Israeli yaongeza masharti katika vita vya Gaza – DW – 17.09.2024

Ofisi ya Waziri Mkuu imesema Netanyahu alielezea juu ya malengo hayo ya vita katika mkutano wa usiku wa kuamkia Jumanne 17.09.24, wa baraza la mawaziri la usalama kwamba sasa anataka Waisraeli waliokimbia maeneo ya karibu na mpaka wa Lebanon waruhusiwe kurejea nyumbani katika eneo la kakskazini.

Hayo yamefanyika huku kukiwa na taarifa kwamba Netanyahu anapanga kubadili nafasi ya Waziri wa Ulinzi.

Mzozo wa Mashariki ya Kati | Israel | Benjamin Netanyahu | Yoav Gallant
Wa nne kutoka Kushoto: Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Wa pili kutoka Kulia: Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant.Picha: Israel Ministry of Defense/Xinhua/IMAGO

Mara tu baada ya kumalizika mkutano huo wa baraza la mawaziri la usalama waandishi wa Habari waliripoti kuwa Netanyahu na Gideon Saar, aliyekuwa zamani waziri wa sheria walikuwa wanakaribia kukamilisha mpango ambao Saar atachukua nafasi ya Yoav Gallant kama waziri wa ulinzi.

Soma Zaidi: Mkuu wa sera za Kigeni ajae EU anamtazamo upi kuhusu Israel 

Saar, katika miezi michache iliyopita amekuwa akikosoa sera za serikali kuhusu vita vya Gaza na kuitaka ichukue hatua zaidi na madhubuti dhidi ya maadui wa Israel, ikiwa ni pamoja na Iran.

Saar pia amekuwa akikosoa hatua ya serikali ya Israel ya kutaka kukubali kufikia makubaliano na Kundi la Hamas ili kuumaliza mzozo wa Gaza, wakati waziri wa ulinzi wa sasa Yoav Gallant, amekuwa akishinikiza kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita yatakayojumuisha kubadilishana mateka wa Israel wanaoshikiliwa katika Ukanda Gaza na Israel kuwaachilia wafungwa wa Kipalestina.

Israel | Yair Lapid
Kiongozi wa Upinzani wa Israel Yair Lapid.Picha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Kwa upande wake kiongozi wa Upinzani wa Israel Yair Lapid, amesema maslahi ya kisiasa yanafaa kuwekwa kando ili kufikia makubaliano yatakayowezesha kuachiliwa kwa mateka wa Israel.

Lapid amesema: “Ninaamini kwamba masilahi yoyote ya kisiasa yanapaswa kuwekwa kando kwa ajili ya kufikia makubaliano. Hii ni njia muhimu zaidi. Israel kama taifa haitakuwa na amani mpaka tutakapowarudisha nyumbani raia wetu waliotekwa. Kwa hivyo, nitampa ushirikiano wowote muhimu, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ili kufanikisha juhudi za kufikia makubaliano.”

Soma Zaidi:  Israel yaonya juu ya kufifia uwezekano wa makubaliano ya kusitisha vita na Hezbollah

Kwingineko nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zitajadili leo Jumanne ombi la Wapalestina la kuitaka Israel kusitisha ukaliaji wake katika maeneo ya Wapalestina na walowezi wa Kiyahudi kuondoka katika maeneo hayo katika kipindi cha miezi 12.

Mswada huo unaotokana na maoni na ushauri wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliouita uvamizi wa Israel wa tangu mwaka 1967 kuwa ni “kinyume cha sheria.” umekosolewa vikali na Israel.

Umoja wa Mataifa | Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: ZUMA Wire/IMAGO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema Israel ina wajibu wa kukomesha uwepo wake kinyume cha sheria katika eneo la Palestina inalolikalia kimabavu.

Nchi za Kiarabu zimeitisha kikao maalum cha baraza hilo siku chache kabla ya wakuu wa nchi na serikali kuwasili kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York baadae mwezi huu kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la mwaka huu.

Vyanzo: AFP/DPA

 

 

Related Posts