Wenza wa marais zaidi ya nchi 15 kujadili afya ya uzazi, mtoto Tanzania

Dar es Salaam.  Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa Kimataifa wa 11 wa Merck Foundation Afrika Asia Luminary 2024 utakaowakutanisha wake wa marais wa Afrika kutoka nchi zaidi ya 15 wakiwa wageni rasmi na wasemaji wakuu.

Mbali na wenza hao wa marais, vilevile utawakutanisha mawaziri, watunga sera, wataalamu, watoa huduma za afya na waandishi wa habari kutoka nchi zaidi ya 70 zinazozungumza Kiingereza, Kihispania, Kifaransa na Kireno.

Mkutano huo wa kwanza kufanyika Tanzania, utaangazia masuala muhimu kama vile afya ya uzazi na mtoto, magonjwa yasiyo ya kuambukiza na mipango inayolenga kujenga uwezo katika sekta ya afya kote Afrika na Asia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Septemba 18, 2024, Waziri wa Maendeleo, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum wa Tanzania, Dk Doroth Gwajima amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua mkutano huo kama mgeni rasmi ambao utaanza Oktoba 29 hadi 30, 2024.

“Mkutano huo utafanyika kwa njia mseto, ukijumuisha ushiriki wa ana kwa ana na mtandaoni kwa zaidi ya watoa huduma za afya 6,000, watunga sera, wataalamu, watafiti, na wawakilishi wa vyombo vya habari vya afya kutoka nchi zaidi ya 70 barani Afrika, Asia, na kwingineko.

“Siku ya kwanza, kikao cha ufunguzi kitafanyika kikihusisha mjadala wa ngazi ya juu na wake wa marais wa Afrika,” amesema Dk Gwajima.

Amesema siku ya pili, vipindi vitano vya kimatibabu na kisayansi vitafanyika vikijadili mada kama vile onkolojia, kisukari, shinikizo la damu, huduma ya uzazi, na uimarishaji wa uwezo wa tiba.

Aidha, fani nyingine kama vile huduma za kupumua, huduma za dharura za watoto na watoto wachanga, na zaidi.

Pia kutakuwa na kikao cha kuhamasisha jamii, mafunzo ya afya ya Merck Foundation kwa waandishi wa habari wa Afrika.

Amesema kikao kitasisitiza jukumu muhimu la vyombo vya habari katika kuhamasisha jamii na kuleta mabadiliko ya kitamaduni kuhusu masuala ya kijamii na afya kama kuacha unyanyapaa wa utasa, kusaidia elimu ya wasichana, kusitisha ukatili wa kijinsia, kukomesha ndoa za utotoni na ukeketaji wa wanawake, kukuza wanawake, na uhamasishaji wa kisukari na shinikizo la damu.

“Washiriki watapata maarifa na uzoefu kutoka kwa wataalamu na watafiti ambao watachimba kwa kina mada kwa lengo la kuongeza uelewa wa umma kuhusu huduma za afya, ikiwa ni pamoja na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, magonjwa ya kupumua, na changamoto nyingine za afya,” amesema.

Amesema kilichofanya Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo mbali na amani na utulivu, pia imetokana na juhudi za Serikali katika kuwekeza kwenye sekta ya afya, hususan katika afya ya mama na mtoto ambazo imefanya Tanzania itekeleze malengo ya kimataifa kama vile Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Akifafanua zaidi faida ya mkutano huo kwa Tanzania, waziri huyo amesema utakuza utalii kwani washiriki wataenda katika maeneo ya kiutalii yaliyopo nchini, kutangaza amani iliyopo, kuongeza pato la nchi kuitangaza kimataifa.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Merck Foundation na Mwenyekiti wa Merck Foundation Africa Asia Luminary, Dk Rasha Kelej, amesema wana furaha kushirikiana na Serikali ya Tanzania, huku akisema watajadili namna ya kuboresha huduma za wagonjwa na kuongeza uelewa juu ya masuala mengi nyeti na muhimu ya kijamii na afya.

“Tutazingatia utetezi wa kuwawezesha wanawake, kusaidia elimu ya wasichana, na kushughulikia unyanyapaa unaohusiana na uzazi. Pia tutasisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa huduma za afya barani Afrika.”

“Tumetoa ufadhili wa masomo 62 kwa madaktari wa Tanzania katika fani 42 za matibabu na utaalam muhimu.  Zaidi ya hayo, tumetoa ufadhili wa masomo kwa wasichana 45 kutoka Tanzania na Zanzibar,” Dk Kelej amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Merck Foundation na Mwenyekiti wa zamani wa Bodi ya Utendaji ya E. Merk KG, Profesa Frank Stangenberg-Haverkamp amebainisha taasisi ya Merck imetoa zaidi ya ufadhili wa masomo 2,000 kwa madaktari kutoka nchi 52.

“Kwa msaada wa serikali za Afrika, tumekuwa tukichagua madaktari na kuwapa mafunzo maalum katika nyanja kama vile saratani, uzazi, kisukari, na kuwawezesha kuhudumia nchi zao katika maeneo haya muhimu,” amesema.

Aidha, amesisitiza elimu kwa watoto wa kike ni suluhu muhimu katika kupambana na ndoa za utotoni, utasa, ukatili wa kijinsia na changamoto nyinginezo.

Related Posts