Janga la mafuriko linaendelea kuwatesa wakaazi wa mataifa kadhaa ya Ulaya ya Kati. Nchini Ujerumani mji wa Dresden umeshuhudia mvua kubwa kwa siku kadhaa na hivi sasa uko kwenye hatari kubwa ya kukabiliwa na mafuriko. Takriban watu 20 wameripotiwa kufariki kufikia leo Jumatano kutokana na mafuriko katika nchi za Poland, Austria,Jamhuri ya Czech na Romania.
Hapa Ujerumani mto Elbe ambao unapitia kwenye mji wa Dresden,kiwango cha maji kimeongezeka hadi mita 6, jambo ambalo limezifanya mamlaka kutangaza hali ya tahadhari ya kiwango cha juu hii leo Jumatano. Wasiwasi wa wakaazi wa mji huo umeongezeka kutokana na kitisho cha mafuriko.
”Katika siku za baadae tutakuwa tunaogopa tukisikia mvua itanyesha kwa siku tatu au nne. Tutakumbuka matukio haya kwa muda mrefu sana”
Maeneo yenye makaazi mengi, barabara kuu za mji huo pamoja na njia za reli zote zimetajwa kuwa katika kitisho cha kukumbwa na mafuriko. Maji ya mto Elbe katika eneo la karibu na mpaka wa Jamhuri ya Czech yameongezeka na yanatarajiwa kuendelea kuongezeka katika kipindi cha siku hii ya leo ingawa maafisa Ujerumani hawaamini ikiwa maji ya mto huo yanaweza kupanda kufika mita saba,jambo ambalo linaweza kusababisha kutolewa tahadhari ya juu zaidi kwenye eneo hilo.Jana waziri wa mazingira wa Jamhuri ya Czech Petr Hladik alitowa tahadhari kuhusu kuongezeka maji ya mto Elbe.
Soma pia: Mafuriko Ulaya: Utabiri wa mvua zaidi huku maelfu wakihama
” Hali ya mafuriko katika Jamhuri ya Czech itaendelea kushuhudiwa kwa siku nyingine nyingi zaidi. Jumanne mchana maji ya mito Vltava na Elbe yataongezeka katika eneo la Melnik. Wakati maji hayo yatakapokuwa yanatoka Jamhuri ya Czech itakuwa Jumatano jioni au usiku na tutashuhudia mito ikifurika. Hii maana yake ni kwamba mito mengine iliyobakia itafikia viwango vyake vya juu vya maji, leo au kesho. Lakini kama nilivyosema awamu ya tatu ya mafuriko itaendelea kwa siku kadhaa nyingine zijazo.”
Ujerumani mpaka sasa ndio nchi kwa kiasi kikubwa iliyonusurika na athari mbali za mvua kubwa na mafuriko ambayo kwa sasa yanalikumba eneo kubwa la Ulaya ya Kati na Mashariki. Watu wasiopunguwa 20 wamekufa kufuatia mafuriko hayo yanayoshuhudiwa Poland,Austria,Jamhuri ya Czech na Romania.Soma pia. Watu 18 wafariki dunia kutokana na mafuriko barani Ulaya
Na waziri wa mambo ya ndani wa Jamhuri ya Czech Vit Rakusan akitowa taarifa kwenye mkutano maalum kuhusu janga hilo leo Jumatano mjini Prague amesema visa vya kwanza vya uporaji vimeripotiwa katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko nchini humo.
Waziri huyo amesema hatua kali zitachukuliwa kwa waliofanya vitendo hivyo wakati wa majanga huku akitahadharisha kwamba wizi wa mabavu ni uhalifu unaobeba adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela bila ya msamaha.
Katika mji wa Usti nad Labern kingo za kuzuia mafuriko na magunia ya mchanga yamepelekwa kulizuia eneo hilo kuathirika huku watu wanaoishi kwenye maeneo mengi ya nyanda za chini wakiwa wamehamishwa.
Jamhuri ya Czech pia imeomba msaada kutoka mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya.Huko Slovakia mto Danube pia maji yameongezeka yakifikia zaidi ya mita 9.7