TIMU ya soka ya Benja FC imetwaa ubingwa wa michuano ya Tulia Trust Uyole Cup 2024 iliyofikia tamati leo kwenye Uwanja wa Mwawinji, uliopo Uyole Mbeya Mjini.
Benja imetwaa ubingwa huo baada ya kuichapa Mbeya Smart Soccer Academy kwa mabao 5-4 yaliyofungwa kwa penalti baada ya kumaliza dakika 90 zikiwa zimetoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1.
Michuano hiyo imefungwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ aliyekabidhi kombe na zawadi kwa bingwa na washindi wengine.
Mbali na kombe, bingwa huyo pia alizawadiwa kitita cha Sh 5milioni na medali.
Mbeya Smart Soccer Academy iliyomaliza ya pili iliondoka na Sh 3milioni na medali na Rojas FC iliyomaliza ya tatu ikiondoka na kitita cha Sh 2milioni na medali.
Mshindi wa nne, Chipukizi iliondoka na kitita cha Sh1 milioni huku mchezaji bora, kipa bora, mfungaji bora na timu yenye nidhamu kila moja ilizawadiwa Sh 100,000 na kikundi bora cha ushangiliaji kikiuawadiwa Sh 300,000.
Akizungumzia michuano hiyo, Naibu Waziri wa Michezo, Mwinjuma alisema inaongeza hamasa ya soka Uyole.
“Tumeona namna timu zilivyohamasika na ushindani ulivyokuwa mkali hadi leo hii bingwa mpya amepatikana,” alisema Mwinjuma, huku akitoa pongezi kwa waandaaji na wadhamini wa Ligi hiyo iliyofanyika kwa msimu wa nne sasa ikishirikisha timu 32 na kudhaminiwa na Taasisi ya Tulia Trust Chini ya Mkurugenzi wake ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani(IPU), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson.
Michuano hiyo ambayo msimu huu ni wa nne inafanyika chini ya Taasisi ya Tulia Trust inatarajiwa kuongeza zawadi kwa bingwa hadi kuwa mara mbili ya iliyotolewa msimu huu.