Fahamu mambo ya kuzingatia, kuepuka unapokuwa mgonjwa

Dar es Salaam. Septemba 17 ya kila mwaka ni maadhimisho ya Siku ya Usalama wa Mgonjwa Duniani.

Lengo la ni kuzingatia usalama wa mgonjwa kwa kuanzisha na kuimarisha mifumo inayotegemea sayansi, kuboresha usalama wa wagonjwa na ubora wa huduma za afya.

Maazimio ya Mkutano wa Mkuu wa 72 wa Afya Duniani (WHA72.6)  uliofanyika mwaka 2019, ulizitaka nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kutoa kipaumbele cha usalama wa mgonjwa kisera na kupitia programu za sekta ya afya kufikia bima ya afya kwa wote.

Pia, nchi wanachama wanapaswa kuanzisha na kutekeleza sera za kitaifa, sheria, mikakati, miongozo, zana na kutoa rasilimali zinazofaa ili kuimarisha usalama wa huduma zote za afya, kadri inavyofaa.

Wataalamu wa afya wameeleza mambo anayopaswa kufanya mgonjwa na yasiyopaswa ili kuimarisha usalama wake hospitalini na nyumbani.

Mtaalamu wa magonjwa ya binadamu Dk Ernest Winchislaus amesema mgonjwa akiwa hospitalini anapaswa kufuata maelekezo ya madaktari na wauguzi.

“Ni muhimu mgonjwa aelewe na kufuata ushauri na matibabu anayopatiwa ili kuhakikisha anapata matokeo bora ya afya,” amesema Dk Winchislaus.

Pia, mgonjwa akiwa hospitali anapaswa kudumisha usafi binafsi, kuosha mikono kabla ya kula na baada ya kutumia choo na kufuata kanuni za usafi ili kupunguza hatari ya maambukizi.

Jambo lingine ni kuchukua dawa kwa wakati na kuwa makini muda wa kutumia dawa na kuhakikisha amekula kama alivyoelekezwa.

“Atoe taarifa kwa wauguzi kuhusu mabadiliko ya hali ya afya iwapo atapata maumivu makali au mabadiliko yasiyo ya kawaida kama homa, alete taarifa mapema ili kupata msaada wa haraka, adumishe mawasiliano na ndugu hii ni muhimu kwa afya ya kiakili na kiroho.

“Mawasiliano na wapendwa yanaweza kusaidia mgonjwa kukabiliana na changamoto za matibabu,” ameeleza Dk Winchislaus.

Amesema mgonjwa anapaswa kuheshimu usiri wa taarifa zake za kiafya na kuhakikisha anafahamu haki yake ya usiri wa taarifa, ikiwa ni pamoja na kuepuka kutoa taarifa zake kwa watu wasiohusika bila ridhaa yake. Hospitali zinapaswa kutunza taarifa zake kwa siri.

“Kutoa ridhaa sahihi ya matibabu kabla ya matibabu yoyote kufanyika, mgonjwa lazima apewe maelezo kamili kuhusu matibabu hayo, madhara yanayoweza kutokea na mbadala wa matibabu ili aweze kutoa ridhaa yake kwa uelewa. Hii ni haki ya msingi ya mgonjwa kuhakikisha anaelewa vyema kile kinachofanyika kwa mwili wake na matokeo yanayotarajiwa,” amesema.

Dk Winchislaus amesema mgonjwa hapaswi kutumia dawa bila ruhusa ya daktari kwa kuwa hatari yake ni kusababisha mgongano wa dawa, kudhorotesha afya au kuchelewesha kupona.

Pia, hapaswi kutembea bila ruhusa au msaada, kama mgonjwa hajaelekezwa kutembea bila msaada, anaweza kuanguka na kuumia zaidi.

“Pia, asipuuze dalili mpya au zisizo za kawaida, kama vile maumivu mapya na mabadiliko katika mkojo au kinyesi, vilevile kujihusisha na shughuli zinazochosha bila idhini. Mgonjwa anapaswa kuepuka kufanya kazi ngumu au mazoezi mpaka aidhinishwe na daktari,” amesema Dk Winchislaus.

Amesema pia mgonjwa hatakiwi kutoa taarifa zake za afya kwa watu wasiohusika.

“Mgonjwa hapaswi kushiriki habari za hali yake ya kiafya na watu wasiohusika ili kulinda usiri na faragha yake. Ni muhimu kuhakikisha mazungumzo yanahusisha tu watu wanaoruhusiwa kisheria, kama vile daktari, wanafamilia waliochaguliwa au wawakilishi wa kisheria,” amesema.

Mbali na hayo, amesema mgonjwa hapaswi kukubali matibabu bila kufahamu kikamilifu yaani bila kupewa maelezo ya kina kuhusu athari zinazoweza kutokea, faida za matibabu hayo na mbadala wa matibabu yanayopendekezwa.

Pia, amesema mgonjwa hapaswi kujitibu kwa kutumia mitishamba bila ushauri wa daktari.

Hali hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa, hasa kama mgonjwa anatumia dawa za hospitali anapaswa kutokula vyakula vilivyokatazwa.

“Mgonjwa anatakiwa kufuata lishe iliyopendekezwa na daktari ili kuzuia madhara au kuchelewesha kupona, kujihusisha na kazi ngumu mapema sana, kufanya kazi ngumu bila ruhusa ya daktari kunaweza kudhorotesha hali ya mgonjwa au kuchelewesha kupona.”

Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige amesema  daktari anapomuandikia mgonjwa sindano ni lazima amfahamishe anamchoma sindano gani na wakati gani kwa lengo la kuokoa maisha yake.

“Kuna sheria 12 ambazo zimewekwa na WHO tangu mwaka 1948 zinazozingatia hali na desturi za mgonjwa na namna anavyopaswa kuhudumumiwa, mosi mgonjwa amfahamu daktari kwa jina lake, daktari amuelimishe mgonjwa kuhusu tatizo lake ili lisijirudie,” amesema Dk Mzige.

Pamoja na hilo, amesisitiza uwepo wa usiri baina ya mgonjwa na daktari akihimiza wagonjwa kutopuuza maumivu au dalili mbaya kwani kunasababisha hali kuwa mbaya zaidi, bila mgonjwa kupata msaada wa haraka.

Related Posts