MWENGE WA UHURU KUPITIA MIRADI 28 YENYE THAMANI YA TRILIONI 8.5 KIBAHA

Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Mei 1

MWENGE wa Uhuru utapitia miradi 28 yenye thamani ya trilioni 8.5 wilayani Kibaha, mkoani Pwani, ambapo umekagua mradi mkubwa wa
Kongani ya Viwanda ya SINOTAN, Kata ya Kwala ambao hadi kukamilika utagharimu trilioni 8.4.

Aidha umeweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa barabara kutoka barabara ya Morogoro kwenda ofisi za Halmashauri, yenye urefu wa mita 300 kiwango cha lami , thamani mil490,018,125 fedha za ujenzi kutoka Serikali Kuu -Maendeleo ya Jimbo.

Akitoa taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava, Meneja wa TARURA wilayani Kibaha, Samwel Ndoveni alisema, mradi umetekelezwa na Mkandarasi M/S Globalink General Contractors Ltd.

Nae Mzava ameridhishwa na mradi huo wa barabara,na kusisitiza umuhimu wa manunuzi ya umma kutumia mfumo wa kidigital wa manunuzi ya umma Nest ambao unasimamiwa na mamlaka ya udhibiti ya manunuzi ya umma (PPRA).

Alieleza mfumo huo, unasaidia kuondoa tabia iliyokuwa ikijitokeza kipindi cha mfumo wa zamani TANREP.

Mzava alifafanua,mfumo huo umeondoa malalamiko ,na tabia za watu kukutana mezani na kupeana zabuni.

“Zamani tulikuwa na mfumo wa TANREP na sasa tuna mfumo wa NEST na waheshimiwa wabunge wametutungia sheria nzuri ya kusimamia mambo hayo na ndio maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ili kupunguza malalamiko na kuweka udhibiti katika matumizi ya umma “alisema Mzava.

Katika hatua nyingine, Mwenge wa Uhuru uliweka jiwe la uzinduzi wa mradi wa maji kijiji cha Ruvu Stesheni, kumtua mama ndoo kichwani ,mradi ambao unasimamiwa na Mamlaka ya maji safi Na mazingira Vijijini (RUWASA) .

Deborah Kanyika Meneja RUWASA Kibaha, alielezea chanzo cha mradi huo ni kisima chenye uwezo wa kutoa lita 11,820 kwa saa na kina urefu wa mita 43 , gharama za mradi 328,719,109.94 kupitia mfuko wa Taifa wa maji (NWF) .

Deborah alisema,kabla ya kujengwa mradi huo kaya 81 zilikuwa zinapata maji kwasasa kaya 164 zinakwenda kunufaika kati ya hizo 33 zimeunganishiwa maji nyumbani, mradi huo umesanifiwa kuweza kutoa huduma hadi kufikia kaya 520 ifikapo 2042.

Mwenge huo pia umekagua na kufungua mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na matundu matano ya vyoo shule ya msingi Kilangalanga na kituo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum shule ya msingi Mlandizi.

Awali akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Bagamoyo, Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Nikkison John alisema, Mwenge huo utapitia miradi 28 katika halmashauri ya Kibaha Mjini na Kibaha Vijijini ,yenye thamani ya trilioni 8.5.



Related Posts