Chadema kuwachuja wagombea 79, waeleza matarajio

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeanza kufanya usaili kwa watia nia wanaomba kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi mbalimbali kwa kanda tatu.

Jumla ya watia nia 79 kutoka kanda za Pwani, Kusini na Pemba kwa nafasi ya uenyekiti, makamu na Mweka Hazina katika ngazi za kichama na mabaraza (wazee, wanawake na vijana) wanafanyiwa mchujo huo na baada ya kuisha yatatangazwa majina ya wale watakaopenya kuwa wagombea na tarehe ya uchaguzi.

Kamati kuu hiyo inaendelea na kikao chake leo Jumanne, Septemba 17, 2024 makao makuu ya Chadema, yaliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mchakato huo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema wanajadili uteuzi wa wagombea wa Kanda ya Pwani inayoundwa na mikoa miwili Dar es Salaam na Pwani.

“Kanda ya Kusini inayoundwa na mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara na Kanda ya Pemba yenye mikoa ya Kaskazini Pemba na Kusini Pemba kisha tutateua baada ya mchujo kwa wanachama 79 waliojitokeza kuomba nafasi,” amesema.

Amesema baada ya mchakato huo kuisha, kamati kuu hiyo itatangaza siku ya kufanyika uchaguzi huo utakaohusisha wagombea watakaokuwa wamepenya katika mchujo huo.

“Mchakato huu wa usaili tunatarajia kukamilika leo kwa sababu wamejipanga vizuri kuhakikisha tunamaliza kwa wakati na baada ya hapo tutoa ratiba inayofuata ikiwemo ya kufanyika uchaguzi,” amesema.

Amesema katika mchakato huo wameanza kuwasikiliza na kuwauliza maswali watia nia wa nafasi kwenye mabaraza ya chama hicho kwa ngazi ya kanda hizo kabla ya kuanza na wanaogombea upande wa chama.

Kwa uchache wanaowania nafasi ya Mwenyekiti na Makamu wake, Pwani ni Boniface Jacob na Gervas Lyenda wakati upande wa Makamu Mwenyekiti ni Shekh Ally Mohamed ‘Kadogoo’ na Baraka Musa.

Kusini nafasi uenyekiti wako watia nia watatu Aden Mayala, Nicholauss Mapunda na Dk Mahadhi Mmoto, kwa makamu ni Belchomas Ponera, Kastor Mmuni na Shaban Mbaruku.

Pemba ni Omar Othman Nassor, Nuhu Jafar Khahamis huku upande wa Makamu ni Time Ali Suleiman na Rukia Abuu Mohammed

Walioanza kutoka katika Usaili

Baadhi ya wajumbe walitoka katika usaili huo, akiwamo Joyce Mwabamba aliyetia nia nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Kanda ya Pwani amesema usaili umezingatia haki huku akieleza amehojiwa kwa kuulizwa maswali ya kawaida.

“Nilihojiwa maswali mengi lakini moja ya swali nililoulizwa iwapo nikibahitika kupata nafasi niliyoomba nini malengo yangu kwa chama nikajibu; na matumaini yangu yote nilijibu kwa ufasaha,” amesema

Mwabamba amesema iwapo atateuliwa kuwa mgombea, akishinda ataanza kushughulika na changamoto ya watu kuwa waoga kujiunga na chama kutokana na aina ya matukio yanayojitokeza.

“Nitajituma na kukabiliana na hali ya kiuchumi kwa kulifanya baraza linakuwa na vyanzo vya uhakika vya kifedha. Ili kuongeza morali na kuunganisha wanawake wote ndani ya kanda ya Pwani,” amesema.

Naye, mtia nia nafasi ya Mweka Hazina Bawacha, Pwani Grace Mgonjo amesema dhamira yake ni kutoa mchango wake katika nafasi hiyo.

“Naamini natosha kushika nafasi hii na nitawatumikia wanawake kwa uadilifu mkubwa,” amesema.

Akizungumzia usaili Mgonjo ambaye ni mke wa Joseph Haule ‘Profesa Jay amesema ulikuwa mzuri kwa sababu aliulizwa maswali mengi lakini aliyajibu kwa ufasaha kwa kuwa yalikuwa ndani ya uwezo wake.

“Siwezi kukutajia ni maswali gani niliulizwa kwa sababu yalikuwa mengi. Nikichaguliwa naenda kuinua Bawacha iwe na nguvu na kufanya shughuli zake bila kutegemea msaada kutoka sehemu zingine,” amesema.

Related Posts