Pwani. Shirika la Kimataifa la Sightsavers limesema mila potofu au uoga umechangia watu kutotoa ushirikiano wanapobainika kuwa na ugonjwa wa vikope, umesababisha baadhi yao kuwa vipofu.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Septemba 18, 2024 na meneja miradi wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele (NTDs), Peter Kivumbi alipokutana na mmoja wa wanafamilia ya Kifalme ya Uingereza, Sophie Helen alipotembelea kituo cha Mlandizi kilichopo mkoani Pwani kuangalia utekelezaji wa miradi inayosaidia kutokomeza magonjwa hayo, ikiwemo vikope.
Amesema wanapokutana na wagonjwa wenye tatizo la vikope, baadhi yao wana mila potofu, wakiamini watakapofanyiwa upasuaji, jicho husika haliona tena.
Amesema ili kukabiliana na tatizo hilo, wanapokutana na watu wenye mila potofu au wale wanaogopa kufanyiwa upasuaji wa jicho lenye ugonjwa huo, wanakuwa na mtu maalumu ambaye kazi yake anatoa ushauri nasaha, ili wakubali matibabu hayo.
“Kwa sababu madhara yake ni makubwa, mtu akifikia hatua ya kupata ugonjwa wa vikope utaona kope za macho zinajikunja ndani ya kioo cha jicho, asipopatiwa matibabu kipindi hicho anakuwa kipofu,” amesema Kivumbi.
Pia amesema mazingira ya inzi ni machafu, mara nyingi ugonjwa huo unapatikana maeneo ya changamoto ya maji na mazingira machafu.
Kivumbi ametolea mfano jamii zinazoishi na mifugo ni rahisi kuambukizwa vimelea vya inzi huyo na maeneo ambayo hayana vyoo.
Amesema ili kijikinga na ugonjwa huo, ni muhimu kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na watu wanatakiwa kunawa uso, ili kuepusha inzi asitue kwenye macho na kuacha vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa vikope.
Amesema wananchi wanapoona dalili hizo waende vituo vya afya kwa kuwa matibabu yanatolewa bure, ikiwemo upasuaji. Kwa sasa tiba hiyo wanaifanya katika mikoa ya Pwani, Lindi na Ruvuma na kwamba Morogoro na Manyara wameshatoa huduma hiyo.
Mkazi wa Kikongo, Ally Mohamed amesema baada ya kwenda hospitalini hapo amegundulika ana ugonjwa wa vikope na atafanyiwa upasuaji wa jicho la kulia.
“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuona watu wa hali ya chini, nimetibiwa hapa sijatoa hela yeyote na siku ya kufanyiwa upasuaji nitafanyiwa bure,” amesema Mohamed.
Daktari wa upasuaji wa macho katika kituo cha afya Mlandizi, Azaria Mohamed amesema wamewafanyia upasuaji wa ugonjwa wa vikope watu 29 ambao sasa wanaendelea na shughuli zao.
“Kuanzia Februari mwaka huu tumewafanyia upasuaji watu 29, hivyo nawaomba wananchi wasiogope kufanyiwa upasuaji kwa kuwa upasuaji ni mdogo, tunafanya kwa nusu saa na kidonda kinapona haraka ndani ya saa 24. Tukishamfanyia tunafunga jicho plasta, ikifika asubuhi tunatoa kisha mgonjwa anaendelea na dawa ndani ya siku 19,” amesema Dk Zaria.
Mmoja wa wanafamilia ya Kifalme ya Uingereza, Sophie Helen amewashukuru wataalamu wa afya kwa kuwatibu wagonjwa wenye vikope, anaamini ugonjwa huo utatokomea.
“Nimekuja Tanzania kujionea kazi kubwa zinazofanywa na wataalamu wa afya kwa kushirikiana Uingereza na Tanzania, tunategemea kutokomeza ugonjwa wa vikope. Inawezekana kwa kuwa unaleta upofu,” amesema.
Waziri wa Afya, Jenister Mhagama amesema Serikali ya Uingereza imetoa zaidi ya Sh11.8 bilioni ambazo zimesaidia kusomesha wataalamu, kufanya upasuaji.
“Yapo magonjwa mengine ambayo tumekuwa tukifanya nao kazi kama matende, mabusha, minyoo na tumefanya kampeni ambazo zinatusaidia kudhibiti magonjwa hayo, ikiwemo kufanya usafi, kunawa uso na mikono,” amesema Mhagama.