Punguzo lenye neema kwa benki, Serikali na wananchi

Sekta ya huduma za fedha ni miongoni mwa zinazokua kwa kasi hapa nchini, huku ujumuishi wa watu katika huduma hizo muhimu za kiuchumi ukiongezeka.

Miongoni mwa huduma zilizojumuisha Watanzania wengi katika huduma za kifedha ukiachilia mbali miamala ya simu ni huduma za kibenki, hata hivyo utitiri wa makato ni kikwazo kikubwa kwa watu.

Hatua ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupunguza makato baina ya wateja wanaotuma fedha kutoka benki moja kwenda nyingine, wachumi wamesema itachochea watu kutumia mifumo rasmi ya fedha.

Loading...

Loading…

Mbali na hayo, wamesema itakuza upatikanaji wa fedha kwenye sekta hiyo, wakisisitiza miamala kupitia benki kwa kiasi kikubwa ina faida kwa usalama wa mtu na taifa kwa ujumla.

BoT kupitia taarifa yake ya Aprili 22 mwaka huu, ilitangaza ukomo wa makato baina ya miamala ya wateja kutoka benki kwenda benki kupitia Mfumo wa Taifa wa Kidijitali wa Malipo ya Papo kwa Hapo (TIPS) na Tanzania Automated Clearing House (TACH).

Kwa mujibu wa Naibu Gavana wa BoT, Sauda Msemo ambaye alitangaza hatua hiyo, BoT ilibaini makato makubwa wanayokatwa wateja wakati wa kutuma fedha benki moja kwenda nyingine kwa njia za rejareja, jambo ambalo linamuongezea mzigo mteja.

Akizungumza na Mwananchi, Gavana wa Benki Kuu, Emanuel Tutuba anasema kupunguzwa kwa makato ya benki ni miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi.

“Kwenye miamala gharama inaposhuka watu wanashawishika kutumia mifumo ya kielektroniki, mwaka huu Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alizindua mfumo wa TIPS, lengo la mfumo huo ni kupunguza gharama,” anasema.

Tutuba anasema kila inapotokea uwezekano wa kupunguza gharama wataendelea kufanya hivyo na sasa wanaendelea na tafiti ‘study’ kuangalia gharama za uendeshaji za benki kuona namna ya kupunguza gharama nyingine.

Kuhusu hatua hiyo, Mwenyekiti Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi anasema benki zinaunga mkono na watatekeleza. “Hii itakuwa na matokea chanya kuongeza watu wanaotumia mifumo rasmi ya kifedha.”

Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka anasema kupunguzwa kwa gharama hizo kutarahisisha huduma za kifedha.

Anasema kwenye miamala ya simu mtu anaweza kutuma fedha kwa gharama nafuu zaidi, hivyo hiyo ni hatua ya kuwaunganisha wadau.

“Kumekuwa na gharama kubwa, kwa hiyo hatua hii inakuja kutoa urahisi kwa wateja mbalimbali na kuongeza watu kutumia mifumo rasmi ya fedha,” anasema.

Dk Mwinuka anaongeza kuwa kwenye jamii kumekuwa na vikundi vingi vya kukopa na kuweka fedha na si zote zinatumia njia rasmi, hivyo kupunguzwa kwa gharama kutawavutia wateja wapya.

Mchambuzi mwingine wa uchumi, Oscar Mkude anasema miamala baina ya benki kwenda benki ndani ya nchi inapaswa kuwa gharama rahisi.

Anasema BoT kupitia mfumo wa TIPS wameweka mfumo ambao muamala ukifanyika utakuwa chini ya mfumo, hivyo gharama za kufanya miamala hazitatofautiana baina ya benki moja na nyingine.

“Gharama za kutuma miamala hazipaswi kutofautiana, sasa kwa sababu benki zote zitakuwa chini ya mfumo ambao unaratibu malipo yote, benki hazitakuwa na sababu ya kutoza gharama kubwa kuliko nyingine,” anasema.

Mkude anasema faida ya kushushwa kwa gharama hizo itasaidia gharama za miamala kushuka.

Anasema pamoja na benki kuwa zinapata faida kubwa, lakini malalamiko ya wateja ni makato makubwa wanayotozwa kwenye benki hizo.

Jambo analosisitiza Mkude, alisema wanaotumia benki ni wale wenye akaunti ya benki, ni chini ya asilimia 10 lakini wanafikiwa na huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.

Mkude anagusia eneo lingine lenye makato makubwa kuwa ni kuhamisha muamala kutoka kwenye simu kwenda benki ambayo nayo ni maumivu.

“Kwa nini iko hivyo, ni kwa sababu miamala kwa njia ya simu kuna watu wengi wanaowezesha miamala kukamilika, sasa kuna haja nayo kuangalia yaliyofanyika kwenye benki iingie kwenye simu, hii itasaidia nia ya Serikali ya kutaka kuona miamala inafanyika kidijitali,” anaeleza.

Hoja hizo zinaungwa mkono na Mchambuzi wa masuala ya uwekezaji, Dk Onesmo Kyauke akisema manufaa ya kupunguzwa kwa makato hayo kutaongeza matumizi ya njia za kielektroniki kwenye utumaji wa miamala.

“Dunia inaelekea kwenye uchumi usiohusisha fedha taslimu, ndiyo maana Serikali imepunguza mapato kwenye malipo kwa njia ya simu,” anasema.

Profesa wa Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Abel Kinyondo akizungumzia hatua hiyo ya BoT, anasema faida ya hatua ipo kwenye benki, Serikali na wananchi wa kawaida.

Anasema kupunguzwa kwa gharama hizo kunamwezesha mwananchi wa kawaida kufanya miamala kwa kutumia huduma za kibenki.

“Moja ya sababu zilizokuwa zinawafanya wananchi kutotumia huduma za kibenki ni tozo zilizopo, unapopunguza gharama maana yake unamfanya mtu wa kawaida kuona benki kuwa njia rahisi ya kutumia kutokana na usalama wake,” anasema.

Usalama wa benki anaoutaja Dk Kinyondo ni tofauti na njia nyingine ambazo ni rahisi mtu kuibiwa akitoa hela, akituma au kubeba mkononi.

Uwezekano wa mtu anayefanya miamala baina ya benki na benki kuibiwa ni mdogo, kama anavyosema Profesa huyo wa uchumi, akisisitiza benki ni salama.

Jambo lingine, Profesa Kinyondo anasema mtu anapokuwa na akiba kwenye benki ni rahisi kukopeshwa kutokana na kutambulika na miamala yake kuonyesha uwezo kama mkopo atakaopewa anaweza kulipa.

Kwa upande wa benki, anasema watu wanapoweka fedha benki kwa kiwango kikubwa maana yake benki zinakuwa na uwezo wa kukopesha zaidi na kuchangamsha uchumi.

Pia Serikali itakuwa na uwezo, kama Serikali inafanya miamala yake kupitia benki itakuwa na uwezo wa kufuatilia malipo yanayofanyika.

“Serikali ikiweza kujua nani kamlipa nani, mambo mawili yanawezekana, jambo la kwanza ni kuweka kodi kwa sababu itajua mtu husika ana kiwango gani na imemlipa nani kiwango gani,” anasema.

Hayo yote Profesa Kinyondo anasema yatawezekana kama watu wote wataona unafuu wa kuweka fedha zao benki.

Hoja yake ya pili, ni suala la usalama, akisema zipo fedha watu wanaweza kufanya matumizi kwa njia isiyo sahihi, ikiwemo kununua dawa za kulevya, kutuma hela kwa magaidi.

Fedha hizo anasema haziwezi kujulikana matumizi yake kama zinapita njia nyingine za kifedha, akitaja njia ya benki inaweza kuonyesha ilipokwenda na matumizi yake yakoje.

Kwenye benki kuna mifumo ambayo kisheria inatakiwa kutoa taarifa BoT kama miamala inayotiliwa shaka.

Mfano kwenye benki yangu nina Sh10,000 na kila siku inaingia Sh1,000 hadi Sh2,000, siku kwenye akaunti hiyo ikiingia Sh1,000,000 hiyo benki inatoa taarifa BoT kuwa mtu A tulimzoea kwenye akaunti yake ikiwa na Sh10,000 sasa leo ghafla imeanza kuingia Sh1,000,000.

Kinachofanyika, BoT hutoa taarifa vya vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi na hapo watabaini uhalali au fedha hizo zinaweza kuiondolea taifa usalama.

“Kwa hiyo tukiwa na uchumi wa kutumia fedha taslimu kulipa au njia za mitandao ya simu ni uchumi wenye faida kwa mtu na usalama wa mtu na taifa,” anasema.

Related Posts