Umeme jua unavyoweza kumbeba mkulima wa kilimo cha umwagiliaji

Dar es Salaam. Katika jitihada za kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na gharama za uzalishaji kwenye sekta ya kilimo, matumizi ya nishati ya umeme jua hasa kwenye umwagiliaji yanatazamwa kama suluhisho.

Teknolojia hiyo sio tu inapunguza gharama za kilimo, bali inachangia kuongeza uzalishaji wa mazao, hasa katika maeneo yenye ukame na upatikanaji mdogo wa maji.

Tayari Serikali imeeleza kuliona hilo na kuweka kwenye mipango yake mikakati ya kuwawezesha wakulima wa skimu za umwagiliaji kutumia umeme jua kwenye uendeshaji wa mitambo.

Pamoja na uhalisia huo, matumizi ya nishati ya umeme jua katika kilimo cha umwagiliaji nchini, bado hayaridhishi kama inavyoonyeshwa katika utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo ya Kilimo Tanzania (Tari) mwaka 2020.

Matumizi ya mifumo ya umeme jua kwenye kilimo cha umwagiliaji imekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Tari, kwa mwaka huo takribani asilimia 85 ya wakulima wanaotumia mifumo ya umwagiliaji wanategemea pampu zinazotumia mafuta ya dizeli ambayo ni gharama.

Takwimu za Tari, zinaakisi matokeo ya ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2021, iliyoonyesha wakulima wengi wadogo nchini wanaendelea kutumia pampu za dizeli kutokana na gharama ndogo za awali za ununuzi wake, ingawa gharama za uendeshaji kwa muda mrefu ni kubwa zaidi.

Mwaka mmoja baadaye 2022, Benki ya Dunia ilitoa ripoti yake ikionyesha wakulima wanaotumia nishati ya umeme jua katika umwagiliaji ni asilimia 15 pekee nchini.

Ingawa hali iko hivyo, matokeo ya tafiti na ushuhuda wa wakulima unaonyesha matumizi ya nishati ya umeme jua katika kilimo cha umwagiliaji yana tija zaidi kuliko nishati nyingine.

Tija ya umeme jua kwenye umwagiliaji

Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) mwaka 2021, liliweka wazi kuwa kwa kutumia pampu za umeme jua, wakulima wanaweza kupunguza gharama za nishati kwa asilimia 70 hadi 90.

Shirika hilo, kupitia mradi wake wa kilimo cha umwagiliaji wa pampu za umeme jua kwa kilimo endelevu, uliofanywa mkoani Dodoma, ulionyesha wakulima walipunguza gharama za nishati kwa asilimia 80 baada ya kubadili matumizi ya dizeli kwenda kwenye umeme wa jua.

Katika hatua nyingine, Ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu nishati mbadala ya mwaka 2022, inakadiria matumizi ya umeme jua kwenye kilimo cha umwagiliaji yanaweza kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wastani wa asilimia 30 hadi 50.

Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) nalo linaonyesha matumizi ya nishati ya jua katika kilimo cha umwagiliaji yameongeza uwezo wa wakulima kukabiliana na majanga ya hali ya hewa kwa kuboresha upatikanaji wa maji.

Kwa mujibu wa Chama cha Nishati Jadidifu Tanzania (Tarea), mkulima atagharimika Sh3.81 milioni kwa mwaka, kumiliki jenereta linalotumia mafuta kwa ajili ya umwagiliaji katika shughuli za kilimo na litadumu kwa miaka mitatu.

Lakini, kwa mtambo wa umeme jua kwa ajili ya umwagiliaji, unagharimu Sh10 milioni, ambao kiuhalisia unadumu kwa miaka 20.

Tarea inaeleza licha ya gharama kubwa za mwanzo katika usimikaji wa mtambo wa nishati ya umeme jua katika kilimo cha umwagiliaji, kuna unafuu mkubwa baadaye.

Unafuu huo kwa mujibu wa Tarea, unatokana na muda mrefu ambao mtambo wa nishati ya umeme jua unadumu, kadhalika hauhusishi gharama nyingine za uendeshaji, wakati jenereta linahitaji mafuta kila siku na huduma zingine.

Chama hicho kimekwenda mbali zaidi na kueleza, jenereta linalotumia mafuta katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji linazalisha kilo 487 za hewa ya ukaa, ambayo ni hatari kwa mazingira kila siku.

Mbali na tathmini ya Tarea, Anthony Machai mkulima anayetumia nishati hiyo mkoani Dodoma, anasisitiza unafuu wa nishati hiyo katika kilimo, ukilinganisha na mtambo unaotumia mafuta.

Kwa mujibu wa Machai, katika shamba la ekari tatu kwa jenereta utalazimika kununua mafuta ya Sh50,000 kila siku kuwezesha kuvuta maji kutoka kisimani hadi kwenye mazao kwa ajili ya umwagiliaji.

Gharama hizo, anasema kwa mwezi ni sawa na kutumia Sh1.5 milioni, kiasi ambacho ni maumivu kwa mkulima. Lakini unapotumia mitambo ya umeme jua, gharama ni kuifunga tu, baada ya hapo mkulima hatagharimika na chochote.

“Pamoja na mazingira hayo, ni wakulima wachache ndiyo tunaotumia nishati ya umeme jua kwenye kilimo, wengi wanaona afadhali watumie majenereta,” anaeleza.

Kinachochochea wakulima wengi wachague majenereta licha ya faida ndogo wanayopata ni kile kilichoelezwa na Machai kuwa, hawana uwezo wa kufunga mitambo ya umeme jua.

Machai anasema mtambo wa umeme jua unaomudu huduma za shamba la ekari nne hadi tano, unagharimu Sh9 milioni hadi Sh15 milioni.

Anasema ni wakulima wachache wenye uwezo wa kuwa na viwango hicho cha fedha kwa mara moja, ndiyo maana wanachagua kuingia gharama kidogo kidogo kwenye mafuta.

“Ni kweli ukifunga mtambo kwa gharama hizo hautahitajika kutoa gharama nyingine yoyote, lakini ni wakulima wachache wenye uwezo wa kupata kiasi hicho cha fedha kwa mkupuo wafunge nishati hiyo,” anasema.

Kinachopaswa kufanywa, anasema ni Serikali iangalie utaratibu wa kuwawezesha wakulima kukopeshwa mitambo hiyo ili wawe wanalipa kidogo kidogo hadi watakapomaliza.

Kwa sababu anasema gharama za mitambo huo, zinarudishwa kwa awamu moja ya kilimo.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa anasema kinachofanywa na mamlaka hiyo ni kutoa elimu kwa wakulima kutumia nishati ya umeme jua katika shughuli za umwagiliaji.

Sambamba na hilo, anasema mamlaka hiyo imeshaanza mkakati wa matumizi ya nishati hiyo kwa kupendekeza nishati ya umeme jua.

Kwa hatua za awali, anaeleza wameanza kuingiza visima 60 kati ya 1,000 mwaka huu vitakavyotumia nishati ya umeme jua katika umwagiliaji.

“Tumeanza na visima 60 kati ya 1,000 mwaka huu. Tumeyabainisha maeneo tutakayoanza nayo lakini kuna uwezekano wa visima hivyo kuongezeka zaidi,” anasema.

Anasema tayari kazi hiyo imeshaanza na kwamba anaamini itakwenda kukamilika.

Related Posts