Arusha. “Anayehitajika kuwajibika ni uongozi wa shule, wao ni wazembe. Ninamtaka mtoto wangu akiwa hai, siyo kwamba tunashidwa kukaa naye nyumbani, tumewaletea watoto wetu muwatunze, hatudaiwi chochote.
“Halafu unaniambia mnampeleka safari haonekani, hapana haiwezekani, hata jana (Septemba 16) mbele ya Ofisa wa Upelelezi nimewaambia nahitaji mtoto wangu akiwa hai, kama hawana ulinzi, ni nini walienda kujifunza huko mlimani?”
Ni kauli ya Johannes Mariki, mzazi wa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bagara, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara, Joel Johannes (14) anayedaiwa kupotea tangu Septemba 14, 2024 katika Mlima Kwaraa walikokwenda kwa ziara ya masomo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Simon Mdee amesema katika safari hiyo wanafunzi 103 walienda mlimani wakiwa na walimu wao na waongozaji wapanda mlima.
Amesema baada ya kushuka na kubainika kuwa Joel hayupo waongoza wapanda mlima walirudi mlimani kumtafuta hadi saa sita usiku bila mafaniko.
Amesema jitihada mbalimbali zinaendelea zikiongozwa na Jeshi la Polisi, halmashauri na kushirikisha jamii ya watu wanaoishi pembezoni mwa mlima huo.
Mdee amesema imeundwa timu, akiwamo Ofisa Elimu Sekondari, ambayo imeenda shuleni kuzungumza na marafiki wa Joel kupata taarifa zaidi.
“Pia tumeagiza Jeshi la Akiba linaenda kuungana na waliopo kufanya operesheni ya kumtafuta,” amesema.
Mariki akizungumza akiwa mlimani hapo leo Jumanne Septemba 17, 2024 wakati wa kumtafuta mwanaye amesema wanachohitaji ni mtoto wao akiwa hai.
Amesema Jumamosi Septemba 14, 2024 walipigiwa simu kuwa mtoto wao haonekani, hivyo waliwasiliana na baadhi ya ndugu zao na kwenda wilayani Babati kufuatilia alipo mtoto wao.
“Tulikuja tukaungana nao tukaondoka hadi mahali wanaita Chokaa, ni mbali tulipofika pale tukakuta Zimamoto wanarudi kutoka mlimani wanasema wamemtafuta kule hawajamuona nasi tukarudi,” amesema.
“Kuna kijana alisema kuna mama alikuwa anaokota kuni alidai kumuona kijana akishuka mlimani mwenyewe, akapigiwa simu akaenda kutuonyesha barabara aliyomuona akiwa amevaa sare za shule, tukamuonyesha picha akasema ndiye,” amesema.
“Jumatatu sisi tukaja shuleni tukaingia hamna mwalimu, nikampigia mkuu wa shule kuuliza kuhusu suala hili, tukamwambia kama hamna ushirikiano tunaenda kwa mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya. Tulipofika tukamkuta Katibu Tawala wa Wilaya ambaye aliwaita na tukatoa wote maelezo,” amesema.
Mariki amesema baada ya kuona hakuna watu wengi wa kuingia msituni, aliahidi kusaidia ili watu waongezeke kwa ajili ya kumtafuta ila mkuu wa upelelezi alimtaka asigharimie chochote na walikubaliana leo wakutane ili waende msituni kuendelea kumsaka.
“Tuko hapa wa kulaumu ni uongozi wa shule kwa sababu hata juzi niliwauliza ulinzi wao msituni ukoje, kawaida ulinzi unakuwa mbele, katikati na nyuma na wengine wenye silaha. Niliwaambia sitawaelewa nataka mtoto wangu akiwa hai,” amesema.
Amedai wiki mbili zilizopita baada ya kujulishwa na uongozi wa shule kuhusu safari hiyo alikataa mtoto wake asiende ila baadaye alilazimika kumruhusu baada ya mtoto kulalamika kuwa ni yeye pekee ambaye hajalipa kwa ajili ya safari hiyo.
“Tuko siku ya nne leo hii, hawajui gharama tunazotumia tumeacha shughuli zetu tunamtaka Joel wetu kwanza,” amesema.
Mama wa mtoto huyo, Germana Wilbard amedai alipigiwa simu na mwalimu aliyemuomba namba za shangazi wa Joel anayeishi Babati na alipouliza kuna shida gani alijibiwa hakuna ila baada ya shangazi huyo kutokupokea, walijulishwa mtoto wao amepotea.
“Nilivyoongea na wenzake wanasema walikuwa makundi mawili na walipofika kwenye kilele cha mlima, walipokuwa wakirudi wengine walipotea akiwemo Joel, walienda njia isiyotoka, wakarudi ila mwanangu hajarudi hadi sasa,” amesema.