Kamati Chadema yaanza kikao, watia nia roho juu

Dar es Salaam. Jopo la wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameanza kikao cha kujadili mambo mawili ikiwamo kupokea taarifa ya hali ya usalama nchini.

Jambo lingine, linalotarajiwa kuangaziwa ni kufanya usaili na kuteua wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwamo uenyekiti kutoka kanda za Pwani, Kusini na Pemba.

Kikao hicho kinafanyika leo Jumanne, Septamba 17, 2024 ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam kikiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja na wajumbe wengine akiwamo makamu mwenyekiti wa Chadema bara, Tundu Lissu.

Viongozi wa Chadema wakizungumza kabla ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho. Picha na Michael Matemanga

Kikao hicho kimeanza saa 4:30 baada ya kuwasili Mbowe katika ofisi hizo kisha kuingia katika ukumbi huo kuanza kujadili taarifa ya hali ya usalama huku watia nia katika nafasi mbalimbali za uongozi kutoka kanda tatu za Pwani, Kusini na Pemba wakisubiri nje.

Watia nia hao wanasubiri kupewa utaratibu ambao kimsingi hautakuwa tofauti na uliofanyika Mei 2024 kwa kanda nne za chama hicho zilizofanyiwa usaili Kanda ya Nyasa, Magharibi, Victori na Serengeti.

Mfumo waliotumia wakati huo walikuwa wanafanya usaili kwa kuanza na kanda moja hadi nyingine na walikuwa wanaita watia nia kwa majina kulingana na nafasi wanazoomba kuteuliwa kugombea na kuulizwa maswali.

Maswali wanayoulizwa katika usaili huo huwa yanajikita katika nafasi wanazoomba na kama aliwahi kuwa kiongozi, huwa wanachimbua historia yake na kama alifanya mambo tofauti huwa anaulizwa na kumpatia nafasi ya kujitetea mbele ya jopo hilo.

Kujichanganya kujibu maswali hayo mara nyingi umekuwa mwiba kwa watia nia hao kuenguliwa, lakini hoja hiyo huwa inasimamiwa na jopo hilo ikiamini kushindwa kwake kujitetea vizuri, hata akipewa nafasi utendaji wake utakuwa na mashaka.

Watia nia kutoka kanda hizo katika ofisi hizo wamekaa kimakundi makundi wakipeana nasaha mbalimbali baadhi wakijipa moyo atakayepenya basi anaenda kukiwakilisha chama, hivyo watamuunga mkono.

Kanda inayotarajiwa kuvuta hisia mseto ni Pwani hasa katika nafasi ya uenyekiti kwa watia nia wawili Boniface Jacob na Gervan Lyenda waliojitosa kuomba kuteuliwa kuomba kugombea nafasi hiyo.

Lakini si hivyo, Pwani inaonekana kuwa na idadi kubwa ya watia nia ikilinganishwa na kanda zingine mbili ya Kusini na Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 16 2024 na Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya Mambo ya Nje, John Mrema kikao hicho kinafanyika kwa kuzingatia katiba ya chama ya mwaka 2006 toleo la 2016.

“Kikao hiki kitaongozwa na mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe kufanya usaili na kuteua wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika kanda tatu za Pwani, Kusini na Pemba,” alisema Mrema.

Hata hivyo, Mwananchi imedokezwa maandamano kufanyika Jumatatu ya Septemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam kupinga matukio ya utekaji na mauaji na waliotekwa kurejeshwa wakiwa hao ama miili yao.

Msingi wa maandamano hayo ni mauaji yaliyofanywa na watu wasiojulikana kwa mjumbe wa sekeretarieti wa Chadema, Ali Kibao.

Kibao alitekwa na watu Septemba 6, 2024, akiwa katika usafiri wa umma, eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam. Mwili wake uliokotwa Ununio ukiwa umemwagiwa tindikali usoni.

Chadema imewataka wanachama na viongozi nchi nzima kwenda Dar es Salaam kushiriki maandamano hayo.

Tayari Jeshi la Polisi Tanzania limepiga marufuku maandamano hayo likisema atakayethubutu kuandamana hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Related Posts