Rais samia amedhamiria kuifungua Kigoma – Dkt. Biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuipatia Kigoma miradi ya maendeleo na fursa mbalimbali ili kuufungua mkoa huo kiuchumi.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Kata ya Kasanda Wilaya ya Kakonko leo Septemba 18, 2024 Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imetekeleza miradi mingi ya maendeleo mfano hospitali na barabara ikilinganishwa na kipindi kilichopita ambapo wananchi walikuwa kitaabika kupata huduma mbalimbali za kijamii.

“ Halmashauri hii imeanzishwa mwaka 2013 na kwa kiasi kikubwa maeneo mengi yalikuwa mapori lakini leo tumetembelea Hospitali ya Wilaya ya Kakonko hali halisi ya maendeleo inaonekana. Rais wetu anataka Kigoma ifikike na watu wakae kwa amani na kufurahia kuwa Kigoma, nimefurahi sana kuona majengo ya hospitali ya wilaya.” Amesema Dkt. Biteko.

Awali wananchi wa Kakonko walikuwa wakipata huduma za afya kutoka Hospitali ya Bugando na Geita, uwepo wa hospitali hiyo utasaidia kupunguza gharama ya kufuata mbali huduma za afya.

Akizungumzia barabara ya Kakonko hadi katika mpaka wa Tanzania na Burundi Dkt. Biteko amesema maisha ya watu ni kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Sita. “Hatutaki maigizo kwenye maisha ya watu, tunataka kuwahakikishia hata barabara ya Nyakanazi Kasulu hadi Kigoma inaunganishwa kwa lami. Rais Samia anataka kuona tunafanya biashara na majirani zetu na kuwa mpakani sio laana bali ni fursa na milango ya biashara itafunguliwa na barabara hii yenye urefu wa km 48 ya Kakonko hadi mpakani itasimamiwa na TANROADS.” Amesema Dkt. Biteko.

 

Vilevile, amewapongeza wananchi wa Kakonko kwa kuzalisha chakula cha ziada tani 81,000 ambapo mahitaji ni tani 76,000 na tani za chakula zilizopo ni tani 157,000.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko ametoa wito kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuendesha mchakato mzuri wa kura za maoni na wachague wagombea wenye sifa na sio kutumia rushwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Zainabu Katimba amesema kuwa Rais Samia amefanya uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa ajili ya majengo na vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, aidha ametoa maelekezo mahsusi kuwa hospitali zote za wilaya nchini ziwe na wodi ya watoto ili kupunguza vifo kwa mama na mtoto.

Vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 556 hadi 104 katika vizazi hai 100,000. Mhe. Katimba amesema hayo mafanikio hayo ni matokeo ya jitihada kubwa inayofanywa na Rais Samia kwa ajili ya akina mama nchini.

Pia, Mhe. Katimba amezungumzia barabara na kusema kuwa awali wilaya hiyo ilikuwa inapokea kiasi cha shilingi milioni 700, katika kipindi cha Rais Samia ameongeza fedha hadi kufikia shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya barabara za dharura.

“ Barabara inayoelekea hospitali ya wilaya yenye urefu wa km 1, mwaka huu Mhe. Rais ametoa fedha shilingi milioni 450 ili iweze kujengwa na muweze kufika hospitali vizuri, hakika wilaya hii imepata uwekezaji mkubwa.” Amebainisha Mhe. Katimba.

Aidha, amewahimiza wananchi wa Kakonko kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na baadae kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kakonko na Diwani Kata ya Gwarama, Bw. Fidelis Nderego amesema “ Kakonko tukipata barabara ya kiwango cha lami hadi Soko Kuu la ujirani mwema kati ya Kakonko na Burundi uchumi wa wananchi wa Kakonko na Mkoa wa Kigoma utafunguka kiuchumi.”

Related Posts