Mwanza/Mbeya. Matukio ya watu kushambuliwa, kujeruhiwa na wakati mwingine kufariki dunia kwa kudhaniwa kuwa ni wezi wa watoto, yameendelea kushika kasi ambapo Msafiri Msekwa (25) amenusurika kushambuliwa na kundi la watu akidhaniwa mwizi wa mtoto.
Msafiri amesema alihisiwa mwizi wa mtoto baada ya kumsaidia mtoto mmoja aliyehitaji msaada wa kufikishwa kwa mama yake.
“Ilikuwa saa 2 usiku wakati nimetoka kwenye mihangaiko yangu, ndipo nikakutana na mtoto mwenye umri kama wa miaka mitatu hivi, akiwa peke yake…aliponiona akanifuata na kuniambia nipeleke kwa mama,” amesema.
Amesema mtoto huyo alivyomuomba ampeleke kwa mama yake, alimuuliza nyumbani kwao ni wapi, lakini alimjibu hapajui bali anaijua sehemu mama yake anapofanyia biashara.
“Nikamuuliza tena sasa nikupeleke kwa mama yako wapi, akasema kibandani, nikamuuliza unapajua akasema ndiyo…ni wapi, akanionyesha kwa ishara ya mkono, basi nikambeba na kuunza kuelekea aliponielekeza.
“Tukiwa tunatembea, huyo mtoto alianza kusinzia akiwa kaniegea begani, inaonekana alikuwa kachoka sana. Sikutaka alale ili anielekeze alipo mama yake, basi nikawa nafanya kazi ya kumrusha rusha ili asilalae…alijitaidi kiasi hadi tulipokaribia kibandani kwa mama yake, akanionyesha ni pale,” amesema.
Msafiri aliyehitimu shahada ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Saut jijini Mwanza, amesema baada ya mtoto huyo kumuonyesha kibanda cha mama yake, alivuka upande wa pili wa barabara ili akamkabidhi, ndipo alijuta kumsaidia mtoto huyo.
“Nilipokaribia kwa mama yake, aliponiona tu nimembeba mtoto wake, bila kuuliza alianza kupiga kelele kuwa nimemuibia mtoto, sababu alikuwa akimtafuta tangu saa 9 alasiri.
“Kitendo hicho kilinishangaza na kupigwa na butwaa nisijue nijibu nini. Akaendelea kupiga kelele na watu walijaa kwa muda mfupi wakaanza kumsikiliza yule mama…kabla hajamaliza kuelezea mumewe alifika na kuuliza yuko wapi huyo mwizi? mke akajibu huyu hapa ndipo mumewe akanisogelea na kuniuliza nimemtoa wapi mtoto waa,” amesimulia Msafiri.
Amesema baada ya baba wa mtoto huyo kuhoji ndipo alipata nafasi ya kuelezea na kumwambia kila kitu na aliposikiliza maelezo yake, alimpiga kofi mkewe kwa kukurupuka na kupiga mayowe kuwa nilikuwa mwizi wa mtoto, kisha baba huyo akamuomba radhi na kumshukuru kumsaidia mtoto wake.
“…watu waliokuwa wamejaa eneo hilo wakaanza kuondoka na mimi nikaondoka. Lakini ukweli tukio hilo liliniogopesha sana, asingekuwa baba wa huyo mtoto sijui kama ningekuwa hai hadi muda huu,” amesema Msafiri.
Meneja wa Shirika la SOS Children’s Villages Mkoa wa Mwanza, John Masenza amesema ikiwa mtu atakutana na mtoto aliyepotea na anahitaji msaada ni vizuri kumfikisha kituo cha polisi, ofisi ya serikali ya mtaa au kanisani na msikitini.
“Kwa ajili ya usalama, ni vizuri akampeleka kituo cha karibu cha polisi, kwa sababu hiyo ni sehemu salama zaidi, sehemu nyingine anaweza kumpeleka ofisi za serikali za mtaa, kata au ofisi yoyote ya serikali iliyopo jirani.
“Kwa kufanya hivyo inaweza kusaidia kwanza yule mtoto akawa salama, lakini na huyu msamaria mwema pia akawa salama kutokana na hiyo changamoto, wakati mwingine uelewa na hisia ni tofauti kwa wazazi au walezi,” amesema John.
Ametaja eneo lingine la kumpeleka mtoto ni kwenye taasisi za dini msikitini, kanisani na ikiwezekana shule.
Kiongozi wa mila, Chifu Soja Mwangove amesema jamii iungane kukemea vitendo hivyo, huku akiwaomba viongozi wenzake wa dini, siasa na mila kukemea tabia hiyo, akieleza ni lazima wananchi warudi nyuma kuangalia wanapokosea na kutopuuza ushauri wanaopewa.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilolo jijini Mbeya, Ezekiel Mwasandube amewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, akiwaasa ni lazima kusikiliza upande wa pili kabla ya kufanya uamuzi.
“Wananchi wasijichukulie sheria mkononi, inapotokea mtoto kaokotwa asishambuliwe aliyemuokota, bali apewe nafasi ya kusikilizwa. Hili ni Taifa letu, tusiishi kama wanyama,” amesema Mwasandube.
Mshauri wa kanisa la Asemblies of God, Gospel Church International, (AGGCI), Askofu Naaman Shauri amesema kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo, mamlaka zichukue hatua na wananchi wasijichukulie sheria mkononi.
Amewaomba viongozi wa dini nchini kila mmoja kwa nafasi yake kusimama imara kukemea vitendo hivyo, akieleza hatua ilipofikia ni kuliaibisha Taifa tofauti na misingi inayoelekezwa na viongozi.
Septemba 11, 2024 saa 8:30 mchana, watu wawili akiwemo mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Lulembela Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Theresia John (18) aliuawa baada ya watu kuvamia Kituo cha Polisi Lulembela wakitaka kuwaua waliodhaniwa kuwa wezi wa watoto.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, chanzo cha vurugu hizo ni baada ya watu wawili kuonekana wakiwa wamebeba watoto wawili na wananchi waliokuwa kwenye mnada wa Lulembelea kuwahisi kuwa ni wezi wa watoto na kuanza kuwashambulia.
Pia, katika taarifa aliyoitoa Agosti 31, 2024, Misime alisema matukio ya watu kushambuliwa wakisingiziwa ni wezi wa watoto yametokea matatu, tukio la kwanza lilitokea Agosti 14, 2024 saa 11 jioni katika Kijiji cha Bargish, Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara ambapo Kurwa Kabata (38) alijeruhiwa kwa kushambuliwa na wananchi sehemu mbalimbali mwili hadi kulazwa hospitalini.
Alisema tukio la pili lilitokea Agosti 16, 2024 saa 3 usiku katika Kijiji cha Sharmo, Wilaya Babati ambapo Mchungaji wa Kanisa la Hema la Utukufu, Joshua Mussa (34) na msaidizi wake, Joseph Athuman (29) walishambuliwa na wananchi wakidhaniwa ni wezi wa watoto, kisha kuchomewa moto gari waliyokuwa nayo baada ya kulazimika kusimama kijijini hapo gari lao lilipoishiwa mafuta wakitokea kwenye mkutano wa injili.
Tukio lingine lilitokea Agosti 25, 2024 saa 10:30 jioni katika kijiji cha Maghang, Wilaya ya Mbulu ambapo wakazi wa Jiji la Arusha, Antony Francis (44), Anold Jackson (37) na Mina Sekibaha (36) walishambuliwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali mwilini na gari walilokuwa wakitumia kuchomwa moto na wananchi waliojichukulia sheria mikononi wakidhani ni wezi wa watoto.
“Tukio hilo lilitokea baada ya gari walilokuwa wanatumia kupata pancha wakati wakitokea kwenye sherehe ya harusi ya ndugu yao iliyofanyika katika Kijiji cha Kidarafa, Wilaya ya Mkalama mkoani Singida. Watuhumiwa 10 walikamatwa baada kuhusishwa na tukio hilo,”alisema Misime
Katika taarifa yake hiyo, Misime aliwataka wananchi kuacha tabia hiyo, huku akiwasihi kutoa taarifa kwa uongozi wa eneo husika au polisi pindi wanapotilia watu shaka kuwa ni wezi wa watoto na siyo kujichukulia sheria mkononi.