Dar es Salaam. Baada ya mtumbwi wa uvuvi unaokadiriwa kuwa na watu 21 kuzama ndani ya Ziwa Victoria usiku wa Septemba 15, 2024, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) limewaonya wanaokiuka sheria na kuhatarisha usalama wa watu na vyombo vidogo majini.
Mtumbwi huo wenye jina la MV Marwa Kiss uliokuwa ukitoka Mwalo wa Iramba kuelekea Mwalo wa Igundu, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara uliondoka saa moja usiku na kuzama saa 2:30 usiku.
Kwa mujibu wa Tasac kupitia taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Septemba 17, 2024, ilikuwa imekodishwa kwa ajili ya kubeba abiria.
Baada ya ajali, abiria 14 waliokolewa huku hadi jana saa mbili usiku abiria saba walikuwa wakihofiwa kufa maji huku mwili wa abiria mmoja wa kike ulipatikana baadaye.
Hata hivyo, wakati taarifa ya Tasac ikieleza hivyo, Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere akizungumza mchana wa leo Jumanne amesema miili miwili imeopolewa kati ya saa 12 hadi saa mbili asubuhi ya leo huku kazi ya kutafuta miili mingine ikiendelea.
“Zoezi la utafutaji na uokozi wa miili bado linaendelea. Abiria ambao hawajapatikana ni wanaume watano na wanawake wawili ambao pia majina yao hayajajulikana,” inaeleza taarifa ya Tasac.
Kwa mujibu wa Tasac chanzo cha ajali ni boti hiyo ya uvuvi kubeba na kuzidisha abiria kinyume na sheria, hivyo kusababisha chombo kutoboka na kuanza kuingiza maji.
Kwa kuwa hakikuwa ni chombo cha abiria hapakuwa na vifaa uokozi hali iliyosababisha abiria kuzama ziwani.
Kutokana na ajali hiyo, shirika linasisitiza umma juu ya uzingatiwaji wa Tangazo Namba 274 la Mwaka 2024 (Merchant Shipping Notice No. 274) likiwa na maelezo ya usalama kwa wamiliki wa vyombo vidogo.
“Waendesha vyombo vidogo na abiria wakiwamo wananchi, wahakikishe wanatumia vyombo vilivyosajiliwa kubeba abiria, kuwa na vifaa vya uokozi ndani ya chombo, kujiepusha kusafiri usiku na vyombo vidogo.
“Na wamiliki wa vyombo vya uvuvi wajiepushe na tamaa ya kubeba abiria kinyume na sheria na taratibu, hivyo kuhatarisha maisha ya watu. Hatua kali dhidi wa wamiliki wa vyombo hivyo zitachukuliwa,” limesisitiza shirika hilo.
Aidha, limesema kwa kushirikiana na mamlaka nyingine linaendelea na zoezi za utafutaji na uokozi wa abiria waliosalia, baadaye hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi mmiliki wa chombo hicho cha usafiri kwa kukiuka Tangazo Namba 274.
Hata hivyo, kazi ya kutafuta miili ya watu hao waliotoka kusherehekea harusi ilipata changamoto kwa muda kutokana na hali mbaya ya ziwa na waokoaji wakashindwa kuona ndani hapo jana.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Vicent Naano amesema kazi ya utafutaji wa miili mingine bado inaendelea kwa kushirikisha wenyeji wa maeneo hayo pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.