Azam mguu sawa nishati safi ya kupikia

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Katika kupunguza utegemezi wa nchi kwenye mkaa na kuni, Bakhresa Group kupitia kampuni yake ya uzalishaji na usambazaji wa unga wa ngano wa Azam inatarajia kusambaza majiko 10 yanayotumia nishati safi ya Ethanol kwa mama na baba lishe nchi nzima.

Majiko hayo yatasambazwa kupitia Kampeni ya Nishati Safi ijulikanayo kama ‘Azam Wheat Flour Clean Energy’ ambayo inalenga kuunga mkono mkakati wa Serikali wa miaka 10 wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ambao ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Mei mwaka huu.

Mama lishe kutoka Soko la Buguruni, Hafsa Anthony, akipika chapati katika jiko linalotumia nishati safi ya kupikia ya Ethanol wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Azam kuhamasisha matumizi ya majiko hayo. Kulia ni Balozi wa bidhaa zinazozalishwa na Makampuni ya Bakhresa, Yvonne Cherrie maarufu Monalisa.

Akizungumza leo Septemba 18,2024 wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika Kiwanda cha Unga cha Buguruni Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Makampuni ya Bakhresa, Hussein Sufiani, amesema mpango huo utatekelezwa kwa mwaka mmoja na kwa kuanzia watasambaza majiko 500 kwa mama lishe jijini Dar es Salaam.

“Kampeni hii ni hatua muhimu katika kuunga mkono mkakati wa kitaifa wa serikali unaolenga kukuza matumizi ya nishati endelevu nchini kote, Bakhresa Group kupitia Azam Flour tumechukua hatua madhubuti kupambana na tatizo la kimazingira,” amesema Sufiani.

Naye Mtendaji Mkuu wa Said Salim Bakhresa (SSB), Ali Asgar Mukadam, amesema kampuni hiyo ambayo ni wazalishaji wa unga wa Azam ina uhusiano wa karibu na jamii hasa wauzaji wadogo wa vyakula wanaotegemea bidhaa zake hivyo, kwa kutambua umuhimu wa kundi hilo watasambaza majiko hayo kama hatua ya kuwasaidia kubadilika na kwenda kwenye nishati safi ya Ethanol.

Mkurugenzi wa Uhusiano wa Makampuni ya Bakhresa, Hussein Sufiani, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Dar es Salaam.

Mmoja wa Mama lishe kutoka Soko la Buguruni aliyeanza kutumia majiko hayo, Hafsa Anthony, amesema ni mazuri kulinganisha na jiko la mkaa alilokuwa akitumia awali.

Kwa upande wake Mratibu Miradi ya Nishati na Mazingira wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (Unido), Victor Hakimu, amesema majiko hayo yatasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira na kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi.

Inaelezwa kuwa majiko hayo ni salama kwani hayatoi moshi wenye sumu, yanapatikana kwa bei nafuu, yanaweza kuzalishwa ndani ya nchi na yanapika kwa haraka.

Related Posts