Madaktari watoa neno matumizi ya vilainishi kwa wanawake

Dar es Salaam. Kama ni mtumaji wa mitandao ya kijamii hususan Instagram, utakubaliana na mimi juu ya ongezeko la watu wanaouza vilaini (lubricant) kwa ajili ya kusaidia wanawake wasipate michubuko wakati wa tendo la ndoa.

Kila mmoja akiuza bidhaa ya aina yake, njia tofauti zimekuwa zikitumika katika kuwashawishi wateja kununua vilainishi hivyo, ili waepuke maambukizi, michubuko wanayoweza kupata wanapokutana na wenza wao.

Licha ya faida yake kutajwa na kuonekana kweli inaweza kusaidia, watalaamu wa afya wanapinga suala hilo, wakitaka wanawake kuacha kununua holela vilainishi hivyo na kuvitumia na badala yake wafike hospitalini kwa ajili ya vipimo ili wasaidiwe.

Hiyo ni kutokana na kile walichoeleza kuwa, uke wa mwanamke kuwa mkavu hauwezi kutibiwa kwa kutumia vilainishi vinavyouzwa holela, badala yake ni vyema kujua sababu za kukosa ute asili ili kama kuna tatizo atibiwe.

Wataalamu wamesema hayo walipozungumza na Mwananchi, huku wakionyesha wasiwasi hasa wafanyabiashara wasiokuwa wataalamu wa dawa wanapokuwa vinara kuuza bidhaa hiyo.

Mwananchi imebaini kupitia mtandao wa Instagram vilaini hivyo huuzwa kuanzia Sh15,000 na kuendelea.

“Ukinunua hii, uke unakuwa umeloana, ile michubuko tena utaisikia kwa wengine, maumivu, maambukizi wewe unakuwa hauna wasiwasi kabisa,” amesema mmoja wa wauzaji anayepatikana Makumbusho alipozungumza na Mwananchi.

Kwa mujibu wa muuzaji, bidhaa yake anainadi kuwa ni asili na haina madhara yoyote pindi mtu anapoitumia huku akielekeza kuwa mwanamke anatakiwa kujidondoshea matone mawili ya kilainishi hicho kilicho katika mfumo wa kimiminika dakika 10 kabla ya tendo la ndoa.

Wakati yeye akisema hayo, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk Isaya Mhando amesema watu wanapaswa kutambua kuwa kila kinachowekwa kwa ajili ya kutibu huwa kina athari zake hasi.

Amesema kwa kawaida sehemu za kike kuingizwa vidole, maji na hata vinginevyo husababisha maambukizi mengine ikiwamo ya bakteria wanaotoka nje.

Pia, amesema kila dawa inapotengenezwa, huwa inawekwa maelekezo juu ya namna inavyopaswa kutumika na inaweza kuwa na matokeo gani hasi.

“Sasa katika kutumia dawa hizi kuna wengine miili yao italazimika kupambana ili kujilinda, wengine zitawakataa na wanaweza kupata maambukizi ya magonjwa mengine,” amesema Dk Mhando.

Amesema badala ya kukimbilia katika vilainishi ni vyema wanawake wakaonana na watalaamu wa afya, kwani vipo vitu vinavyoweza kuwa sababu ya yeye kupoteza ute wa asili ikiwamo maambukizi ya magonjwa mbalimbali, mabadiliko ya homoni na msongo wa mawazo.

Maneno yake yanaungwa mkono na daktari bingwa wa kinamama, Cyrill Masawe anayewataka wanawake kujenga tabia ya kwenda hospitali wanapokuwa na matatizo badala ya kununua vilainishi holela.

“Akionana na daktari atamshauri atumie nini, kama ni kilainishi cha aina gani au anatakiwa matibabu si tu kuanza kutumia vilainishi,” amesema Dk Massawe.

Amesema wakati mwingine badala ya kujitibu, watu wamekuwa wakiingiza magonjwa kutoka nje kwenda ndani.

Amesema ukavu wa uke huweza kuchochewa na maambukizi ya magonjwa mbalimbali, umri mkubwa, mazingira yasiyo rafiki kwa mwanamke.

Mtaalamu wa fiziolojia ya homoni na mazoezi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki cha Sayansi Muhimbili (MUHAS), Fredrick Mashili amesema licha ya tatizo hilo kuwakumba zaidi wanawake, limekuwa likiwapata pia wanaume na ndiyo chanzo cha wengi kukosa nguvu za kiume.

Amesema mvurugiko wa homoni husababishwa na mambo mengi huku msongo wa mawazo ukitajwa kuwa chanzo kikuu za kuruga homoni katika mwili wa binadamu.

Amesema wanawake wamekuwa wakikumbwa na tatizo la ukavu wakati wa tendo na wakati mwingine kukosa kabisa hamu, hiyo husababishwa na kutozalishwa kwa ute.

“Ute kwenye mzunguko wa mwanamke, utengenezwaji wake na mabadiliko yaliyopo kwenye uke asilimia 99 yanafanywa na homoni, kwa sababu katika mzunguko wa mwanamke ule ute unabadilika badilika kwa kiasi na kiwango jinsi ulivyo hiyo yote hutokana na homoni.

“Mzunguko huo unaweza kubadilishwa na msongo wa mawazo unabadilisha vipi kwa sababu za kisaikolojia inaingia kwenye ubongo inafanya mabadiliko yanayobadilisha utengenezwaji wa homoni,” amesema.

Dk Mashili ambaye pia ni daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni amesema iwapo msongo wa mawazo utaathiri homoni zinazohusika na kazi hiyo kuna uwezekano wa kupungua kwa kasi ya utengenezwaji ute na hii itachangia kwa kiasi kikubwa kutokuwepo na ute.

“Stress ina nafasi kubwa sana mwanamke anaweza akawa na mawazo kuhusu kazi, watoto, pesa chochote kile kinacholeta msongo kwa kiasi kikubwa kinaweza kuathiri mfumo wa homoni na msongo wa mawazo kitu kikubwa kinachoathirika ni homoni,” amesema.

Hata hivyo, Dk Mashili amesema homoni ya estrogen inayochagiza hamu ya tendo huanza kutengenezwa kwa mwanamke kati ya miaka 14 mpaka 15 na huanza kuisha kipindi cha kukoma kwa hedhi au ‘menopause’ kati ya miaka 45 mpaka 55.

Mbali na maambukizi ambayo yametajwa na wataalamu hao, tovuti za afya za nchi tofauti zinaeleza kuwapo kwa faida na hasara za matumizi yake.

Tovuti ya Women’s Voice for the Earth inaeleza kuwa baadhi ya vilainishi huweza kuwa na aina ya viambata vinavyoweza kusababisha magonjwa sugu na ya muda mrefu, ikiwamo saratani na wakati mwingine matatizo katika uzazi.

Kuhusu uzazi, Tovuti ya Sukhamlife inaeleza kuwa si vilainishi vyote ni salama baadhi huweza kuathiri uwezo wa mbegu kuogelea na kulifikia yai kwa ajili ya kulirutubisha jambo linaloweza kuwafanya kuhangaika kupata watoto.

Haya yanasemwa wakati ambao takwimu zinaonyesha kuwa katika kila wagonjwa 100 wanaougua saratani nchini, 23 kati yao wanaumwa mlango wa kizazi.

Pia, haya yanasemwa wakati ambao takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya nne kwa kuwa na wagonjwa wengi wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi ikitanguliwa na Eswatini, Zambia na Malawi.

Badala ya kukimbilia vilainishi, wataalamu wanashauri njia za asili kutumiwam ikiwemo mwanamke kuandaliwa ipasavyo kabla ya tendo la ndoa, kuhakikisha kuwa yuko sawa kisaikolojia ili awe huru kukutana na mwenzake.

Kufanya, hivyo ndiyo kutamfanya kuwa na uwezo wa kuzalisha ute wake mwenyewe na kuondoa ulazima wa matumizi ya vilainishi vya kutengeneza.

Dk Mashili naye ameonya kuwa ni vyema matibabu yake yasikimbilie kwenye kutumia dawa, bali yakimbilie kwanza kwenye msaada wa kisailokolojia.

“Hapa matibabu yake ni kutafuta namna ya kupambana na hilo tatizo kwa kuliondoa kwa kutumia wataalamu ambao watakupa tiba kulingana na vipimo kwa kiasi kikubwa inaweza kubadilisha kiwango cha homoni, kubadilisha ute na vitu vingine vyote na mambo mengi ambayo kikubwa yanakuwa yanaendeshwa na homoni,” amesema Dk Mashili.

Mtaalamu wa afya ya akili na mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Mental Health Tanzania, Semeni Lukaga amesema matatizo kwa binadamu yeyote yanaenda kuathiri mwili kibaolojia.

Ametolea mfano mwanamke mwenye madeni mengi hasa ya vikoba ambaye hajui wapi atapata fedha, akisema wengi wanapata msongo wa mawazo ambao huwa chanzo cha kukosa hamu ya tendo.

“Kaenda kwenye vikoba kakutwa na hayo matatizo, cha kwanza kitaalamu mwili huwa unapokea matatizo kwa maana kuna ubongo unaotema zile sumu, kama ana hasira ina maana zile hasira kuna homoni za sumu ambazo zitatemwa na ubongo zitasambaa kwenye mwili kwa kupitia mfumo wa neva.

“Kama ni msongo wa mawazo utatembea kwenye mwili utasababisha hamu ya kula kuisha, utasababisha msisimko kutotokea kwa kuwa misuli haiwezi kufanya kazi,  kwa hiyo muunganiko wa matatizo na kutofanya tendo la ndoa vizuri au kutokuwa katika emotional attention ya mapenzi ni kubwa sana kwa mwanamke ambaye ana matatizo,” amesema na kuongeza;

“Kwa sababu muda ambao kisaikolojia hata binadamu alivyo awe mwanamke au mwanaume linapoingia suala la hisia za kimapenzi, ubongo huwa hauhitaji nafasi nyingine hutakiwa utanuke uzibe ma-gape yote, sasa hawezi kufanya tendo la ndoa kama anawaza kuna deni anadaiwa au simu inaweza ikapigwa muda wowote au wadai wangu wanapajua nyumbani nina deni hili na lile hawezi ku-enjoy mahusiano.”

Tatizo la msongo wa mawazo likizidi husababisha sonona na baadaye tatizo la afya ya akili.

Related Posts