MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Mohamed Mang’una amesema kuwa, mafanikio katika sekta ya afya yaliyopo mkoani humo yanatokana na ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.
Awali, katika taarifa iliyopita, Dk. Mang’una amesema kuwa zaidi ya watoto 430, wanazaliwa kwa siku katika mkoa huo ambapo kati yao, watoto 100 ambao ni sawa na asilimia 22 hadi 23 wanahitaji matibabu zaidi kutokana na changamoto mbalimbali wanazozaliwa nazo.
Amesema kuwa, watoto hao wanzaliwa katika hospitali binafsi na awrikali, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa, kumekua na maboresho katika sekta ya afya hususani Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza hivi karibuni, Dk Mang’una anasema kuwa, licha ya serikali kujenga zahanati na vituo vya afya ngazi ya kata Ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za Wilaya, Mkoa na Rufaa, kumekua na ongezeko la hospitali, zahanati na vituo vya afya vya watu binafsi kuanzia ngazi ya mtaa, kata hadi hospitali kuu ambazo zimekua zikitoa huduma mbalimbali ikiwamo ya mama na mtoto.
Dk. Mang’una anasema kuwa, kuzinduliwa kwa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kumeleta chachu ya ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi lakini pia imeleta chachu ya utoaji wa huduma bora za matibabu kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
” Asilimia 84 ya hospitali, zahanti na vituo vya afya vinamilikiwa na watu binafsi, huku serikali ikimiliki asilimia 14, jambo ambalo linasaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya mkoani kwetu lakini pia kupunguza mlundikano wa wagonjwa waliokua wakipatiwa matibabu katika hospitali za kata.
” Wagonjwa wenye matatizo ndio wanaolazimika kupewa rufaa kwenye ngazi ya Wilaya, Mkoa au hospitali za rufaa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),” amesema Dk. Mang’una.
” Mkoa wetu kwa siku tunaweza kuzalisha watoto 430 katika hospitali mbalimbali zilizopo Mkoani kwetu na kati yao, watoto 100 ambao ni sawa na asilimia 22 hadi 23 wanahitaji huduma ya ziada ya matibabu, jambo ambalo tunalimudu kutokana na kuwepo kwa watalaamu wa afya, vifaa tiba na qatumiahi kutimiza wajibu wao,” amesema Dk. Mang’una.
Ameongeza kuwa, hayo ni mafanikio, kwa sababu wananchi wanapata huduma ya mbalimbali ikiwamo ya afya ya uzazi ya mama na mtoto, kujifungua na hata watoto kupelekwa kliniki kuanzia ngazi ya mtaa, jambo ambalo linapunguza mlundikano wa wagonjwa katika hospitali kubwa.
Amesema kuwa, wakaguzi wa afya kwa kushirikiana na maofisa Ustawi wa jamii ngazi ya kata wamekuwa wakipita kwenye hospitali na vituo hivyo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuangalia mazingira ya utoaji wa huduma za afya, ikiwamo ya mama na mtoto, vifaa tiba, watumisji wenye sifa na changamoto zilizopo ili ziweze kufanyiwa maboresho.
Ameongeza kuwa, mkakati iliyopo ni kuendelea kutoa huduma bora za afya ikiwamo ya uzazi salama ili wanawake wanaojifungua katika maeneo hayo waweze kujifungua salama na watoto wenye afya Bora.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa huo, Nyamala Elisha amesema kuwa, wamekuwa wakishirikiana na watalaam wa afya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vituo vya utoaji wa huduma za afya Ili kuangalia mazingira yaliyopo na kutoa ushauri.
” Watalaam wanakagua vituo vyote iwe vya serikali au sekta binafsi Kwa sababu wanaopewa huduma hizo ni wananchi, hivyo basi ni muhimu huduma zikatolewa kwa usawa Ili kupunguza vifo vya mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano.
” Lakini pia tumekua tukishirikiana na Ofisa Lishe kwa ajili ya kutoa elimu ya lishe kwa wagonjwa na wazazi wanaoleta watoto kliniki Ili waweze kuwapa lishe Bora jambo ambalo linawexa kupunguza udumavu,’ amesema Nyamala.
Amesema kuwa, gharama zinazotozwa katika hospitali hizo ni rafiki Kwa sababu zinaakisi mazingira husika, hivyo basi mwananchi ndio mwenye uamuzi aende kujifungua kwenye kituo cha afya cha kata au binafsi kulingana na uwezo wake.
Baadhi ya wananchi wanasema kuwa, ongezeko la vituo vya afya vya binafsi ngazi ya kata na mtaa linasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za Serikali.
” Mfano Mimi nilienda kituo cha afya cha watu binafsi ambacho kipo jirani na makazi yangu Kwa ajili ya kujifungua, kina huduma zote za mama na mtoto, wauguzi na madaktari ni wale wenye uzoefu na hata lugha ya matusi hakuna.
” Nilipolazwa wakaguzi walikuja wakatuhoji na kuondoka, kwangu hayo ni mafanikio makubwa kkwa sababu miaka ya nyuma huduma hizo zilikua hazipo na kama vilikuwepo baadhi ya maeneo, watalaam wachache, lugja za matusi, vifaa tiba hakuna,” amesema Fransisca Ismael mkazi wa tank bovu Manispaa ya Kinondoni.
Ameongeza kuwa, maeneo karibu na anapoishi kuna kituo cha afya cha serikali, lakini aliamua kujifungulia kwenye hospitali binafsi kutokana na ukaribu wa uamuzi wake Kwa sababu huduma zinazotolewa kwenye kituo cha afya cha serikali ni sawa na Cha binafsi.
Naye Asha Juma mkazi wa Magomeni Manispaa ya Kinondoni amesema kuwa, Mwaka 2020 alijifungua salama katika kituo cha afya cha Magomeni na mpaka sasa mtoto wake anaendelea vizuri na anaptiwa huduma ya kliniki kwenye kituo hicho.
Amesema kuwa, kuwepo Kwa vituo vya afya vya serikali na binafsi vimesaidia kuboresha Kwa utoaji wa huduma za afya kuanzia ngazi ya mtaa Hadi kata, jambo ambalo limepunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali kubwa zilizokua zikitoa huduma ya afya ya mama na mtoto Mkoa wa Dar es Salaam.
” Zamani ukitaka kujifungua lazima uende hospitali za Muhimbili, Amana, Temeke na Mwananyamala, lakini sasa hivi hali ni tofauti ambapo katika maeneo mengi kuna kituo cha kutoa huduma za afya ya mama na mtoto au kuna hospitali binafsi, ambalo limepunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali kubwa za Mwananyamala,Temeke, Ilala na Muhimbili,” amesema Asha.
Amesema kuwa, mama mjamzito akifika kwenye kituo cha matibabu ananyenyekewa mpaka atakapojifungua na kuomba serikali kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara pamoja na kutoa elimu kwa watoa huduma za afya Ili waweze kuendelea kuwapenda wagonjwa na kuishi kwenye viapo vyao.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne,Jakaya Kikwete amesema kuwa, serikali imejitahidi kupunguza vifo vya kina mama wajawazito kutoka 556 kwa mwaka 2016 mwaka hadi kufikia 104 kwa mwaka 2022.
Amesema kuwa, kupungua kwa vifo hivyo kunatokana na kujengwa vituo vya afya kila kata pamoja na kuongeza watalaam wa afya wakiwamo madaktari, wauguzi na watalaam wengine iii waweze kutoa huduma bora kwa wananachi.
Amesema kuwa, inafedhehesha kuona mama mjamzito ambaye analeta kumbe duniani anafariki kutokana na kukosa huduma bora za afya.
Aliwataka watalaam wa sekta ya afya na watalaam wengine kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kuisaidia serikali kupungiza vifo vitokanavyo na uzazi na wajawazito waweze kupata uzazi salama wao na watoto wao.
Hata hivyo, serikali ilisaini Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendelo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kuanzia umri sifuri hadi miaka minane ili kuhakikisha watoto wanaozaliwawanapata malezi jumuishi katika afua ya afya,,elimu, lishe, ulinzi na usalama na malezi yenyewe mwitikio.