UDSM kuendeleza ujenzi wa majengo kampasi mpya mkoani Kagera kupitia mradi wa HEET

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kimeendelea kutekeleza mradi wao ujenzi wa Kampasi mpya inayojengwa Bukoba mkoani Kagera.

Ujenzi huo unajumuisha madarasa,kumbi za mihadhara, karakana, ofisi za walimu pamoja na mabweni kwa ajili ya wanafunzi.

Akizungumza na Waandishi wa habari Septemba 18,2024 katika eneo la Mradi huo, Naibu Mratibu wa Mradi, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Dkt. Liberato Haule amesema mradi huo ni kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Biashara unaosimamiwa na kampuni ya China Jiangxi.

Aidha Dkt.Haule amesema ujenzi huo utakapokamilika sambamba na mradi wa ujenzi wa Kampasi mkoani Lindi, Dar es Salaam pamoja na Zanzibar utasaidia kuongeza uwezo wa madarasa kubeba idadi kubwa ya wanafunzi.

“Tutakapokamilisha haya maeneo kwa ujumla wake kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tutakua tumeongeza sehemu ya wanafunzi kujisomea kwa maana ya madarasa yenye uwezo wa kukaa wanafunzi 2130 kwa mara moja, vilevile tutakuwa na maabara zenye kuchukuwa wanafunzi 881 kwa mara moja, karakana yenye kuchukua wanafunzi 280 kwa mara moja na vilevile tutakuwa na mabweni yenye kubeba wanafuunzi 480”, amesema Dkt. Haule.

Amesema wamepiga hatua kwenye mageuzi ya mitaala pamoja na mbinu za kujifunzia ambapo baada ya kufanya ufuatiliaji wa wahitimu kwa kutumia kamati za kitasnia pamoja na kupokea maoni kwenye vyuo vikuu vya kimataifa huko nje pamoja na wadau ambao ndio waajiri, walifikia uamuzi wa kuboresha mitaala iliyopo na kuunda mitaala mingine mipya.

Pamoja na hayo Dkt Haule ameeleza kuwa wameunda mifumo ya kidijitali ambayo itamsaidia kila mtu kupata nafasi kusoma katika mazingira alipo bila kumlazimisha mwanafunzi kuhudhuria eneo la Kampasi.

Vilevile Dkt.Haule amesema chuo kimeunda utaratibu wa ushirikiano na sekta mbalimbali zinazofundishwa chuoni hapo kwa lengo la wanafunzi pamoja na wakufunzi kuelewa zaidi kwa undani kile ambacho kinafundishwa na jinsi kitakavyomsaidia muhitimu.

“Sasa hivi wewe mtaalamu uliyebobea kwa uzoefu wako unaweza kuja Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, tunaweza kukualika kwenye kipindi ukazungumza wanafunzi wafanye nini kwenye hiyo sehemu”, amesema

Sambamba na hayo, Dkt.Haule amesema wamenunua vifaa saidizi vya kisasa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambapo wamelenga kugusa makundi yote bila kuacha kundi lolote nyuma.

Kwa upande wake,Dkt.Paul Ndumbaro, Mtaalamu wa Maendeleo ya Miundombinu ikiwemo majengo katika Mradi wa HEET Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema ujenzi upo katika hatua ya majengo ambapo ujenzi tangu uanze ni miezi mitatu na umefikia asilimia 10.

Naye Diwani wa Kata ya Karabagaine Samwel Aulila ameonesha furaha yake kwa kuletwa mradi huo katika kata yake, ndani ya vijiji viwili vya Kangabusharo na Itahwa, kwani anaamini maendeleo yatafanyika baada ya kuletewa mradi huo ikiwemo barabara na soko.

Vilevile, Afisa Mipango Miji na Vijiji Wilaya ya Bukoba Bruno Barongo amewataka wawekezaji kuchangamkia fursa na kwenda kuwekeza katika maeneo hayo kwa ajili ya kurahisisha huduma kwani tayari serikali imeyapima kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii na kibiashara.

Related Posts