Wangoni hawaishiwi na mambo. Kabila hilo wenyeji wa Mkoa wa Ruvuma, achilia mbali umaarufu wao wa ushujaa vitani, wana simulizi ya kuvutia.
Ni simulizi ya asili ya majina ya jadi ya kabila hilo linalotajwa kuingia Ruvuma miaka ya mwishoni mwa 1930 likitokea kwenye chimbuko la Wanguni na Wazulu nchini Afrika Kusini.
Kwa Wangoni, sio jambo geni kukuta majina kama Simba, Nyoka, Tembo, Komba, Mbawala, Mbuzi, Kifaru na mengineyo kedekede.
Wangoni pia wana ufundi wa kutumia majina ya wanyama kwa kuongeza herufi aghalabu nyuma ya majina hayo. Ndipo unapokuta majina kama Ngonyani, Mapunda, Katembo.
Hata hivyo, kuna siri kubwa nyuma ya utamaduni huu wa kutumia majina. Kumbe Wangoni walitumia majina hayo kama njia ya kuficha utambulisho hasa kwa maadui zao wakati wa vita
Chifu wa Wangoni Manispaa ya Songea, Samwel Mbano, anasema majina ya wanyama yalikuwa na maana maalum na yalitumiwa na mababu zao ili wasitambulike hasa katika harakati za vita.
Anasema kwa kutumia majina hayo bandia wapiganaji waliweza kupita maeneo mbalimbali kwa urahisi.
“Anatumia jina la Nguruwe, akiulizwa nguruwe mbona ni mnyama analiwa, anajibiwa basi kamuangalie huyo mnyama yupo wapi, hivyo tayari anapata upenyo wa kupita na hivyo aliweza kutembea mikoa mbali mbali na nchi mbali mbali kutoka Afrika kusini kwa miaka 45 mpaka kufika Tanzania, anasema.
Hata hivyo, anaeleza kuwa ikiwa mtu atataka kutumia jina kama vile Tembo au Nyoka, anatalazimika kwenda kufanyiwa mila ndogo za kukaribishwa kwenye ukoo huo na kukaribishwa rasmi.
” Ukienda tofauti bila kufanyiwa mila kuna madhara makubwa yatamkuta tofauti na unavyotarajia, hivyo mila ziheshimiwe,” anasisitiza chifu Mbano ambaye ni mjukuu wa Chifu Songea Mbano aliyawahenyesha vilivyo Wajerumani wakati wa Vita vya Majimaji.