Madrid kufanya kufuru mpyaa! | Mwanaspoti

MOTO wa Real Madrid hii unatosha au hautoshi? Basi kabla hujafikiria chochote, miamba hiyo ya Bernabeu, huenda ikawa kwenye mwonekano tofauti kabisa wa Galacticos mpya msimu ujao.

Miamba hiyo ya Hispania imetumia miaka mitano kujikusanya na kujiweka pazuri kifedha na sasa ipo tayari kuanza kutumia kwa kuleta mastaa wa maana kabisa kwenye kikosi chao kwa ajili ya matumizi ya msimu wa 2025-26.

Ripoti zinafichua, staa wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold amewekwa kwenye namba moja katika orodha ya mastaa ambao Los Blancos itahitaji kuwa nao kwenye kikosi chao, wakimtazama Mwingereza huyo kama mrithi sahihi kabisa wa Dani Carvajal kwenye beki ya kulia.

Alexander-Arnold, 25, mkataba wake huko Anfield utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, kwa maana ya dirisha la majira ya kiangazi la mwakani, hivyo atakuwa huru kuzungumza na kusaini mkataba wa wawili na klabu ya ng’ambo wakati dirisha la Januari litakapofunguliwa.

Mabingwa hao wa Hispania wana mpango pia wa kuboresha safu yao ya kiungo huku matamanio yao ni kumnasa kiungo wa Kihispaniola, anayekipiga kwenye kikosi cha Manchester City, Rodri.

Kutokana na Man City kukabiliwa na mashtaka 115 yanayohusu kukiuka kanuni ya usawa kwenye matumizi klabuni hapo, kwa maana ya ulingano wa mapato ya matumizi, hilo linaweza kumsukuma mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania kubadili timu mwishoni mwa msimu.

Rodri, 28, ameripotiwa anataka kurudi nyumbani kwao Hispania wakati bado akiwa kwenye kiwango bora cha soka lake na Real Madrid wanamtazama kama mchezaji mwafaka wa kwenda kurithi buti za Toni Kroos.

Real Madrid inayonolewa na Mtaliano, Carlo Ancelotti inahitaji pia beki wa kati mpya baada ya Nacho kutimkia zake Saudi Arabia na kwenye hilo, jina linalodaiwa kuwekwa ubaoni ni la beki Mfaransa anayekipiga kwenye kikosi cha Arsenal, William Saliba.

Mchezaji mwingine ambaye wamekuwa wakimfukuzia kwa muda mrefu, Alphonso Davies naye anaweza kwenda kujiunga na Real Madrid bure kabisa kutokana na mkataba wake huko Bayern Munich kuelekea ukingoni na hakuonekani kuwapo na mpango wa kusaini dili jipya la kuendelea kubaki huko Allianz Arena. Usajili huo ukifanyika basi Real Madrid itakwenda kuwa na mwonekano tofauti kabisa kwenye ligi za msimu ujao.

Alexander-Arnold atakwenda kucheza kwenye beki ya kulia, wakati beki ya kushoto atakuwa Davies huku Saliba akisimama na Antonio Rudiger kwenye beki ya kati kumlinda kipa Thibaut Courtois.

Rodri atakuwa kwenye kiungo sambamba na Eduardo Camavinga na Jude Bellingham kutengeneza utatu matata kabisa, huku kwenye fowadi yao, kocha Ancelotti atakuwa na huduma ya Kylian Mbappe, Vinicius Junior na Endrick.

Related Posts