KOCHA wa Dar City, Mohamed Mbwana amekiri haikuwa kazi rahisi kwa timu hiyo kupata ushindi mbele ya UDSM Outsiders wakati wakiishindilia pointi 73-60 katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) kwenye Uwanja wa Donbosco Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Dar City inaendelea kuongoza katika ligi hiyo kwa pointi 53, ikifuatiwa na UDSM yenye pointi 52.
Dar City ambao ndio watetezi wa ligi hiyo, imebakiwa na michezo miwili dhidi ya ABC na Mgulani JKT ili ikamilishe michezo 30.
Kocha Mbwana, aliliambia Mwanaspoti, ushindani katika mchezo huo na UDSM ulikuwa ni mkubwa na kuibuka kwao ushindi ni kuwazidi mbinu na ufundi, lakini haikuwa kazi rahisi.
“UDSM ni timu nzuri ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, na siyo timu ya kuibeza,” alisema.
Katika mchezo huo, mchezaji Josephat Peter wa Dar City alikuwa kivutio katika mchezo huo kutokana na kiwango kikubwa alichoonyesha.
Peter anayecheza nafasi ya ‘pointi gurd’ aliingia uwanjani dakika 12 ya robo ya tatu na kuibadilisha timu yake iliyoanza kupotea katika robo hiyo .
Katika mchezo huo Peter alifunga pointi 18, akifutiwa na Swalehe Burhan aliyefunga pointi 13, huku kwa upande wa UDSM kinara alikuwa Tyrone Edward aliyefunga pointi 18, huku Ally Faraji akifunga pointi 10.