Dar es Salaam. Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania wamesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia ili kuimarisha umoja na amani katika taifa hilo.
Mabalozi hao wamebainisha hayo leo Alhamisi Septemba 19, 2024 wakati wa mkutano wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia inayoadhimishwa kila Septemba 15 na maadhimisho hayo yameambatana na majadiliano kuhusu tathmini ya hali ya demokrasia nchini.
Mkutano huo ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwano Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Mwenyeki wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku na mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Mwenyekiti wa TCD, Freeman Mbowe.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima na Askofu wa Kanisa la Uamsho la Moravian Tanzania, Emmaus Mwamakula.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle amesema siku zote Marekani imewekeza kwa watu na demokrasia, hivyo wanathamini mchakato wa demokrasia unaowahusu watu moja kwa moja.
Amesema siku za hivi karibuni kuelekea kwenye uchaguzi, Tanzania na Marekani zimekabiliwa na vurugu ambazo zinatishia mchakato wa demokrasia katika mataifa hayo.
“Ni wazi kwamba mauaji na kupotea kwa watu hazitakiwi kuwa na nafasi katika demokrasia yetu, si Marekani wala hapa Tanzania,” amesema Balozi Battle.
Balozi huyo amebainisha mwaka huu, Tanzania ina fursa ya kufanya uchaguzi huru na wa haki wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 na kila Mtanzania anatakiwa kuwakilishwa katika mchakato huo.
Amesisitiza Marekani na Tanzania zina ushirikiano wa muda mrefu na katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Marekani imetoa Dola za Marekani 7.5 bilioni kwa ajili ya kuimarisha uchumi, afya na elimu kwa Watanzania.
“Tunafurahi washirika wa Tanzania…Hatutarudi nyuma, inapokuja kwenye masuala ya haki za binadamu ambayo ndio msingi wa demokrasia,” amesema Battle.
Kwa upande wake, Balozi wa Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe De Boer amesema demokrasia ni mchakato unaomtaka kila mmoja kushiriki, iwe ni wananchi, asasi za kiraia au vyama vya siasa.
“Demokrasia siyo uwakilishi wa vyama vya siasa, bali ni uwakilishi wa wananchi wote katika kufanya uamuzi,” amesema Balozi Boer.
Amesisitiza tathmini ya demokrasia inaangazia mambo muhimu kama vile uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa vyombo vya habari, haki za binadamu na utawala wa sheria.
Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan amesisitiza ushirikishwaji wa wanawake na wasichana katika mchakato wa kidemokrasia hasa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwa sababu nao wana uwezo wa kuwa viongozi.
Amebainisha asilimia 2 pekee ya wanawake ndiyo viongozi wa vijiji wakati asilimia 12 pekee ni wenyeviti wa mitaa. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanawake kwenye mchakato mzima na kuwapa nafasi hiyo.
“Uchaguzi wa serikali za mitaa ni muhimu katika kubadilisha hali hii kwa kutambua kwamba wanawake wana uwezo wa kuwa viongozi. Ni muhimu kuwashirikisha wanawake na wasichana katika mchakato wa kidemokasia,” amesema.
Endelea kufuatilia zaidi kujua kinachoendelea katika kikao hicho.