Leo ni siku ya kadi, mara ya mwisho lini ulimtumia umpendaye?

Dar es Salaam. Kulikuwa na utaratibu wa kutumiana kadi za aina na jumbe mbalimbali. Kuna waliofanya hivyo kuwapa zawadi waliokuwa wakiadhimisha siku zao za kuzaliwa, kumaliza hatua fulani ya masomo, kupata mtoto na vitu vya namna hiyo.

Baada ya kukua kwa teknolojia na ujio wa simu za mkononi, kutumiana kadi za makaratasi kumepungua.

Lakini, kwa wapenzi kutumiana kadi walifanya hivyo kwa kuzipakua mtandaoni na kuwatumia wapendwa wao.

Je, unamjua mwandishi wa kadi au mchapishaji? Kama yupo nenda kamkumbatie, kwani leo dunia inaadhimisha Siku ya kuwakumbatia waandishi wa kadi kwa kimombo: ‘Hug a Greeting Card Writer Day’.

Maadhimisho hayo ni mahususi kwa waandishi wa kadi za salamu. Wahenga wenzangu mtakuwa mnakumbuka, hadi redioni tulikuwa tunatumiana kadi hizi zinasomwa na aliyetumiwa anasikia huko aliko kuwa amekumbukwa.

Ilikuwa sehemu ya salama za upendo na kuonyeshana utu, kukumbukana na mambo mengine yanayochochea mapenzi ya ndugu, wenza na makundi mengine.

Wahusika wa kuandika hizi kadi kwa kawaida ni kama hawajulikani, lakini wanaishi kwenye mioyo na maisha ya walio wengi, leo tuwape maua yao hata kwa kukumbuka kuwa wapo.

Kupitia kadi hizi za salamu hutuwekea mashairi, vichekesho au hata ujumbe maridhawa unaotia moyo na kuheshimu uwepo wa wengine.

Historia ya kutumiana kadi ilipoanzia

Utamaduni wa kutumiana salamu kwa maandishi ulianzia nchini China na Misri, ambapo kadri siku zilivyokuwa zinakwenda ukawa unaboreshwa na hadi kufikia kwenye hatua ya kadi.

Kadi za kwanza za salamu barani Ulaya zilitengenezwa nchini Ujerumani karne ya 15, zikiwa na sanaa na mashairi ya kipekee.

Mwaka 1843, kadi ya kwanza ya Krismasi ilitengenezwa London, iliyoandikwa na msanii kwa ajili ya Sir Henry Cole.

Kwa nini Cole alitengenezwa kadi? Katika familia ya Cole, kipindi cha Krismasi kilikuwa cha shughuli nyingi, na barua nyingi zikiwa hazijajibiwa, ilihitajika suluhisho la kuokoa muda.

Henry Cole, aliamua kumshirikisha rafiki yake, msanii John Callcott Horsley ambaye anatambulika kama mbunifu wa kwanza kubuni kadi za salamu.

Bada ya kushirikishwa alibuni kadi. Katika kumbukumbu yake ya Desemba 17, 1843, Cole aliandika, “Jioni, Horsley alikuja na kuleta muundo wake wa kadi za Krismasi.”

Hivi ndivyo historia ya kadi za Krismasi ilivyoanza, ikiashiria mabadiliko makubwa katika jinsi tunavyotuma salamu na kuwasiliana na wapendwa wetu wakati wa sherehe za Krismasi na nyinginezo.

Tangu wakati huo, kadi zimekuwa sehemu ya maadhimisho na furaha. Leo, takriban kadi bilioni 170 hutumwa kila mwaka.

Unaweza kusherehekea siku hii kwa kuwakumbatia waandishi wa kadi iwapo unawajua, kama kuwapongeza kuwa juhudi zao.

Pia unaweza kujifundisha mwenyewe kutengeneza kadi kupitia mtandao kwa sababu dunia imeshabadilika.

Si vibaya pia ukinunua kadi leo hii na kumtumia mpendwa wako.

Kwa wale wa siku nyingi, leo pia unaweza kufungua kwenye kumbukumbu zako na kuangalia kadi ulizowahi kutumiwa maishani mwako na kuwakumbuka waliofanya hivyo.

Related Posts