KONA YA MALOTO: Kenya na harakati za Gen-Z, Tz ni hofu ya wasiojulikana

Desemba 9, 1961, Tanganyika ilipopata uhuru, Watanganyika wote walisherehekea kuwa huru. Baba wa Ali Kibao, babu wa Deusdedith Soka na bibi wa Ben Saanane, walikuwa juu kabisa kwenye wingu la tisa, kwa furaha.

Uhuru ni chemchemi ya utu, usalama na amani, ndivyo babu wa Azory Gwanda na bibi wa Simon Kanguye, waliamini. “Wakoloni na walowezi waondoke, tujitawale wenyewe,” ni wimbo ulioimbwa hadi na babu yake Edgar Mwakabela “Sativa”.

Karamu na nderemo za siku ya uhuru, zilijengwa kwa mantiki ya ukombozi. Kila aliyekuwa shereheni Desemba 9, 1961, hakudhani kuwa ingefika Septemba 2024, ambayo sauti kutoka kwa viongozi wa dini, zingebeba ujumbe wa kukemea utekaji na mauaji ya Watanzania.

Wakoloni waliondoka zao. Miaka 63 baada ya kujitawala wenyewe, Watanzania wanaishi kwa hofu. Ni kama hadithi ya filamu ya “Fear Over the City”, iliyochezwa na gwiji wa Kifaransa, Jean-Paul Belmondo. Maharamia Marcucci na Minos, walisababisha jiji lisiwe na amani wala utulivu.

Uhalifu wa Marcucci na njama za Minos, kuua warembo vijana, kwa pamoja, matukio yao yalifanya hofu iligubike jiji la Paris, Ufaransa. Ni filamu ya mwaka 1975, kutoka kwa mwongozaji na mwandishi, Henri Verneuir. Miaka 49 baadaye, Tanzania siyo filamu, bali maisha halisi, yenye kujaa hofu kubwa.

Watu wanaogopana kupita kiasi. Ikibishwa hodi mlangoni, unauliza mara mbili-mbili, maana unaweza kufungua mlango, ukajikuta asusa ya jumuiya ya watu wasiojulikana. Wakikunasa, wakikurudisha salama, itabidi familia yako ifanye sherehe na wanajamii wajumuike. Vinginevyo utakuwa hadithi isiyo na maelezo.

Si kauli yenye kuvutia. Haieleweki jamii itakuchukuliaje, ukisema “afadhali Ali Kabao, ndugu zake wameona mwili, japo uliumizwa, lakini wamezika, wanajua baba, kaka, mjomba, babu, mtoto wao, yupo kaburini.” Ndiyo, Ali amezikwa kijijini Darigube, Tanga. Yupo mtu atahoji; afadhali ipo wapi, wakati alikatishwa maisha kwa vipigo vya mateso ya kinyama na kumwagiwa tindikali?

Rombo, Kilimanjaro, familia ya Ben Saanane, kwa miaka nane sasa, hawajui waweke matanga, wakubali yaishe, ndugu na mtoto wao hatarudi tena, alishakufa au kuuawa. Wapo njiapanda yenye maumivu makali. Ipo minong’ono kwamba alishauawa. Wanong’onaji nao hawana uhakika na wanachokinong’ona.

Jumuiya ya watu wasiojulikana ina “miguvu” isiyomithilika. Waliingia ndani ya nyumba za viongozi Dodoma, wakampiga risasi 38 Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu. Risasi 16 wakazizamisha kwenye mwili wa binadamu. Hawakumuua, ila wamemwacha mlemavu. Walifeli, maana lengo lao lilikuwa kumtoa roho.

Walinzi ambao hulinda nyumba hizo kila siku, hawakuwepo siku Lissu anashambuliwa. Walikimbia? Walijificha? Ulikuwa mpango? Wapo watu wanatuhumu kuwa walinzi waliondolewa kazini ili Lissu atunguliwe shaba bila upinzani. Ukiwa bado unazitafakari nguvu za watu wasiojulikana, jielekeze kwa Ali Kibao, alikuwa amepanda basi, usafiri wa umma. Basi lilijaa watu. Hiyo haikuwazuia kuingia kwenye gari na mitutu ya bunduki, wakamfunga pingu Ali na kuondoka naye. Wakampiga na kumuumiza mno kichwani. Uso wake wakauharibu na tindikali.

Kichwani kwako tafsiri ni kuwa jumuiya ya wasiojulikana ni watu katili mno. Mimi nitakwambia, ukatili wao ni matokeo ya kukosa akili na aibu, hivyo wamekuwa wanyama. Halafu, ulinzi wao ni nguvu zao zenye kuielemea hadi dola. Wanaua na inajulikana, kama Ali Kibao, wanashambulia mchana kweupe kwenye nyumba za viongozi, palipo na ulinzi pamoja na CCTV Camera, na hakuna wa kuwafanya kitu.

Jumuiya ya watu wasiojulikana ni kama jini. Chatu si chatu. Saanane, Azory na Kanguye, walinyakuliwa. Ni kama walimezwa wakapotelea tumboni. Au hadithi ya pipa la tindikali, wakayeyushwa. Watu hao ni Watanzania na walipata madhila Tanzania, kwenye mikono ya Watanzania wenzao.

Uhuru ulileta matumaini. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akasema: “Tunawasha Mwenge juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro. Upeleke upendo palipo na chuki, utu kwenye unyonge, heshima palipo na dharau, matumaini palipokata tamaa.” Miaka 63 baada ya tamko la uhuru, chuki ipo, Watanzania wanauana, sababu ni ujinga mtupu.

Suala la uhai wa Mtanzania linapaswa kuwa jambo lenye kuunganisha Watanzania wote. Ni masilahi ya pamoja. Haipo hivyo.

Nyakati ambazo watu wanapotezwa na haijulikani walipopelekwa. Walionyakuliwa nyumbani kama Azory na Kanguye, waliobebwa saa 5 asubuhi kweupe kama Soka na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise. Aliyechukuliwa Dar es Salaam, akapelekwa Arusha, halafu akatupwa porini Katavi. Hilo ni tukio la Sativa.

Leopold Lwajabe, alikuwa Mkurugenzi wa Miradi, Wizara ya Fedha, alipotea wiki moja, kisha akakutwa Mkuranga, akiwa siyo yeye, bali mwili wake. Ni tukio la mwaka 2019.

Afadhali, Mdude Nyagali na Ibrahim Mshana “Roma Mkatoliki” na wenzake, walisulubiwa, lakini walirejeshwa. Ni kama ilivyotokea kwa mfanyabiashara bilionea, Mohammed Dewji “MO”.

Baba na mama au babu na bibi, walioshiriki harakati za uhuru na kufurahi kupata dola yao, laiti wangejua watoto na wajukuu wao, wangetekwa na kuuawa na Watanzania wenzao, halafu kusiwe na uchunguzi, wala maendeleo yoyote ya kuwafikia wahalifu, pengine wangerudi nyuma. Wangeona bora wakoloni waendelee. Maumivu ya kusababishiwa na ndugu, yanatesa kuliko yaletwayo na adui.

Kenya, vijana wa kundi rika la waliozaliwa mwaka 1996 mpaka 2010 (Generation Z), wanaungana kusukuma agenda ya mabadiliko ya kimsingi. Wanazuia hadi muswada ambao wanaona ungesababisha maisha yao kuwa magumu. Nguvu ya vijana na umma, inaonekana.

Tanzania, vijana wanaopaza sauti mitandaoni kukosoa Serikali, ndio wanageuka shabaha ya jumuiya ya watu wasiojulikana. Kenya, vijana wanajaa ujasiri wa kuipigania nchi yao. Tanzania, wasiojulikana wanajaza hofu kwa utekaji na mauji.

Viongozi wa dini wanakemea utekaji na mauaji. Sauti zimesikika kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki (Tec) hadi Baraza la Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata). Nilikuwepo Arusha, katika wiki ya Asasi za Kiraia, nikasikia hotuba kali ya Askofu wa KKKT, Dayosis ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, akilaani vikali utekaji na mauaji. Ni nchi ya hofu. Viongozi wa dini kazi yao ni kulaani.

Miaka inakatika, hakuna majibu ya vifo mfululizo na maiti zilizokutwa fukwe za Bahari ya Hindi, zikiwa kwenye vifurushi, kati ya mwaka 2016 mpaka 2018. Mkuranga, Kibiti na Rufiji, watu wengi wamepotea. Tanzania Bunge lipo. Matukio haya yanajiri kwenye majimbo yenye wabunge. Bunge halijaweka alama yoyote ya kupigania uhai wa watu ili kukomesha matendo haya kujirudia. Ni dola ya hofu.

Related Posts