BAADA ya kucheza mechi tatu mfululizo bila kufunga bao lolote, jioni ya leo Alhamisi, Azam FC ikiwa chini ya kocha Rachid Taoussi imepata ushindi mnono kwa kuishindilia KMC mabao 4-0 katika mfululizo w mechi za Ligi Kuu Bara.
Azam ikicheza uwanja wa ugenini wa KMC Complex, ilipata ushindi huo uliokuwa wa kwanza msimu huu katika ligi na wa kwanza kwa kocha Taoussi aliyetua hivi karibuni kutoka Morocco na kuifanya ichupe kutoka nafasi ya 12 hadi ya sita kwa kufikisha pointi tano.
Katika mchezo huo mkali ambao Azam ilitembeza boli mwanzo mwisho, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Feisal Salum ‘Fei Toto’ aling’ara kwa kuasisti mara mbili, lakini akihusika pia kwa bao la nne ambalo beki wa KMC, Fredy Tangalo alijifunga katika harakati za kuokoa mpira mbele ya Nathaniel Chilambo.
Azam iliana karamu ya mabao dakika ya 19 wakati Fei Toto alipomnyang’anya mpira beki wa KMC na kumpasia Idd Seleman ‘Nado’ aliyeukwamisha kwa kumopiga chenga kipa Fabien Mutombora bado lililodumu hadi mapumziko, licha ya wenyeji kucharuka kwa kutaka kulisawazisha.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Azam kuongeza bao la pili dakika ya 55 kupitia kwa nahodha Lusajo Mwaikenda aliyemaliza kazi nzuri ya Fei Toto na dakika tano baadae Nassor Saadun aliandika bao la tatu lililokuwa tamu kutokana na kuwapiga chenga mabeki watatu wa KMC sambamba na kipa Mutombora.
Wakati KMC akijiuliza watayarudisha vipa mabao hayo, Fei Salum aliambaa pembeni mwa uwanja na kupiga krosi iliyookolewa vibaya na mabeki wa wenyeji kabla ya Chilambo kuusuma wavuni mpira uliopigwa na beki Tangalo dakika ya 67.
Hata hivyo marudio ya bao hilo ilionyesha Tango amejifunga.s
Matokeo hayo yameiacha KMC iliyocheza mechi nne kusaliwa na pointi nne, ikishika nafasi ya nane, lakini iklilifanya pambano hilo kuwa la pili msimu kuu kuwa na mabao mengi baada ya ile ya Simba dhidi ya Fountain Gate iliyolala pia 4-0 kwenye uwanja huo wa KMC Complex, uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, sio mara ya kwanza kwa KMC kufungwa na Azam kwa idai kubwa ya mabao, kwani msimu uliopita katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu ilifumuliwa mabao 5-0.
Rekodi za ujumla zinaonyesha KMC imepoteza mechi nane kati ya mechi 13 ilizokutana na Azam tangu 2018 (ilipopanda Ligi Kuu) na yenyewe ikishinda mara tatu tu, huku michezo miwili ikiisha kwa sare.
2023-2024
KMC 1-2 Azam
Azam 5-0 KMC
2022-2023
KMC 2-1 Azam
Azam 1-0 KMC
2021-2022
KMC 2-1 Azam
Azam 2-1 KMC
2020-2021
KMC 1-0 Azam
Azam 2-1 KMC
2019-2020
KMC 0-1 Azam
Azam 3-1 KMC
2018-2019
KMC 2-2 Azam
Azam 0-0 KMC