Sekta ya huduma inavyoshikilia uchumi wa Zanzibar

Wakati sekta ya huduma imeendelea kubeba uchumi wa Zanzibar na pato la Taifa lilikua (GDP), wadau wanataja maeneo ya kuboresha kuchochea ukuaji zaidi wa sekta hiyo.

Ripoti mpya iliyotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar (OCGS) ya Zanzibar Abstract 2023 inaonyesha ukuaji wa asilimia 12 wa Pato halisi la Taifa la Zanzibar hadi kufikia Sh6.04 trilioni mwaka 2023, ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, karibu nusu ya GDP, sawa na asilimia 46.6 ilitoka kwenye sekta ya huduma.

Ukuaji huo wa pato halisi ulienda sambamba na ukuaji wa pato la mtu mmoja lililofikia Sh3.11 milioni kwa kipindi husika kutoka wastani wa Sh2.86 milioni kwa mwaka 2022.

Hata hivyo, pato la Taifa la mwaka 2023 kwa thamani ya bidhaa za mwaka 2015 ni sawa na Sh3.75 trilioni ambayo ni ongezeko kutoka Sh3.5 trilioni mwaka uliotangulia. Ukuaji huu ni sawa na asilimia 7.4.

Uchangiaji wa sekta ya huduma katika pato la Taifa la Zanzibar unatajwa kuchochewa na shughuli za utalii ambao unafanya vizuri, ambapo ongezeko la watalii limeendelea kushuhudiwa kila mwezi.

Uchangiaji wa Sekta hii ya huduma unafuatiwa kwa karibu na sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi inayobeba asilimia 24.9 ya Pato lote la Taifa, ikizitangulia sekta za viwanda iliyo na asilimia 20.8 na kodi ya bidhaa yenye asilimia 7.8.

Akizungumzia suala hilo, mchambuzi wa masuala ya Uchumi, Dk Balozi Morwa alisema ili kuendelea kuingiza fedha nyingi na kusisimua sekta ya huduma, ni vyema Zanzibar ikaendelea kufanya uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa utalii.

Akitolea mfano, alisema Zanzibar inazo fukwe ambazo bado hazijatumiwa kikamilifu, zinazoweza kutumika kuvutia wageni wengi na endapo uwekezaji ukifanyika kikamilifu fedha nyingi za kigeni zinaweza kuingizwa.

Alisema ni vyema fukwe hizo ziwekwe katika namna nzuri na ikiwezekana kama nchi ijifunze kwa wengine ambao wamefanya vizuri katika eneo hilo kwa kuangalia kitu walichokifanya na huku hakijafanyika

“Zetu bado zimekaa kiajabu ajabu, tuziweke katika hali nzuri ili ziweze kushindana na nyingine,” alisema Dk Morwa.

Mtaalamu wa uchumi na biashara, Oscar Mkude alisema huduma nyingi zinazotolewa Zanzibar ni mnyororo wa thamani katika sekta ya utalii, hivyo ni vyema kuangalia uboreshaji unapofanyika uwe ni ule unaoweza kuvutia watu wengi zaidi.

Alisema kuendelea kuja kwa watu hao ndiyo namna unavyoweza kuchangamsha sekta ya huduma mbalimbali ili kuongeza mapato na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Hata hivyo, Mkude alionya kuwa ni vyema kuangalia namna nyingine ambayo kama nchi inaweza kujiingizia kipato badala ya kutegemea eneo moja pekee, kwani ikitokea kitu kinachoweza kuathiri utalii inaweza kusababisha kuyumba kwa uchumi.

Alitolea mfano wa kipindi cha Uviko-19 namna ambavyo nchi nyingi zilifunga huduma na baadhi ya ndege kusitisha safari zake, jambo ambalo lilifanya watalii washindwe kusafiri.

“Sasa mbali na kuangalia namna nyingine ya kujiingizia kipato unapokuwa unategemea uchumi wa kitalii ni lazima uangalie vitu vingi, hata unapotengeneza sera, angalia ni kwa namna gani watalii wanaweza kuzipokea na ni katika mtazamo gani,” alisema Mkude.

Alisera sera hizo rafiki ni vyema kuangalia zaidi watalii wadogo wadogo ambao hutunza akiba ya fedha zao kwa miezi kadhaa kabla ya kufanya safari, kwani wao ndio wengi ikilinganishwa na walio na ukwasi mkubwa ambao wanaweza kwenda sehemu yoyote wanayojisikia.

“Hawa watalii wadogo ndio wengi na ndio wa kuwaangalia kwa makini na kujua namna ya kuwalinda, mazingira yanayowekwa yanawalinda vipi na sera zinazowekwa zitawavutia kiasi gani,” alisema Mkude.

Haya yanasemwa wakati ambao, Zanzibar ilirekodi ongezeko la wageni wa kimataifa hadi kufikia 68,223 Julai, 2024 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 16.2 ikilinganishwa na wageni 58,711 waliorekodiwa mnamo Julai 2023.

Ongezeko hilo pia ni ukuaji wa asilimia 32.3 ikilinganishwa na wageni 51,559 waliorekodiwa katika mwezi uliotangulia, yaani Juni 2024.

Wageni kutoka Ulaya waliendelea kuwa vinara kwa kutawala soko hilo kwa asilimia 66.4 ya wageni wote Julai 2024, ambao nchi ya Italia iliongoza kwa kuleta asilimia 11.3 ya wageni wote walioingia Zanzibar kipindi hicho, ikifuatiwa na Ufaransa kwa asilimia 8, Japan ikirekodi chini ya asilimia 1, ambayo ndiyo ndogo zaidi.

Takwimu zinaonyesha, watalii 60,178, sawa na asilimia 88.2 ya wageni wote waliingia kupitia Uwanja wa Ndege, ambapo wageni 56,821 waliingia kwa ndege za kimataifa na 3,357 kwa ndege za ndani. Wageni wengine 8,045 waliingia kupitia bandari ya baharini kwa boti kutoka Tanzania Bara.

Huenda ongezeko hili la watalii, likawa ni kichocheo cha kuwapo kwa uhitaji wa sehemu zaidi za malazi kwa wageni hao jambo ambalo linatumika kama fursa kwa wawekezaji.

Ripoti hii inaonyesha kuwapo kwa ongezeko la miradi mipya iliyosajiliwa hadi kufikia 114 mwaka 2023, ikiwa na thamani ya Sh4.64 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 22.6 kutoka miradi 93 iliyokuwapo mwaka uliotangulia. Katika miradi hiyo, asilimia 38.6 ilikuwa ni kwa ajili ya hoteli na migahawa.

Hata hivyo, ripoti hii inataja baadhi ya maeneo ambayo yamechangia upatikanaji wa fedha hizo katika sekta ya huduma kuwa ni biashara, usafirishaji, elimu, malazi na huduma za vyakula, huduma za kifedha na bima, huduma za afya na jamii, sanaa, burudani.

Katika hili, Dk Morwa alisema kwa Zanzibar ni ngumu kuwa na eneo la kilimo kinachoweza kusaidia kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja, lakini uvuvi ukitumiwa ipasavyo kwa kuweka njia nzuri za uvuvi na kisasa unaweza kunufaisha wengi.

“Mbinu ambazo zinaweza kusaidia kupata samaki wengi, si kwa ajili yetu tu bali kwa ajili ya masoko ya nje, mbinu zinazotumika pia ziwe rafiki ambazo zinakubaliwa katika masoko ya nje, kwani kuna namna ambayo tukivua inaweza kuonekana ni hatarishi kwa baadhi ya watu, hivyo ni muhimu kuzingatia hili,” alisema Dk Morwa.

Kwa upande wake Mkude, alishauri kuwapo kwa mpango mkakati ambao unaweza kuifanya Zanzibar kutembea katika mstari uleule bila kujali mabadiliko ya kiuongozi yanayoweza kutokea ndani ya miaka tofauti.

Hiyo ikiwa na maana kuwa kila kiongozi atakayeingia atatakiwa kuendeleza pale alipoishia mtangulizi wake kwa ajili ya kufikia malengo waliyojiwekea badala ya kuja na kitu chake kipya.

Alitolea mfano wa nchi ya Ireland ambayo pia haina eneo kubwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, kama kilimo namna ambavyo iliamua kujiwekeza katika elimu kwa ajili ya kuzalisha nguvu kazi inayoweza kuuza ujuzi wake maeneo mbalimbali duniani.

“Nchi hii iliamua kufanya elimu ndiyo mwelekeo wao, wakawekeza sana katika ujuzi, ndiyo maana kampuni kubwa kama Google na nyinginezo zina ofisi zao Ireland, walijua kuwa hawawezi kuuza nje mtama, mahindi au korosho kwa sababu ardhi yao si kubwa, lakini katika ujuzi wanaweza kuuza,” alisema.

Alisema jambo kama hilo linaweza kufanyika pia Zanzibar, kwa kuwa na mikakati ya kudumu katika kuinua uchumi wakati ambao tayari uelekeo wa kutaka kuleta mapinduzi ukianza kuonekana baada ya kuzinduliwa kwa Silicon Zanzibar

Alisema hili litawezekana kwa watu wote kukubali kuwa kitu kizuri matokeo yake yataonekana ndani ya muda mrefu na hivyo kuondoa ile dhana ya watu kutaka kuona matokeo ya kitu ndani ya muda mfupi. “Tatizo wengi wetu tunataka kitu kikianza leo kionekane kesho, hasa wanasiasa wamekuwa na sera za muda mfupi kwa ajili ya kuwashawishi watu, ili washinde uchaguzi, matokeo yake inawanufaisha wao lakini inawaumiza wananchi,” alisema Mkude.

Alisema matokeo ya muda mrefu yanashindwa kuleta tija kwa sababu watendaji wanataka kuonyesha matokeo yao ya muda mfupi, hivyo kuwapo kwa mpango mkakati wa kitaifa unaoonyesha uelekeo wa mtu yeyote atakayeingia madarakani ndiyo suluhisho.

“Kuwe na mfumo unaotakiwa kuangalia zaidi mahitaji ya soko na nini kizalishwe kuingia sokoni, wenzetu waangalie namna wanayoweza kutengeneza utamaduni na kuboresha ujuzi, elimu yetu iweze kujibu mahitaji ya leo na kesho na kujenga uchumi wa nchi na mtu mmojammoja,” alisema Mkude.

Related Posts