RC Tanga atoa ‘ramani’ ya uchaguzi wa serikali za mitaa

Tanga. Serikali mkoani Tanga imetangaza ratiba ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Imesema matukio mbalimbali yataanza rasmi Oktoba 11, 2024 hadi siku ya uchaguzi huo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema kazi ya uandikishaji wapigakura mkoani humo itaanza rasmi Oktoba 11 hadi 20.

“Oktoba 21 itakuwa ni siku ya kubandikwa na kukagua majina ya wapigakura na kazi ya marekebisho ya majina itafanywa kabla ya Oktoba 28,” amesema Balozi Burian.

Amesema viongozi waliopo madarakani, uongozi wao utakoma rasmi Oktoba 25, 2024 na wanatakiwa kukabidhi ofisi zao kwa mamlaka husika.

Aidha, amesema wale wanaotaka kugombea nafasi hizo kwa mara nyingine na wagombea wengine wote watatakiwa kuchukua na kurejesha fomu kati ya Novemba mosi hadi 7, na siku ya mwisho ya kurejesha fomu itakuwa Novemba 8, 2024.

“Teuzi za wagombea zitaanza kufanyika katika vyama vyao, zikiambatana na uwasilishaji wa pingamizi kabla ya hatua nyingine kufuata,” amesema Balozi Batilda. Kampeni zitafanyika kuanzia Novemba 20 hadi 26, kisha uchaguzi utafanyika Novemba 27,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Kwa mujibu wa Balozi Burian, idadi ya vijiji imepungua na sasa viko 763 baada ya baadhi ya maeneo kuwa miji midogo, hivyo vitongoji vimepungua kutoka 4,566 na kufikia 4,531.

“Kwa mujibu wa GN ya 2024, vijiji vimepungua, kwa sasa kuna vijiji 763 na vingine vimeingia kwenye miji midogo na kuwa mitaa, kwa hiyo jumla ya vitongoji vimepungua kutoka vitongoji 4,566 mpaka 4,531 hivyo vitongoji 35 vinaguswa kwenye mgawanyo huo,” amesema.

Kwa nini mabadiliko ya maeneo ya kiutawala

Mabadiliko ya maeneo ya kiutawala katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini Tanzania yanahusu marekebisho au mabadiliko yanayofanywa kwenye mipaka ya kiutawala ya vijiji, kata, au mitaa.

Mabadiliko haya yanaweza kujumuisha kugawanywa, kuunganishwa, au kupanuliwa kwa maeneo fulani kwa sababu mbalimbali, kama vile ongezeko la idadi ya watu, mabadiliko ya kiuchumi, au maendeleo ya miundombinu.

Lengo kuu la mabadiliko haya ni kuhakikisha kuwa huduma za kijamii na kiutawala zinapatikana kwa ufanisi zaidi, pamoja na kurahisisha usimamizi wa shughuli za kiutawala na uchaguzi. Katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mabadiliko haya yanaweza kuwa na athari katika upangaji wa mipaka ya vituo vya kupigia kura, uteuzi wa wagombea, na hata idadi ya wapiga kura katika eneo husika.

Mabadiliko haya pia yanafuata sheria na kanuni za utawala wa nchi, huku ikihusisha ushirikishwaji wa wananchi na viongozi wa eneo husika ili kuhakikisha kuwa yanazingatia mahitaji ya kijamii na maendeleo ya eneo.

Mabadiliko ya maeneo ya kiutawala katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania yanarejelea marekebisho ya mipaka, idadi, au muundo wa vitengo vya kiutawala kama vijiji, mitaa, na kata ambayo yanaweza kufanywa na mamlaka ya Serikali. Mabadiliko haya yanaweza kuwa na athari katika uchaguzi wa viongozi wa mitaa, ambapo maeneo yanapangwa upya kwa mujibu wa mahitaji ya kiutawala, maendeleo ya watu, au mahitaji ya huduma bora zaidi.

Mabadiliko haya hutekelezwa kwa sababu kadhaa na miongoni mwazo ni pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma: Kwa kuongeza au kupunguza ukubwa wa eneo au idadi ya vitengo vya kiutawala, serikali inalenga kuhakikisha kuwa rasilimali za umma na huduma zinawafikia wananchi kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi.

Kukuza uwakilishi wa haki. Mabadiliko yanaweza kufanywa ili kuhakikisha kuwa uwakilishi katika ngazi za serikali za mitaa unalingana na idadi ya watu au mahitaji ya maendeleo ya jamii husika. Pia kuna kurekebisha mipaka ya kiutawala kwa lengo la kupunguza migogoro ya kijiografia kati ya vijiji, mitaa, au kata. Hii inahusisha kubadilisha mipaka ili kufuata vizuri hali ya kijiografia au idadi ya watu katika maeneo hayo.

Pia kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii ili kusaidia kusimamia vema mipango ya maendeleo kwa kuzingatia ukuaji wa uchumi, ongezeko la watu, au mabadiliko ya kijiografia katika maeneo fulani.

Jingine ni kuboresha demokrasia na ushiriki wa wananchi ikilenga kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwa na vitengo vidogo vya kiutawala vinavyowezesha uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi.

Kwa hiyo, mabadiliko ya maeneo ya kiutawala yanaathiri jinsi maeneo yanavyogawanywa, kusimamiwa, na jinsi chaguzi zinavyoendeshwa, kwa lengo la kuleta ufanisi, maendeleo na uwakilishi bora katika serikali za mitaa.

Imeelezwa kuwa nafasi zinazogombewa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hutegemea aina ya halmashauri inayofanya uchaguzi, kama ni Mamlaka ya Wilaya au Mji.

Kwa Mkoa wa Tanga, kuna maeneo ya utawala yanayohusika kwenye uchaguzi huo ambayo ni Mamlaka ya miji midogo mitatu,kata 245,mitaa 270,vijiji 763 na Vitongoji  4,531.  

Hii ni kwa mujibu wa amri ya mgawanyo wa maeneo ya utawala katika mamlaka ya serikali za mitaa iliyotolewa chini ya kifungu cha 30 cha sheria ya serikali ya mitaa sura 287 na kutangazwa kwenye gazeti la serikali namba 796 la tarehe 6/09/2024.

“Kwa mujibu wa GN ya 2024 vijiji vimepungua kuna vijiji 763 na vingine vimepungua kwa kuingia kwenye miji midogo  na kuwa mitaa,kwa hiyo jumla ya vitongoji vimepungua kutoka vitongoji 4,566 mpaka 4,531 hivyo vitongoji 35 vinaguswa kwenye mgawanyo huo”,anasema Balozi Batilda.

Anasema ni muhimu kuzingatia kuwa nafasi inayogombewa katika Mamlaka ya Mji Mdogo ni moja tu, yaani mwenyekiti wa kitongoji.                                    

Ametaja nafasi za uongozi zitakazogombewa katika ngazi ya mtaa kuwa ni mwenyekiti wa mtaa, wajumbe watano wa kamati ya mtaa ambao kati yao, wawili watakuwa wanawake.

Kwa mujibu wa Balozi Burian, mkazi yeyote ana haki ya kuandikishwa kupiga kura kama atakuwa anasifa ya kuwa ni raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi, awe mkazi wa eneo la kitongoji au mtaa husika na awe na akili timamu.

Mkuu huyo wa mkoa ametaja makosa ya kuepukwa wakati wa uchaguzi ambayo ni pamoja na ya kuiandikisha zaidi ya mara moja kwenye orodha ya wapigakura, kupiga kura zaidi ya mara moja kwa wagombea wa nafasi moja, kutishia wapiga kura au wagombea ili kuvuruga uchaguzi, kufanya kampeni siku ya uchaguzi na kuvaa mavazi au kuonyesha ishara zinazoashiria kumtambulisha mgombea au chama cha siasa ndani ya mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura.

Balozi Batilda amesisitiza kuwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kosa lolote la uchaguzi atakabiliwa na adhabu ya faini isiyozidi Sh300,000 au kifungo kisichozidi miezi 12, au vyote kwa pamoja.

Amewahimiza wakazi wenye umri wa miaka 18 au zaidi, au wale watakaofikia umri huo kabla ya tarehe ya uchaguzi, kujitokeza kujiandikisha ili wasipoteze haki yao ya kupiga kura. Pia, wananchi waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wanatakiwa kujiandikisha tena kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024.

Aidha, amewataka wale wenye sifa za kugombea kujiandikisha kupitia vyama vyao vya siasa na kushiriki uchaguzi huo ili kuchangia maendeleo ya maeneo yao.

Kauli za Wanasiasa Kuhusu Uchaguzi

Katibu wa CCM mkoa wa Tanga, Seleman Sankwa, amesema chama chao kimejiandaa vizuri kwa uchaguzi huo na kwamba wagombea wao watachaguliwa kwa urahisi kutokana na ubora wao katika jamii. Ameeleza kuwa hawatatumia maneno mengi katika kuwanadi wagombea wao, kwani wamejipambanua vizuri kwa matendo yao.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Tanga, Michael Haule, ameeleza kuwa chama chao kimejipanga kikamilifu kwa uchaguzi huo, huku akisisitiza kuwa wamewapatia wanachama wao elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kupiga kura.

Mwajuma Mshana, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Swahili. Kata ya Ngamiani, amesema kuwa wapo tayari kushiriki uchaguzi huo, na kila mmoja anatambua mchango wake kwa jamii kupitia uongozi wake.

Related Posts