73 wapenya, kuchuana kanda tatu za Chadema

Dar es Salaam. Watia nia 73 wameteuliwa na Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwania nafasi mbalimbali katika kanda tatu za chama hicho.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya usaili wa watia nia 79 kutoka Kanda ya Pwani inayoundwa na mikoa ya (Dar es Salaam na Pwani), Kusini (Mtwara, Ruvuma na Lindi) na ya Pemba (Kaskazini Pemba na Kusini Pemba) uliofanyika jana Septemba 17, 2024.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema leo Septemba 18 kuwa, kati ya watia nia 79 ni 73 walioteuliwa.

“Kamati Kuu iliyoketi kwenye kikao chake cha kawaida Septemba 17 na 18 jijini Dar es Salaam imeteua wagombea 73 kati ya 79, sasa wataruhusiwa kugombea  nafasi mbalimbali katika kanda za Pemba, Kusini na Pwani,” amesema.

Mrema amesema Kamati Kuu ikiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe imefanya uteuzi huo kwa mujibu wa Katiba ya Chadema ibara ya 7.7.16 (s) Kuteua wagombea wa Uenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Mtunza Hazina wa Kanda.

“Baada ya uteuzi, Kamati Kuu itatangaza tarehe rasmi ya kufanyika kwa uchaguzi wa kanda hizo hapo baadaye, baada ya kumaliza vikao vinavyoendelea,” amesema.

Amesema katika kanda zote walioomba nafasi ya uenyekiti na makamu wote wamepenya, akieleza sita walioenguliwa kuendelea na mchakato huo hawakukidhi vigezo kulingana na nafasi walizoomba.

Waliopitishwa Kanda ya Pwani ni uenyekiti, Boniface Jacob na Gervas Lyenda, huku makamu mwenyekiti ni Shekh Ally Mohamed ‘Kadogoo’ na Baraka Musa.

Kusini kwa nafasi ya uenyekiti ni Aden Mayala, Nicholaus Mapunda na Dk Mahadhi Mmoto, upande wa makamu ni Belchomas Ponera, Kastor Mmuni, na Shaban Mbaruku.

Kanda ya Pemba uenyekiti ni Omar Othman Nassor na Nuhu Jafar Khahamis. Makamu mwenyekiti ni Time Ali Suleiman na Rukia Abuu Mohammed.

Related Posts