NEMC YAPIGA KAMBI KANDA YA ZIWA, ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA ZEBAKI YATOLEWA .

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Afisa madini Mkazi Mkoa wa Mwanza wametoa elimu ya matumizi sahihi ya zebaki kwa wachimbaji kutoka mgodi wa Chata, Shokeraera, Shilalo na luhala zilizopo Wilaya ya Misungwi Mkoa wa Mwanza

Akitoa elimu hiyo iliyohusisha matumizi salama ya zebaki kwa wachimbaji, Bw.Musa Kazumila Meneja wa usajili wa kemikali na maabara za kemia, kutoka ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali amesema ni kufuatia mkataba wa Minamata(Minamata convention) unaotaka kutekeleza matakwa yake ambapo moja likiwa la kudhibiti matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo.

Amesema katika mradi huu unaofadhiliwa na Bank ya Dunia na kuratibiwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mkemia Mkuu amepewa jukumu la kutoa elimu ya usimamizi salama pamoja na matumizi salama ya zebaki kwani ndiye anayesimamia utekelezaji wa Sheria Na.3 ya mwaka 2003 inayohusu usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani ikiwemo zebaki.

Aidha amefafanua kuwa lengo la utoaji wa elimu hii pia ni kuwajengea uwezo wa uelewa kwa wachimbaji na watumiaji wa zebaki ili waweze kutambua jinsi zebaki inavyoingia mwilini, madhara yake namna ya kujikinga.

Naye Bw. Dereki Masako kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dodoma alipozungumza aliainisha maeneo ambapo madhara ya zebaki yanatokea kuwa ni wakati wa usagaji wa mawe na kudondosha matope ili zebaki ikamate na wakati wa uchukuaji wa kusanyiko anapokamua na kitambaa kwani matone hudondoka chini na kusambaa ardhini na hewani na kuleta madhara.

Amesema ni vema wachimbaji wakatumia vifaa Kinga ili kujilinda dhidi ya athari za zebaki na kubainisha madhara yake kuwa ni kuharibu mfumo wa fahamu na kuleta athari ya kushindwa kuhisi, kukakamaa kwa mwili, macho kuharibika na Figo.

Kwa mama wajawazito huathiri ukuaji wa mtoto kwa sumu kupita kwenye kondo la mama, kupoteza nguvu za kiume kwa wanaume, msongo wa mawazo na mwili kuwasha na kupungua.

Naye katibu wa Chama cha wachimbaji wadogo Wilaya ya Misungwi alipozumngumza alikiri kutokuwa na uelewa wa madhara ya zebaki na amedurahishwa na elimu hii kwani wengi wao wamekuwa wakijishughulisha na uchimbaji wa dhahabu bila kuzingatia madhara ya kiafya yanayoweza kutokea.






Related Posts