Miradi yenye thamani ya Sh78 bilioni yakutwa na kasoro Zanzibar

Unguja. Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca) imefuatilia miradi 70 ya maendeleo kati ya hiyo, 32 yenye thamani ya Sh78.76 bilioni imekutwa na kasoro.

Pia miradi 35 ufuatiliaji wake upo hatua za awali, huku miradi mitatu ikiwa katika hatua za kiuchunguzi, baada ya kuonekana kuwa na kasoro kubwa zinazosababisha jinai kwa mujibu wa sheria ya nambari 5 ya mwaka 2023.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Suleiman amesema hayo leo Septemba 18, 2024 wakati wa kikao cha baraza la wawakilishi

Haroun alikuwa akijibu swali mwakilishi wa Kwerekwe Ameir Abdallah Ameir aliyetaka kujua tathmini ya kuziba mianya ya rushwa na hatua zinazochukuliwa.

Amesema miradi hiyo imefanyiwa ufuatiliaji kwa kipindi cha mwaka 2023/24.

Ili kukabiliana na kadhia ya uchafu katika mji wa Zanzibar, kupitia mradi wa Big-Z watapata vifaa maalumu kwa ajili ya usafi.

Vifaa hivyo ni pamoja na gari la kusafisha barabara, makontena 30 ya kubebea taka, magari mawili ya kubebea makontena, magari 11 aina ya Compactor, magari 15 ya wazi, ujenzi wa vizimba vya taka pamoja na maeneo mawili ya kukusanyia taka.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohamed amesema Serikali imeziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya mazungumzo na kampuni zinazosambaza vifaa vya usafi kwa mkopo kupitia njia za kibenki.

Waziri alikuwa kijibu swali la mwakilishi wa Kiembesamaki, Suleiman Haroub Suleiman wakati wa mkutano wa Baraza la wawakilishi aliyetaka kufahamu mikakakti ya kukabiliana na ukosefu wa vifaa vya usafi Zanzibar.

“Vile vile Serikali ipo katika hatua ya kutafuta kampuni zenye sifa na uwezo wa kutoa huduma za usafi katika miji yetu,” amesema.

Matabibu 746 tiba asilia wasajiliwa

Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa zaidi ya asilimia 30 ya watu kutoka katika mataifa yanayoendelea wanatumia tiba asilia na tiba mbadala katika kukabiliana na maradhi ya aina mbali mbali, kisiwani Zanzibar imesajili watabibu nan a wasaidizi wa tiba asili 746.

Naibu Waziri wa Afya, Hafidh Khamis amesema baraza la Tiba asili limesajili kliniki za tiba asili 54, kliniki za tiba mbadala sita, maduka ya dawa asili 238, maghala mawili ya kuhifadhia dawa asili.

Ametoa kauli hiyo barazani leo na kuongeza kuwa Serikali kwa mujibu wa Sheria namba 8 ya 2008 pamoja na muongozo, hutumia usajili wa mwaka 2009 humtaka kila mtoa huduma za tiba asili na tiba mbadala kufuata taratibu, baada ya mhusika kuomba na kufanyiwa ukaguzi kuona iwapo anakidhi vigezo.

Ikiwa ni mdau wa kutoka Tanzania bara atalazimika kuwa na kibali cha Baraza la Tiba asili Tanzania bara au mdhamini ambaye ni mtabibu wa tiba asili aliyesajiliwa Zanzibar.

“Kwa wataalamu wa tiba mbadala watalazimika kuwasilisha vyeti vya taaluma zao kulingana na huduma zao,” amesema.

Related Posts