Kwa wiki mbili sasa, mada iliyotawala vyombo vya habari, baraza na vijiwe vya mazungumzo Tanzania Bara na Visiwani ni matukio ya watu kutekwa nyara na kupotea, wengine kuteswa na miili yao kuokotwa kwenye vichaka au fukwe za bahari.
Katika suala hili, tumesikia sauti za wanasiasa, taasisi za kiraia, viongozi wastaafu, wanasheria na watu mbalimbali.
Vilevile, yamechomoza maoni yenye mawazo tofauti kuhusu suala hili yanayoeleza wasiwasi mkubwa wa maisha uliopo nchini hivi sasa na kujiuliza ni nani hao wanaoitwa watu wasiojulikana wanaofanya mambo haya?
Baadhi ya viongozi wa taasisi za ulinzi na usalama wa taifa na wanasiasa wamenyooshewa vidole vya tuhuma ya kuhusika na hali hii ya kusikitisha na kutisha iliyopelekea watu kuwa katika hamkani.
Pia, zimesikika kauli za kutaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Yusuf Masauni na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura wawajibike, kama ilivyotokea siku za nyuma katika matukio kadha ya aina hii.
Miongoni mwa hao waliowajibika alikuwa Rais wa pili wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi, wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, mwaka 1976 kufuatia mauaji ya kikatili yaliyofanyika Shinyanga. Wengine wameshauri kama viongozi hawa hawatajiuzulu basi Rais Samia Suluhu Hassan awaweke kando ili watu warudishe imani yao kwa Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi.
Katika mjadala unaoendelea Zanzibar kwenye suala hili, kinachosikika kwa sauti kubwa ni kutaka hiyo Tume ya uchunguzi iwe huru na ni vema watakaoifanya kazi hiyo wawe wataalamu kutoka nje ya nchi.
Lakini kubwa zaidi ni kutaka kazi yake ijumuishe pia mauaji, utekaji nyara na mateso yaliyowakuta watu wa Visiwani, wakiwemo wanasiasa, viongozi wa dini na watu wa kawaida.
Ukiachilia mbali watu wengi waliouawa, wakiwemo mawaziri na viongozi waandamizi wa serikali na hata miili yao kutojulikana imefukiwa wapi katika miaka ya 1960 na 1980, mwendo wa watu kuuawa, kutekwa nyara na kupotea na wengine kuumizwa vibaya umekuwa ukiendelea.
Habari hizi zimekuwa zikisambaa na hata kuonyeshwa watu walivyojeruhiwa vibaya katika mitandao.
Katika matukio ya aina hii, ukiachilia yale yaliyowahi kutawala vyombo vya habari, hasa ya viongozi wa ACT Wazalendo, Nassor Mazrui na Ismail Jussa, wapo wengi walioumizwa na kupotea.
Kati ya walioumizwa baada ya kuvamiwa nyumba yake usiku, akaumizwa vibaya na kuiaga dunia akiwa katika hospitali ya Al Rahma ni mzee maarufu wa Bwejuu, Ameir bin Soud (Bindu) ambaye alikuwa akichambua katika mitandao historia ya Zanzibar.
Mwingine ni aliyekuwa Kamishna wa Bajeti, Juma wa Juma, ambaye inasemekana alichukuliwa akiogelea hapo Mazizini, nyuma ya hoteli ya Beach Resort.
Juma alikuwa amejitokeza kutaka kugombea kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi wa Rais wa mwaka 2020.
Juhudi za wake zake wawili, wanafamlia na marafiki za kutaka Polisi iwaeleze walifikia wapi katika uchunguzi, zimegonga mwamba, huku zikisikika tetesi huku na kule kuhusu suala hili.
Kwa matukio yote haya, haijawahi kutolewa taarifa yoyote ya Polisi wala hata mtu mmoja kufunguliwa mashitaka, kama vile walitekwa au kuuawa na upepo mkali wa Bahari ya Hindi.
Sasa, baada ya matokeo ya kuuliwa kwa kiongozi wa Chadema, Ally Mohammed Kibao na wenzake, chagizo la kuitaka Serikali iunde Tume huru ya uchunguzi imepamba moto Tanzania Bara.
Watu wa Zanzibar nao wanataka uchunguzi huo uvuke bahari na hasa ukitilia maanani kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ni ya Muungano.
Tatizo kubwa linaloonekana Zanzibar ni watu wanaofanya maovu haya ya mauaji, wamekuwa siku zote hawaguswi na wanapozeeka na wengine kuadhirika njiani na hata kusema maneno ya ovyo wanajitokeza wengine, kama vile mchezo wa kupokezana vijiti.
Uzoefu umedhihirisha kwamba unapofumbia macho uhalifu wa kinyama wa aina hii, basi wengine wanaopenda mambo hayo hupata nguvu na ujasiri wa kuyafanya kwa kujua hawataguswa kisheria, isipokuwa watalaaniwa tu midomoni.
Uchunguzi huru wa kuwatambua na kuwawajibisha hao wanaoitwa watu wasiojulikana ambao bado wanaendelea kuhujumu watu majumbani, una umuhimu mkubwa katika kuhakikisha upo utawala bora na wa haki na sheria Zanzibar kama alivyoahidi Rais Hussein Mwinyi.
Uchunguzi huru, kama utafanyika, huenda ukawa mwarobaini wa kukomesha vitendo vya kinyama vya hao watu wanaoitwa wasiojulikana, ambao wamepewa majina ya kila aina kama Janjaweed na Mazombi.
Uchunguzi wa mauji ujumuishe Zanzibar. Utasaidia kupunguza joto la wasiwasi wa maisha Zanzibar kuelekea uchaguzi wa 2025 na hasa ukitilia maanani tayari hali imeanza kuwa tete.