasa ndiyo zero point ya jiji inakoanzia, ukitaka kuhesabu maili unaanzia pale,” anasema.
Sheikh Kaluta ambaye pia alisifika kwa umahiri wa utunzi wa mashairi na elimu ya dini ya dini, aliwahi pia kushika nafasi ya uwaziri wa katiba katika Serikali ya awamu ya kwanza.
Kwa upande wake, Sheikh Said anasema anasema jirani na mnara huo, kulikuwa na eneo likiitwa Kichwere, uwanja uliosifika kutoa riziki kwa wafanyabiashara wadogo.
“Hilo eneo liliitwa Kichwere kwa kuwa kina mama walikuwa wakipeleka biashara zao, yoyote aliyekuwa akipeleka biashara hapo, hata iwe saa ngapi atauza, ikawa eneo hilo linaitwa la biashara hadi kichwere,”anasema.
Huo ndio Mnara wa Saa wa Jiji la Dar es Salaam. Si jiji hili pekee, minara ya aina hiyo inaweza kuwapo maeneo mbalimbali. Ni muhimu Watanzania wakajihimu kujua historia ya alama hizo muhimu za miji yetu.
Ikiwa na maoni, ushauri wasiliana nasi kwa namba 0754990083