Dar es Salaam. Watanzania wanajiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, 2024, huku kumbukumbu za kuvurugika kwa uchaguzi uliopita wa mwaka 2019 na ule wa 2020 zikiendelea kuumiza vichwani mwao.
Wadau wa siasa kila wanapopata fursa kwenye majukwaa hukumbushia matukio yaliyotikisa kwenye uchaguzi huo, huku wakitahadharisha yasitokee tena kwani, yameacha doa kwa demokrasia ya Tanzania.
Hata hivyo, Jaji mstaafu Joseph Warioba amesema kilichotokea katika uchaguzi huo ilikuwa ni ajali na kwamba, hakikupangwa.
“Nasema ilikuwa ajali kwa sababu kilichofanyika hakikuwa katika utaratibu wa kawaida wa mchakato wa uchaguzi. Kila uchaguzi una dosari lakini kilichotokea mfano mawakala wengi walisambaratishwa. Hata upigaji na uhesabu kura wenyewe ulikuwa tatizo. Halikuwa jambo la kawaida.
“Sasa hivi ugomvi mkubwa uliopo ni je wale waliosimamia uchaguzi huo ndio wataendelea kuusimamia unaokuja na je, wanaaminika ndio swali lililipo,” amesema Jaji Warioba.
Jaji Warioba ametoa kauli hiyo leo Septemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kilichowakutanisha wadau kujadili tathmini ya hali ya demokrasia nchini.
Mkutano huo unafanyika huku taifa likitarajia kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24, mwaka huu kisha uchaguzi mkuu mwakani.
Jaji Warioba ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, amesema tangu mwaka 1994 hadi 2014 uchaguzi wa Serikali za mitaa ulikuwa ukisimamiwa na Serikali na kulikuwa na dosari za hapa na pale lakini, kwa ujumla ulikuwa huru na haki.
“Kipindi hicho chote hata vyama vya upinzani viliweza kushinda viti, lakini changamoto inakuja mwaka 2019 kulibadilika kabisa tukajikuta kama tumerudi katika mfumo wa chama kimoja,” amesema.