Dodoma. Familia ya mfanyakazi za ndani, Makiwa Abdalah (16) aliyefariki dunia kwa kupigwa na kitu butu kichwani katika familia iliyovamiwa na watu wasiojulikana jijini Dodoma, imejitokeza na kueleza sababu za kudaiwa kususia mwili wa ndugu yao.
Tukio hilo la mauaji lilitokea Septemba 16, 2024 katika Mtaa wa Segu Bwawani, Kata ya Nala Wilayani Dodoma, ambapo watu watatu walipoteza maisha, huku mama mwenye nyumba, Lusajo Mwasonge (40) akijeruhiwa na amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Wengine waliopoteza maisha ni Milcah Robert (12), aliyemaliza darasa la saba katika Shule ya Msingi Chilohoni pamoja na Mkazi wa Mailimbili jijini Dodoma, Fatuma Mohamed (20) waliokutwa wakiwa wameunguzwa moto.
Akizungumza leo Jumatano Septemba 18, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, baba mdogo wa marehemu Makiwa, Ramadhan Issa amesema alipigiwa simu Jumatatu ya Septemba 16, 2024 akielezwa kuwa mtoto wa kaka yake amechinjwa jijini Dodoma katika nyumba aliyokuwa akifanyia kazi.
Amesema jambo hilo lilileta taharuki miongoni mwa ndugu kutokana na mazingira ya kifo chake na kuwa familia haikuelewa.
“Sikupata taarifa zote, hivyo ikanibidi kuja mwenyewe hadi Dodoma. Hatukususia ni namna tulivyopokea taarifa ya tukio hilo. Mara tuliambiwa tuko polisi tunahojiwa na ndio maana watu walipokea taarifa hizo kwa jazba,” amesema.
Amesema familia ya Robert ilitaka watu wote waliouawa wazikwe Dodoma, lakini wao hawakutaka ndugu yao azikwe Dodoma kwa sababu huko hawana ndugu wengine, mbali na dada yake pekee, Jamila.
“Hawa unaowaona walizaliwa wenyewe, wako wawili tu na sisi hatutaki ndugu yetu azikwe mahali pengine mbali na Geita. Tulitaka kwa mazingira haya ahusike mwajiri wake, baada ya mwajiri kuelewa hilo hakuna utata,” amesema.
“Hata sasa tumechelewa sana, sisi kwa kawaida yetu mtu akifa azikwe muda huo, hatusubiri mtu. Habari ikishakaa vizuri tutapiga simu waandae kaburi maana tutazika wakati tutakaofika,” amesema.
Amesema watasafirisha mwili wa Makiwa kuelekea kijiji cha Shilungule, kata ya Busanda, wilayani Geita ambako yatafanyika maziko.
Dada ya mfanyakazi huyo aliyefariki dunia, Jamila Ibrahim (23) amesema jana ndugu zake walikuwa hawaelewi ni sababu zipi zilizonifanya kutopokea simu zao baaada ya kupata taarifa hiyo.
Amesema alikuwa hapokei simu kwa kuwa alikuwa kwenye mahojiano na polisi baada ya kutokea mauaji hayo juzi Septemba 16, 2024.
“Niliwaambia aje mtu mmoja aungane nami katika kufanikisha hili. Ndio baba (baba mdogo) akaja kuungana nami. Msiba huu umenifanya nimekuwa mpweke. Sisi tulikuwa wawili kwa mama yangu ambaye alishafariki,” amesema.
Kwa upande wake, ofisa elimu wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Ngwano Ngwano amesema halmashauri hiyo imebeba gharama muhimu za mazishi kwa watu waliopoteza maisha katika familia hiyo ya mwalimu mwenzao.
“Pamoja na gharama hizo, rambirambi kama Serikali inavyoagiza tutampatia mhusika na hao wanaokwenda kuzika Geita tumewawezesha gharama kidogo za mazishi, ili wafike huko Geita, kwa sababu msiba ni wa kwetu,” amesema.
Ngwano ambaye amemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, amesema kwa sababu mwili umeharibika safari ya kwenda Geita inafanyika leo Septemba 18, 2024 ili kuzuia kuendelea kuharibika.
Fatuma amezikwa jana Mailimbili, huku Milcah Robert (12) akizikwa leo katika Kata ya Nala.