Nani kuibuka na ushindi uchaguzi wa Rais Marekani?

Wapigakura nchini Marekani wataenda kupiga kura Novemba 5, mwaka huu, kumchagua Rais wao anayefuata.

Uchaguzi huu ulianza kama marudio ya uchaguzi wa mwaka 2020, lakini ulipinduliwa Julai wakati Rais Joe Biden alipojiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kumuunga mkono Makamu wa Rais, Kamala Harris.

Swali kuu sasa ni je, matokeo yataleta muhula wa pili wa Donald Trump au Rais wa kwanza mwanamke wa Marekani?

Kadiri siku ya uchaguzi inavyozidi kukaribia, Wamarekani na dunia kwa ujumla wanazidi tufuatilia kura za maoni na kuona jinsi kampeni inavyoathiri mbio za kuelekea Ikulu ya White House.

Zaidi ya Wamarekani milioni 67 walijitokeza kushuhudia Harris na Trump wakipambana kwenye mdahalo huko Pennsylvania Septemba 10, mwaka huu. Lakini kura za maoni zinasemaje kuhusu nani alifanya vyema zaidi kwenye mdahalo huo?

Kura ya maoni ya Reuters/Ipsos iliyokuwa na wapigakura 1,400 waliokuwa wamepata angalau taarifa fulani kuhusu mdahalo iligundua kuwa 53% waliona Harris alishinda na 24% waliona Trump alishinda. Pia, ilionyesha kuwa Harris aliongoza kwa pointi tano zaidi ya mpinzani wake kitaifa, yaani asilimia 47 hadi asilimia 42, ikilinganishwa na asilimia 45 hadi asilimia 41 za Agosti.

Kura ya maoni ya ‘YouGov’ ya watu wazima 1,400 nchini Marekani iligundua kuwa kati ya wale walioshuhudia mdahalo, asilimia 55 waliona kuwa Harris alishinda na asilimia 25 walimpa Trump.

Hakukuwa na ongezeko kwa Harris katika kura ya maoni ya ‘Morning Consult’ ya wapigakura 3,300 ambayo katika hiyo, Kamala aliongoza kwa asilimia 50 hadi 45, ingawa Trump alikuwa chini kwa pointi moja kutoka asilimia 46 katika kura yao kabla ya mdahalo.

Anayeongoza kura za maoni kitaifa

Katika miezi kadhaa kabla ya uamuzi wa Biden kujiondoa kwenye kinyang’anyiro, kura za maoni mara kwa mara zilionyesha kuwa alikuwa nyuma ya Trump. Hata hivyo, kura kadhaa zilionyesha kuwa Harris hangekuwa bora sana.

Lakini mbio zilipopamba moto na yeye kuanza kampeni ameanza kuonekana kuwa yuko mbele ya mpinzani wake katika wastani wa kura za maoni kitaifa ambao ameuendeleza tangu wakati huo.

Ingawa kura hizi za maoni kitaifa ni mwongozo mzuri wa jinsi mgombea alivyo maarufu nchi nzima, hazitatoa utabiri sahihi wa matokeo ya uchaguzi ujao.

Hii ni kwa sababu Marekani inatumia mfumo tofauti na mifumo ya uchaguzi inayotumika katika nchi nyingi. Katika mfumo huo unaoitwa ‘Electoral College’, Marekani ina jumla ya kura 538 za ‘Electoral College’. Kila jimbo linapewa idadi ya kura za uchaguzi kulingana na idadi ya wawakilishi wake katika Baraza la Wawakilishi (House of Representatives) na Seneti.

Kwa mfano, jimbo la California lina kura nyingi zaidi kwa sababu lina idadi kubwa ya watu, wakati majimbo madogo kama Wyoming yana idadi ndogo ya kura za uchaguzi.

Wapigakura wanachagua wawakilishi wa ‘Electoral College’ wakati wa uchaguzi. Kura hizi zinaitwa “kura za uchaguzi”. Kila jimbo lina mchakato wake wa kupata wawakilishi hawa, lakini mara nyingi, chama kinachoshinda kura nyingi za jimbo, hicho kinapata kura zote za uchaguzi za jimbo hilo (sheria ya “winner-takes-all”).

Ili kushinda urais, mgombea anahitaji kupata angalau kura 270 za ‘Electoral College’ kutoka kwa jumla ya kura 538.

Ikiwa hakuna mgombea anayeweza kufikia kiwango hiki, uchaguzi hupelekwa Baraza la Wawakilishi ambako kila jimbo lina kura moja na hutegemea uamuzi wa majimbo kuchagua rais.

Kwa kawaida, mgombea anayeongoza kitaifa kwa kura za wananchi (popular vote) si lazima awe ndiye anayeshinda urais.

Kwa mfano, mgombea anaweza kushinda kura za wananchi, lakini akashindwa kura za ‘Electoral College’, kama ilivyotokea kwa Al Gore mwaka 2000 na Hillary Clinton mwaka 2016.

Uchaguzi mkuu hufanyika Jumanne ya kwanza baada ya Jumatatu ya kwanza Novemba kila mwaka wa uchaguzi, na ndiyo sababu utafanyika Jumanne, Novemba 5, mwaka huu.

Baada ya uchaguzi, kura za ‘Electoral College’ zinakusanywa na kuwasilishwa kwenye Congress kwa uthibitisho rasmi.

Hii hufanyika Desemba, wakati wawakilishi wa ‘Electoral College’ wanakutana katika miji yao wenyewe na kumpigia kura Rais na Makamu wa Rais. Matokeo haya kisha yanatangazwa rasmi na Congress, Januari.

Kwa sasa, hali ya kura za maoni ni ngumu sana katika majimbo saba ya mapambano ambayo ni majimbo yenye umuhimu mkubwa katika uchaguzi huu. Hali hii inafanya iwe vigumu sana kwa wachambuzi na wapigakura kujua ni nani anayeshikilia nafasi ya kuongoza katika mbio hizi za urais.

Kura za maoni za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kuna tofauti ndogo sana, chini ya asilimia moja, inayotenganisha wagombea wawili katika majimbo kadhaa muhimu. Hii inajumuisha jimbo la Pennsylvania, ambalo ni muhimu sana kwa sababu lina idadi kubwa zaidi ya kura za uchaguzi. Kwa hivyo, jimbo hili linaweza kuwa na athari kubwa kwa mshindi kufikia lengo la kura 270 zinazohitajika ili kushinda urais.

Pennsylvania, pamoja na majimbo ya Michigan na Wisconsin, yalikuwa ngome imara za chama cha Democrats kabla ya Rais Trump kuzigeuza kuwa ngome za chama cha Republican katika uchaguzi wa mwaka 2016. Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Rais Joe Biden alifanikiwa kurejesha majimbo haya kuwa ngome za Democrats.

Ikiwa Kamala Harris atafanikiwa kufanya vivyo hivyo mwaka huu, itamwezesha kuwa kwenye njia sahihi ya kushinda uchaguzi na kuingia katika nafasi ya urais.

Hali hii inaonyesha kwamba mbio za uchaguzi zinaendelea kuwa ngumu na zinazoshikilia nafasi ya kushinda inategemea sana jinsi wagombea wanavyoendelea kupambana katika majimbo haya muhimu.

Kura za maoni zitakuwa na jukumu muhimu katika kuelewa mwelekeo wa mwisho wa uchaguzi na matokeo yatategemea sana hali ya majimbo haya muhimu.

Je, kura za maoni zinaaminika?

Kwa sasa, kura za maoni zinaonesha kwamba Kamala Harris na Donald Trump wanapishana kwa pointi chache za asilimia ya kila mmoja kitaifa na katika majimbo ya mapambano.

Kwa kuwa wamekaribiana sana, ni vigumu sana kutabiri mshindi kati ya hao wawili.

Related Posts