Gadiel aanza kazi Chippa United, Majogoro kicheko

KIUNGO mkabaji wa Chippa United, Baraka Majogoro amefurahishwa kucheza na Mtanzania mwenzake beki Gadiel Michael aliyejiunga na timu hiyo, akiamini kuna kitu kikubwa kitaongezeka.

Gadiel alijiunga na timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Cape Town Spurs ya nchini humo ambapo Majogoro amesema amepata mtu wa kushauriana, hivyo anaamini watafanya kazi kwa ubora wa juu zaidi.

Majogoro aliliambia Mwanaspoti namna ambavyo wanapata wepesi wa kuyatatua baadhi ya mambo wanapokutana.

“Nina furaha Gadiel kusaini katika timu ninayoichezea. Hatapata shida ya kuyafahamu mazingira ama utamaduni wa timu, kwani nitamwelekeza. Nina uzoefu nilitangulia kujiunga pia itatupa nguvu ya kupambana ili kuwaonyesha viongozi kwamba Tanzania kuna vipaji na tutafanyika milango ya wengine kujiunga zaidi ama kuja kucheza soka Afrika Kusini,” alisema.

“Kitu kingine kinachofanya nifurahie ujio wa Gadiel ni beki mwenye uwezo mkubwa, nimecheza naye Ligi Kuu Bara, hilo litatufanya kupeana moyo kupambana zaidi.”

Kabla ya kujiunga na Chippa United, Majogoro alicheza KMC, Mtibwa Sugar, Polisi Tanzania, Ndanda FC huku Gadiel akicheza Azam, Yanga, Simba na Singida Fountain Gate.

Ukiachana na Majogoro, Gadiel, Mtanzania mwingine anayecheza Ligi Afrika Kusini ni Abdi Banda ambaye kwa sasa yupo Baroka Swallows na nje na timu hiyo alizichezea Highlands Park, TS Galaxy, Chippa United na Richards Bay.

Related Posts