Mpole apewa kazi ya kuimaliza Singida Black Stars

KOCHA wa Pamba Jiji, Goran Kopunovic ameonyesha kuwa na matumaini na safu ya ushambuliaji inayongozwa na George Mpole licha ya kutofunga katika michezo mitatu iliyopita ya Ligi Kuu Bara.

Mserbia huyo anaamini safu hiyo inaweza kuonyesha makucha leo Jumanne kwenye uwanja wa nyumbani wa CCM Kirumba, Mwanza itakapoikaribisha Singida Black Stars inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zake tisa kileleni.

Kopunovic alisema kadri ambavyo wamekuwa wakicheza ndivyo kikosi chake kimekuwa kikiimarika, hivyo mashabiki wa timu hiyo wategemee mazuri.

“Najivunia kundi hili la wachezaji, vipo viashiria vingi vizuri juu ya mwenendo wetu, tulifunga dhidi ya Azam lakini bahati haikuwa upande wetu na tulitengeneza nafasi kadhaa.

“Ingekuwa mbaya kwetu kama tungekuwa tukishindwa kutengeneza nafasi, nina imani na washambuliaji wangu na tumekuwa na programu mbalimbali za mazoezi ambazo zinaweza kuleta matunda,” alisema.

Mpole ambaye anatazamwa kama mshambuliaji kinara kwenye kikosi hicho anakumbukwa na wadau wengi wa soka kwa kile alichofanya 2021/2022 akiwa na Geita Gold kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu akiweka kambani mabao 17.

Akiuongelea mchezo wa leo, Kocha wa  Singida Black Stars, Patrick Aussems anaamini utakuwa mgumu lakini amewaandaa vijana wake kukabiliana na ugumu huo ili kuendeleza kile ambacho walikianza.

“Itakuwa mechi ngumu kwa sababu wenyeji wetu watakuwa wakitafuta ushindi wa kwanza, tupo hapa na sisi kuendeleza kile ambacho tumekianza katika michezo mitatu iliyopita,” alisema Mbelgiji huyo.

Licha ya Singida Black Stars kufunga mabao sita katika michezo mitatu iliyopita, watatakiwa kufanya kazi ya ziada kutokana na wenyeji hao kutoruhusu bao katika michezo mitatu iliyopita.

Pamba Jiji ambayo huu ni msimu wa kwanza Ligi Kuu Bara baada ya kukosekana kwa takribani miaka 22, imeanza taratibu kwa kutopata ushindi wowote, huku ikiwa haijafunga bao wala kuruhusu nyavu zake kutikiswa ikishuka dimbani mara tatu.

Singida Black Stars iliyoshinda mechi zote tatu ilizocheza, imefunga mabao sita na kuruhusu mawili.

Kwa upande mwingine, mechi hii ya leo inawakutanisha makocha wakuu ambao waliwahi kuifundisha Simba kwa nyakati tofauti.

Kopunovic anayeinoa Pamba Jiji, alipita Simba msimu wa 2014/15 akiifundisha timu hiyo kuanzia Januari 2015 hadi Juni 2015 akidumu kwa takribani miezi sita na kuondoka.

Aussems wa Singida Black Stars, naye alikuwa Simba kuanzia Julai 2018 hadi Novemba 2019, akifundisha msimu mzima wa 2018/19, kisha 2019/20 akiishia njiani.

Related Posts