LHRC yatoa kauli kukamatwa kwa ‘Boni Yai’

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa wito kwa Jeshi la Polisi kufafanua tuhuma zinazomkabiliĀ  aliyekuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob maarufu Boni Yai na kuhakikisha uchunguzi unafanywa kwa uwazi, huku sheria ikifuata mkondo wake.

Pia kimetaka sheria na taratibu zizingatiwe katika mchakato wa ukamataji, ili kupunguza taharuki kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema hayo katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano Septemba 18, 2024.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime katika taarifa aliyoitoa leo Septemba 18, 2024 amesema Jeshi hilo limemkamata na linamshikilia Jacob, mkazi wa Mbezi Msakuzi, jijini Dar es Salaam kutokana na makosa ya kijinai anayotuhumiwa nayo.

Misime amesema katika taarifa hiyo wananchi wapuuze uwongo unaosambazwa mitandaoni kuwa ametekwa.

Boni Yai amekamatwa leo Septemba 18, akiwa maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa wakili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Hekima Mwasipu anayemwakilisha Jacob, ambaye ni kada wa chama hicho.

Henga kwa upande wake amesisitiza kufuata sheria kama zinavyoeleza wazi taratibu sahihi za ukamataji na uwasilishaji wa watuhumiwa mbele ya vyombo vya sheria.

Amesema taarifa walizopata kupitia mashuhuda na mawakili wa Jacob wamedai ukamataji uliotumika haukuzingatia taratibu zote za kisheria hivyo kuzua taharuki.

“Huu ni mwendelezo wa matukio ya ukamataji usiozingatia taratibu za kisheria ambao umekuwa ukiongezeka kwa kasi bila mamlaka husika kutoa ufafanuzi wa kina pindi tu yanapojitokeza,” amesema.

Henga amesema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia ambayo kila raia ana haki ya kuishi kwa amani na kujieleza bila hofu.

Related Posts