Mwanga. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeungana na makundi mbalimbali ya Watanzania kulaani matukio ya mauaji na utekaji yaliyotokea nchini, huku likiitisha maombi maalumu ya kuondokana na hali hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa leo Jumanne Septemba 17, 2024 wakati akitoa salamu za kanisa katika ibada ya maziko ya aliyekuwa Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Mwanga, Chediel Sendoro.
Ibada hiyo imefanyika katika Kanisa Kuu la Mwanga mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali, wakiongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko.
Askofu Sendoro alifariki dunia Septemba 9, 2024 kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro, baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani kwake Mwanga kugongana uso kwa uso na lori.
Jana, Septemba 16, 2024, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kupitia kwa Katibu Mkuu wa baraza hilo, Alhaji Nuhu Mruma alisema baraza hilo linaungana na Rais Samia Suluhu Hassan kulaani vitendo hivyo na wanavitaka vyombo vya ulinzi na usalama vifanye uchunguzi huru kubaini waliohusika na matukio hayo.
Septemba 15, 2024, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), pia, lililaani matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea nchini na kuvitaka vyombo vya dola kutimiza wajibu wao ipasavyo, ili kurudisha heshima ya Tanzania iliyozoeleka ya kuwa ni kisiwa cha amani.
Akizungumza leo kwenye mazishi ya Askofu Sendoro, Askofu Malasusa amesema kumekuwa na matukio ambayo hayakuzoeleka nchini ya watu kutoweka au kutekwa, hivyo amewataka waumini kusema ifike mwisho, kanisa liombe kwa ajili ya jambo hilo.
“Nchi inalaaniwa damu inapomwagika, hatutaki laana hii iingie katika nchi yetu. Tuombe kila mwenye kujua maana ya maombi kuliombea jambo hili, najua wanasiasa wamekuwa wakilizungumza, lakini hebu tulisogeze pia hili kama haja zetu mbele ya Mungu.
“Nachukua fursa hii kuomba Jumapili zijazo, wachungaji, maaskofu katika kanisa letu, tuanze kuomba kama kitu cha pekee kilichotokea katika nchi yetu,” amesema Askofu Malasusa wakati wa ibada hiyo.
Ameongeza kuwa wanasiasa waruhusu kuwepo na meza ya majadiliano, huenda kukawa na suluhisho la mauaji hayo, ametaka uwekwe muda wa kusikilizana ili kutafuta suluhisho la pamoja katika jambo hilo.
Awali akihubiri kwenye ibada hiyo, Askofu Malasusa amewataka waombolezaji, wachungaji na maaskofu kutumia kifo cha Askofu Sendoro kama funzo la kujiandaa hapa duniani, ili siku ya kuitwa waache ushuhuda.
“Nilimbariki Sendoro kuwa mchungaji na wenzake wanne, sasa wamebaki wawili, Mungu amenipenda kwa kunipa mchungaji ambaye hata sasa yapo ya kushuhudia. Niombe msiba huu usipite hivihivi, uwe funzo kwetu, wachungaji ninawaomba haya shime tutengeneze maisha yetu hapa duniani, ili siku tutakapoitwa tuwe na kitu ambacho tumeacha,” amesema.
Akitoa salamu za Serikali kwenye ibada hiyo, Dk Biteko amesema suala la utekaji na mauaji yanayoendelea nchini, tayari Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo ya uchunguzi kufanyika kwa haraka.
Amesema suala la watu kuzungumza naye anakubaliana nalo kwa kuwa suala linalohusu uhai wa mtu halihitaji mzaha hata kidogo.
“Niombe Askofu tuendelee kuliombea kanisa kama ulivyosema, tuiombee nchi yetu, Rais yeye mwenyewe anategemea kanisa, anawategemea Watanzania wote katika kuiendesha nchi hii.”
“Hata hili ulilolizungumza, yeye mwenyewe alishatoa maelekezo ya uchunguzi kufanyika haraka iwezekanavyo na ndani ya chama chetu tayari tumeshazungumza na Watanzania wanaendelea kuzungumza.
“Hili ulilolisema watu tuzungumze nakubaliana na wewe, kwamba katika Taifa la watu wote hawa, kitu pekee ambacho kinaweza kutuweka pamoja ni kuzungumza matatizo yaliyopo ili tuyatafutie suluhu kwa pamoja,” amesema Dk Biteko.
Amesema: “Unapokuja wakati wa uhai wa mtu ni jambo ambalo halihitaji kuwa na mzaha hata kidogo, ni jambo linalohitaji kila mmoja alizungumze kwa mzigo anaodhani atakuwa amesema kwa namna inavyofaa na yeyote anayesema asionekane kuwa mtu mbaya kwa sababu wote tunakusudia kuijenga nchi yetu.”
Akimzungumzia Askofu Sendoro, Dk Biteko amesema alikuwa kiongozi mwema na mzalendo na kuwataka wanaMwanga na waombolezaji wote waliofika, kuenzi yote mazuri aliyoyafanya enzi za uhai wake.
“Nilikuwa nafuatilia mahubiri yake, mara zote aliyapambania maadili yetu, tuendelee kuyalinda kwa wivu mkubwa, tusiruhusu tamaduni nyingine za nje zije hapa zitugawanye kwa namna yoyote ile, alikuwa akihubiri umoja wetu, Utanzania wetu, bila kujali dini zetu wala makabila yetu mahali tunapotoka,” ameongeza.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya amewapa mzigo viongozi wa dayosisi hiyo na kanisa kuhakikisha wanatafuta mtu anayeweza kuvaa viatu vya Askofu Sendoro.
“Askofu Sendoro amefanya mengi na makubwa Mwanga, pamoja na kazi kubwa aliyofanya, sasa ni lazima tujipange tupate uongozi unaoweza kuvaa viatu vyake, kwani alikuwa kijana, mtu mwenye ari kubwa ya kazi, nilikuwa sijaona maaskofu wanapita usiku wanatembea ikiwa kuna jambo ameona ni lazima lishughulikiwe na alitaka kutafsiri maneno kwa vitendo.
“Niombe wale watakaohusika kutafuta mbadala wake, watupatie mtu ambaye yale yote aliyoanzisha yataendelea, atakayewasha moto kama alivyouwasha, atatuunganisha kama alivyotuunganisha wananchi wote na Wakristo hapa Mwanga, atatuunganisha dayosisi ya Mwanga na dayosisi nyingine ndani na nje ya Tanzania. Tafuteni mtu anayeweza kuvaa viatu vya Askofu Sendoro,” amesema.
Mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo amesema kifo cha Askofu Sendoro ni pigo katika wilaya hiyo kwa kuwa alikuwa kiongozi aliyehusika na changamoto za jamii na hata kulipotokea migogoro, walimkimbilia na alitafuta suluhisho la mgogoro huo.