Dar/Mbeya. Madhara ya mvua yameendelea kuleta adha kwa makazi ya wananchi, huku baadhi ya wakiiomba Serikali kuwahamishia katika maeneo salama.
Wakati hayo yakiendelea, wataalamu wa maji na uhandisi wa ujenzi wameeleza sababu za madhara ya maji ya ardhini na njia sahihi za ujenzi unaoweza kuhimili kishindo cha wingi wa maji.
Licha ya mvua kukatika tangu Jumamosi Aprili 26, 2024, bado maji yameendelea kuibuka na kusababisha mashaka kwenye makazi ya watu.
Wakizungumza leo Mei Mosi, 2024 na Mwananchi Digital, baadhi ya wakazi wa Mbagala kwa Mwanamtoti walisema nyumba zao zimekuwa zikipasuka na kuanguka.
Mkazi wa eneo hilo, Simon Milanzi amesema hali si nzuri katika eneo hilo, licha ya mvua kukatika lakini kumekuwa na changamoto ya maporomoko ya ardhi yanayoathiri nyumba zao.
“Ardhi katika eneo hili si rafiki, kuna nyumba hapa imeanguka jana bila mvua kunyesha kutokana na maporomoko ya udongo, hali hii inatishia nyumba zingine zilizopo katika maeneo haya kutokuwa salama,” amesema.
“Eneo tunaloishi limepimwa na Serikali na tunalipa kodi, tumewaita wanahabari kwa sababu tunaona hali si nzuri, licha ya mvua kukata lakini tunaishi kwa hofu ya mmomonyoko wa udongo,” amesema Milanzi.
Amesema mvua iliyonyesha hivi karibuni imekuwa kama kichocheo cha ardhi kumomonyoka zaidi, ndiyo maana baadhi ya kaya zinahama siku hadi siku ili kuokoa maisha.
“Kwa hali iliyopo hapa Mwanamtoti hakuna tofauti sana na tukio lililotokea kule Hanang’ mkoani Manyara, maana ardhi inamomonyoka haipo salama,” amesema Milanzi.
Milanzi ameiomba Serikali kwenda kufanya tathmini katika eneo hilo ili kujua kama kuna umuhimu wa watu kuendelea kubaki au wahamishwe na kupelekwa sehemu salama zaidi.
Regina John, ameiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la tatu, akisema hali si nzuri katika maeneo wanayoishi kutokana na tishio la mmomonyoko wa udongo ambalo linaendelea kutokea.
“Nyumba imeondoka, tangi moja la maji limeondoka kutokana na mmomonyoko wa udongo, Serikali itusaidie kama wanataka kulichukua eneo hili sawa na kutupeleka eneo jingine sawa,” amesema Regina.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mwanamtoti, Halima Songoro amesema hali si nzuri kwa wananchi wa mtaa huo, akieleza nyumba sita zimepata madhara kutokana na tukio hilo.
“Msaada unatakiwa kwa wananchi, maana udongo unaporomoka, kuna wananchi wengine wameyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wao, nyumba hazikudondoka wakati mvua ikinyesha bali zilivyokata mmomonyoko ukaanza kutokea,” amesema Songoro.
Kutokana na mvua zilizonyesha na kusababisha maafa maeneo mbalimbali nchini, wataalamu wameeleza sababu za mafuriko na maporomoko, wakishauri hatua za kufanya ili kuondokana na changamoto hizo.
Miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na majanga hayo hadi kusababisha vifo, majeruhi na kufukiwa kwa nyumba, huku mifugo na mali zikisombwa na maji ni Manyara, Mbeya, Kagera, Morogoro na Geita.
Mhandisi wa maji, Petro Ndolezi amesema kuna maeneo maji chini ya ardhi yanakutana na ya mvua baada ya kunyesha na huchukua muda mrefu kutoweka.
Hata hivyo, Ndolezi amesema si maeneo yote yanaweza kuwa na maji yanayopanda juu kulingana na jiografia.
“Water table (mpaka wa maji ya ardhini) inatofautiana kutokana na hali za kijiografia na muundo wa ardhi wa eneo husika. Kuna mahali ambapo water table inakutana na maji ya juu ya ardhi, yaani mvua ikinyesha sana, maji yanakutana na ya chini, sasa maeneo hayo maji yanaweza kukaa muda mrefu bila kukauka,” amesema.
Hata hivyo, amesema yapo maeneo ambayo water table iko mbali, hivyo mvua ikinyesha maji hukauka haraka.
Mhandisi wa Jiji la Mbeya, Mozea Deusidedit amesema sababu ya maporomoko ni janga la asili, japokuwa linaweza kudhibitiwa kwa kujengewa mimea inayoweza kupunguza tatizo.
Amesema changamoto za mafuriko au maporomoko inasababishwa na tabianchi na mvua ambazo husababisha udongo kufyonzwa na kinachohitajika ni kupanda miti.
“Tunachoshauri, wananchi waondoke katika maeneo yenye tatizo, ujenzi wowote lazima uzingatie usalama wa maisha ya mtu bila kusubiri athari kama hizo kujitokeza.
“Ndiyo maana kwa sasa hatuwezi kupima viwanja katika maeneo yenye milima, lakini kuzuia ujenzi ambao haukidhi mahitaji na ikibainika tunazuia muhusika akigoma hatua kali zinachukuliwa,” amesema Deusidedit.
Mtaalamu wa ujenzi, Mhandisi Hamis Manyaje, amesema mafuriko hutokea maeneo ya mijini kwa sababu ya wingi wa nyumba zinazosongana na kuficha eneo kubwa la ardhi na kusababisha maji kukosa pa kwenda.
Mayanje amesema ujenzi holela ni sababu nyingine inayosababisha mafuriko, akieleza kuwa maji hufuata mkondo wake, hivyo wananchi lazima wajiridhishe na maeneo ya makazi kabla ya kuanza ujenzi.
“Wananchi wapewe elimu, japokuwa baadhi yao ni wagumu lazima waelewe kwamba maporomoko ni janga la asili kuliko mafuriko ambayo husababishwa na binadamu wenyewe,” amesema mtaalamu huyo.
Kwa upande wake mtaalamu wa majengo Jiji la Mbeya, Yunusi Nsegobya amesema sababu za maporomoko sehemu za milima ni shughuli za binadamu akitolea mfano Kawetere kuwa watu walikata miti.
Amesema hatua ya kukata miti ilisababisha udongo kupata uzito uliotokana na unyevu na kuvutwa na nguvu ya uvutano.
“Ili kuondokana na maporomoko kama hayo, ipandwe miti kulinda mlima, lakini shughuli za binadamu zisiendelee wala kujengwa nyumba vinginevyo maafa yatakuwa makubwa zaidi,” amesema Nsegobya.
Mhandisi wa majengo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, (MUST), Dk Gislar Kifanyi, amesema maporomoko huletwa na uharibifu wa uoto wa asili, akisema inashauriwa kabla ya kujenga makazi udongo upimwe na kufanyiwa utafiti.
Mambo ya kuzingatia wakati wa ujenzi
Mtaalamu mwingine wa ujenzi, Mhandisi Goliath Mfalamagoha, ameshauri kabla ya kuanza kwa ujenzi wahusika watafute mtaalamu wa majengo, msanifu au mbunifu majengo ili kujengewa uelewa wa kisayansi.
“Kuna changamoto kubwa inayozikabili nyumba nyingi hasa zilizojengwa kwenye maeneo ambayo kina cha maji hakiko mbali sana chini ardhini, ni tatizo ambalo limekuwa sugu na kuharibu rangi ya nyumba kuanzia chini kupanda juu.
“Sababu kubwa ya changamoto hii ni ufundi wa mwanzo kutozingatia hatari hii na hivyo kutoweka karatasi pana la chini kabla ya kumwaga zege la sakafu ya chini,” amesema.
Ameongeza: “Kwa mahali ambapo nyumba ilishajengwa na madhara yameanza kuonekana, suluhisho la changamoto hii ni kufanya ukarabati wa nyumba nzima kuziba yale maeneo yanayopandisha unyevu kwa kutumia vipande vya karatasi, zulia la plastiki kuzunguka nyumba nzima.”