Dk Chami azikwa kijijini kwao Urori, Hai

Moshi. Vilio na simanzi vimetawala kwenye mazishi ya Dk Dismas Chami (32) ambaye amezikwa leo Septemba 17, 2024 kwenye makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Urori, Kata ya Machame Narumu, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Mwili wa Dk Chami, ambaye ni daktari wa Kituo cha Afya cha Ulyankulu, ulipatikana Septemba 13, 2024 baada ya kutoweka nyumbani kwake kwa zaidi ya siku 11.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi mwili wake ulikutwa eneo la Kombo Masai, Kata ya Malolo mkoani Tabora.

Akitoa mahubiri kwenye ibada ya mazishi yaliyofanyika nyumbani kwa wazazi wake, Askofu wa Kanisa la Yesu ni Lango la Uzima, Askofu  Shukuru Mongela amesema kifo cha Dk Chami kiwe ni fundisho kwa kila mwanajamii kuonyeshana upendo  na kuachana na mambo maovu ambayo yamekuwa yakigharimu maisha ya watu.

Amewataka wanajamii kutengeneza maisha yao na Mungu ili siku atakapoondoka hapa duniani akumbukwe kwa mazuri yake aliyoyaacha hapa duniani.

“Duniani hapa hatuishi milele, tuishi vizuri na jirani tutengeneza maisha yetu na Mungu, maisha yako ni ya thamani ukiwa hai hapa duniani. Hivyo, kama umepanda mahindi, utavua mahindi, kama umelima migomba, utavuna migomba. Ni wakati sasa kila mmoja wetu ajitafakari kwamba siku ukiondoka hapa duniani utakuwa umeacha nini au utakumbukwa kwa lipi,” amesema askofu huyo.

Pamoja na mambo mengine, ameitaka jamii kuacha ulevi, mauaji ya kukusudia ambayo yameendelea kutokea duniani, hivyo akawataka wanajamii kumwomba Mungu ili maovu yanayoendelea yaweze kukoma.

Akisoma historia ya marehemu, Kanek Simbo amesema ndugu yao alitoweka nyumbani kwao Septemba 2, 2024, juhudi za kumtafuta kupitia Jeshi la Polisi, wafanyakazi wenzake zilifanyika hadi hapo mwili wake ulipookotwa Septemba 13, 2024 katika pori la Malolo mkoani Tabora.

“Dk Dismas Chami aliondoka nyumbani Septemba 2, 2024, juhudi za kumtafuta zilifanywa na Jeshi la Polisi, familia na wafanyakazi wenzake na hatimaye mwili ulipatikana katika Pori la Malolo, Tabora Septemba 13, 2024,” amesema Simbo.

Amesema uchunguzi wa kifo cha Dk Chami hadi sasa unaendelea na kwamba wameliachia Jeshi la Polisi.

Simbo amesema Dk Chami aliajiriwa mwaka 2017 katika Kituo cha Afya cha Igwisi, Kaliua na alihamishiwa  kituo cha afya  Ulyankulu, Mkoani Tabora hadi umauti ulipomkuta.

Amesema Dk Chami, ameacha mke na mtoto mmoja mdogo wa kike.

Akimzungumzia Dk Chami, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkindo, Tomson Banigo kutoka Tabora, amesema Dk Chami atakumbukwa kwa ushirikiano wake kwa jamii na kwamba kifo chake kimewahuzinisha.

“Dk Dismas alikuwa ni jirani yangu, kwa kweli kifo chake kimetukosesha amani kwakuwa alikuwa ni mtu wa watu, muda wowote akihitajika kutoa huduma kwa jamii alikuwa anajitahidi, tutamkumbuka sana,” amesema Binigo.

Related Posts