Kamanda wa kikosi maalumu cha Akhmat cha Chechnya ambaye pia ni naibu mkuu wa idara ya kijeshi na kisiasa wa wizara ya ulinzi ya Urusi, amesema Urusi imevikomboa vijiji vya Nikolayevo-Darino na Darino.
Vijiji hivyo viko umbali wa takriban kilomita 15 kutoka mistari ya mbele ya vita ya awali iliyoanzishwa na vikosi vya Ukraine mnamo Agosti.
Vikosi vya Urusi vyasonga mbele kuelekea mashariki mwa Ukraine
Alaudinov ameongeza kuwa vikosi vya Urusi pia vinasonga mbele kuelekea upande wa mashariki wa Ukraine.
Soma pia:Mifumo ya ulinzi ya Urusi yadungua droni 54 za Ukraine
Kulingana na jeshi la Urusi, Ukraine imekuwa ikijaribu kuvamia mpaka wa Urusi katika sehemu nyingine kwenye eneo la mashariki ambapo vikosi vya Urusi vinasonga mbele, katika harakati za kugeuza vikosi hivyo kutofanya shambulizi kubwa katika eneo hilo.
Urusi, ambayo inadhibiti takriban 18% ya Ukraine, pia imekuwa ikisonga mbele mashariki mwa Ukraine na siku ya Jumanne, iliuteka mji wa Ukrainsk.
Ukraine yasema imeandaa mpango wa ushindi dhidi ya Urusi
Mbali na hayo, hapo jana wakati wa hotuba yake ya kila jioni kwa taifa, Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky alisema kuwa tayari nchi hiyo imeandaa kikamilifu mpango wake wa ushindi wa kutamatisha vita na Urusi.
Huenda Urusi inakiuka sheria ya kimataifa ya haki za binadamu
Ujumbe wa kufuatilia haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine HRMMU umesema Katika kipindi cha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Urusi imerusha mamia ya makombora na droni katika vituo vya kuzalishaji umeme, usafirishaji na usambazaji nchini Uraine.
Ripoti ya ujumbe huo imesema kuwa wimbi kubwa la kwanza la mashambulio lilifanywa katika msimu wa vuli na baridi wa mwaka 2022, miezi michache baada ya Urusi kuanza uvamizi kamili dhidi ya Ukraine. Mashambulizi hayo yameendelea muda wote wa vita ingawa Urusi imeimarisha mashambulizi yake tangu mwezi Machi.
HRMMU iliangazia ripoti yake katika mashambulizi tisa ya kati ya mwezi Machi na Agosti mwaka 2024 na kusema kuna sababu za kimsingi za kuamini kwamba masuala mengi ya operesheni hiyo ya kijeshi ya kuharibu miundo mbinu ya kiraia ya uzalishaji na usambazaji umeme imekiuka kanuni za msingi za sheria ya kimataifa ya kibinadamu.
Urusi yafanya mashambulizi katika mji wa Sumy nchini Ukraine
Urusi imefanya mashambulizi ya usiku kucha dhidi ya miundo mbinu ya nishati katika mji wa Sumy ulioko kaskazini mashariki mwa Ukraine. Haya yamesemwa leo na shirika linalosimamia gridi ya taifa ya Ukraine Ukrenergo na kwamba shambulizi hilo lilisababisha kukatika kwa umeme kwa muda katika eneo hilo.