Bukoba. Mwili wa mtoto Rwegasira Jackson (14), aliyezama akiogelea Ziwa Victoria katika fukwe za Gymkana, Manispaa ya Bukoba, Mkoa wa Kagera, umepatikana kando mwa Mwalo wa Bunena ukiwa umeharibika.
Mtoto huyo alizama katika ufukwe huo Jumapili ya Septemba 15, 2024, alipokuwa amekwenda na rafiki yake na tangu siku hiyo jitihada zilikuwa zikifanyika za kumtafuta baina ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na wavuvi wa eneo hilo.
Leo Alhamisi, Septemba 19, 2024, Ofisa Habari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa Kagera, Shaaban Mussa akizungumza na Mwananchi, amesema mwili wa mtoto huyo umepatikana baada ya kushirikiana na wavuvi.
“Naomba tusiruhusu watoto kwenda kiholela ziwani hata watu wazima tuache tabia hizo kuna majanga mengi yanaweza kutokea,” amesema Mussa.
Mmoja wa wavuvi Mwalo wa Bunena, Datius Wilson amesema baada ya kupokea taarifa za mtu kuzama aliwaambia wenzake wakaanza kukagua kila siku kwenye kando za mwalo.
Amesema jana Jumatano waliitwa na mvuvi mwenzao kuwa kuna harufu sehemu fulani walipofika wakakuta mwili huo unaelea.
Mkazi wa mtaa wa Kafuti, Kata Bakoba, Kelvin Mwijage amesema jana Jumatano saa 12 asubuhi baada ya kufika mwaloni alichukua mtumbwi wake na kuanza kuelekea ziwani kwenda kuweka mitego ya samaki na alipopita katika mojawapo ya fukwe hizo alihisi harufu mbaya.
“Niliwaita wenzangu baada ya kuhisi harufu mbaya ya kitu maana nilikuwa nakumbuka kuwa kuna mtu alizama majini siku nne hajapatikana, hivyo tulipofika tukakuta ni mwili wa binadamu tukaujulisha uongozi kisha Zimamoto wakaja na kuuchukua mwili huo,” amesema.
Kwa upande wake, Agripina Wiston amabaye ni dada mlezi wa Rwegasira, Mkazi wa Buyekela, Kata Bukoba, amesema Julai, 2024 mtoto huyo alimuomba kwa wazazi wake kijijini kwao ili amlete mjini kwa ajili ya kumsaidia kazi za kuuza vyombo mtaani kwa kutembeza (Machinga).
Amesema Jumapili ya tukio alimuaga anakwenda mjini kudai fedha kwa wateja wake na ilipofika alasiri ya siku hiyo alirejea nyumbani na kuomba kutoka kwenda kutembea na rafiki yake.
Amesema baadaye yeye (Agripina) alipokwenda fukwe ya Gymkana alimkuta kijana aliyemweleza kuwa maji yamempeleka Rwegasira.
Awali, Diwani wa Bakoba, Shaaban Rashid amesema jamii inashindwa kuweka ulinzi wa kutosha wa watoto kwani kwa hali ilivyo sasa wanasambaa ufukweni huku akiiomba Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwakamata watoto na kuwawajibisha wazazi ambao wameshindwa kuwalinda.