Tanzania yazidi kupanda viwango vya Fifa

Kuvuna pointi nne kwa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Ethiopia na Guinea hapana shaka kumechangia kusogea huko kwa Tanzania katika viwango vya ubora wa soka duniani.

Tanzania imepanda hadi katika nafasi ya 110 kutoka ile ya 113 iliyokuwepo katika viwango vya ubora wa soka duniani vya mwezi Julai mwaka huu.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Tanzania, Uganda yenyewe imesogea kwa nafasi tano kutoka ile ya 95 hadi ya 90 kidunia, jambo linaloifanya iongoze kwa nchi wanachama wa baraza la vyama vya mpira wa miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Kuna kupanda kwa nafasi sita kwa Kenya ambayo kwa mujibu wa viwango vya ubora wa soka vya leo Septemba 19, 2024, ipo nafasi ya 102 kutoka nafasi ya 108 iliyokuwepo awali.

Nafasi za timu nyingine za ukanda wa Cecafa kwenye viwango hivyo vya ubora wa soka vilivyotolewa leo ni kama zinavyoainishwa hapo chini.

Sudan imepanda kwa nafasi moja kutoka 121 hadi 120, Rwanda imepanda kutoka nafasi ya 131 hadi ya 130 na Burundi imesogea kwa nafasi tatu kutoka nafasi ya 139 hadi ya 136 mtawalia.

Ethiopia imeshuka kwa nafasi mbili kutoka nafasi ya 143 hadi nafasi ya 145 huku Sudan Kusini ikishuka kwa nafasi tatu kutoka nafasi ya 169 hadi nafasi ya 172.

Djibouti imepanda kutoka nafasi ya 193 hadi ya 192, Somalia imebakia katika nafasi yake ya 202 huku Eritrea ikishika mkia kidunia.

Nchi tano zinazoongoza kidunia ni Argentina, Ufaransa, Hispania, England na Brazil wakati kwa Afrika vinara ni Morocco, Senegal, Misri, Ivory Coast na Tunisia.

Viwango vipya vya ubora wa soka duniani vinatarajiwa kutolewa Oktoba 24 mwaka huu.

Related Posts