Waandishi 17 wa Mwananchi kuwania tuzo za Ejat

Dar es Salaam. Waandishi 17 wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ni miongoni mwa wateule 72 watakaowania tuzo za umahiri za uandishi wa Habari (Ejat) zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Kati ya waandishi 72 watakaoshiriki kinyang’anyiro hicho Septemba 28, 2024 wanaume ni 45, sawa na asilimia 62.5 na wanawake ni 27 sawa na asilimia 37.5.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Septemba 19, 2024, Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura amesema kati ya wateule hao, 14 wanatoka katika runinga, 13 vyombo vya mtandaoni, redio 20  na wateule 25 wanatoka kwenye magazeti.

“Wateule wamepatikana kwa kukidhi vigezo vya ubora ambavyo ni pamoja na ukweli, usahihi, uanuai, haki, kina, utafiti, ubunifu, uvumbuzi, upekee, uchambuzi, uwajibikaji, ufichuaji maovu, uadilifu, uwasilishaji unaoeleweka na uchunguzi,” amesema Sungura.

Pia amesema vigezo maalumu vilitumika kwa kuzingatia aina tofauti ya vyombo vya habari kama vile redio, televisheni, magazeti na habari za mitandaoni.

Kinyang’anyiro cha kumtambua mshindi wa kwanza, wa pili na wa tatu na mshindi wa jumla kwa makundi 20 kitafanyika mbele ya Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson atakayekuwa mgeni rasmi.

Mbali na utoaji wa tuzo hizo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa atazindua Jarida la Tuzo na Tuzo Magazine ambayo yanajikita kuhamasisha umahiri katika sekta mbalimbali Tanzania na nje ya Tanzania.

Majarida hayo ambalo moja litakuwa la Kiingereza na lingine la Kiswahili, yatabeba maudhui ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) ambapo moja ya maudhui katika majarida yote mawili ni simulizi ya maisha ya wateule wote.

“Kazi ya kuandika simulizi hizo inaanza leo, hivyo wateule wote wawe tayari kufikiwa na waandishi wa Jarida la Tuzo wakati wowote kuanzia sasa. Maudhui mengine ni ya wafadhili wa tuzo ambao simulizi zitahusu mchango wao katika kubadilisha maisha ya watu, ikiwemo kukuza na kujenga tasnia ya habari,” amesema Sungura.

Mbali na hilo, Sungura amesema kwa mara ya kwanza kazi za kihabari kwa EJAT 2023 zimeongezeka hadi kufikia 1,135 kutoka kazi 893 za EJAT 2022. EJAT mwaka 2020 zilikuwa kazi 396 na EJAT 2021 kazi zilikuwa 608.

Katika kazi hizo, waandishi wa habari wa Mkoa wa Dar es Salaam wameongoza kwa kuwasilisha kazi 290, wakifuatiwa na Arusha uliokuwa na kazi 81, Mwanza kazi 74, Iringa ilishika nafasi ya nne kwa kuwa na kazi 72.

“Wakati huo Mkoa wa Mtwara ulishika nafasi ya tano kwa kuwa na kazi 49. Kwa upande wa Zanzibar, kazi zilizopokelewa ni kutoka Kaskazini Pemba (36) Pemba Kusini (43) na Mjini Magharibi (29),” amesema Sungura.

Mbali na majina mengine yaliyotajwa, kutoka Mwananchi walioteuliwa ni Jacob Mosenda, Julius Maricha, Eliya Solomon, Zourha Malisa, Harrieth Makwetta na George Helahela.

Wengine ni Elizabeth Edward, Pamela Chilongola, Ephraim Bahemu, Kelvin Matandiko, Haika Kimaro, Yohanna Challe, Mgongo Kaitira, Imani Makongoro, Salome Gregory, Anna Potnus na Hellen Nachilongo.

Akizungumzia uteuzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo kutoka MCL, Rashid Kejo amesema idadi ya waandishi walioteuliwa si ya kubahatisha, bali inatokana na mikakati madhubuti iliyowekwa na kampuni.

Mikakati hiyo ambayo iliwashirikisha wadau mbalimbali, ililenga kuwajenga waandishi kuwa na uwezo wa kutengeneza maudhui mbalimbali ambayo yanalenga kuiwezesha jamii kama dhamira ya kaulimbiu ya kampuni inavyosema ‘Tunawezesha Taifa’.

“Katika hilo tulijikita kuwapa mafunzo ambayo yanalenga kuzalisha maudhui yanayowezesha Taifa, tumeandika na kuleta matokeo, bahati nzuri kazi za uandishi wa habari zinaonekana ni kama mpira wa miguu,” amesema Kejo na kuongeza;

“Ni jambo linalotia moyo sana kuona jitihada zinazofanywa na waandishi kwa kushirikiana na wahariri zinazaa matunda.”

Katika mkutano huo na waandishi, Sungura anabainisha katika siku za usoni, MCT inafikiria kuanza kufanya shughuli zake kidigitali kwa kuanza kufuatilia waandishi na kazi wanazozifanya, ili kuhakikisha kinara anayepatikana anakuwa na uwezo wa kushindana na waandishi wa nchi nyingine.

Hiyo ni kutokana na kuwepo kwa tabia ya baadhi ya waandishi wanaofanya kazi nzuri zilioleta mjadala mkubwa, lakini hawataki kutuma kazi zao kwa hiari.

“Hii ilifanya hata majaji kuhoji juu ya baadhi ya kazi ambazo waliona zina vigezo, lakini hazikuwasilishwa. Kupitia njia hii tutakuwa na uwezo wa kuwatambua, itafika wakati tutakuwa tukitambua waandishi wanaofanya vizuri kila wiki, mwezi, miezi mitatu na baadaye aliyefanya vizuri kwa mwaka mzima,” amesema Sungura na kuongeza;

“Kufanya hivi pia itatufanya kuwa na uhakika kuwa wanaoshinda wanakuwa ni wenye weledi wa kushindana kimataifa,” amesema.

Akizungumzia kazi iliyofanyika, Mwenyekiti wa Jopo la Majaji, Halima Sharrif amesema kazi ilifanyika kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.

Related Posts