Dar es Salaam. Ikiwa imesalia miezi mitatu kabla ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT), awamu ya pili kutoka Mbagala hadi Gerezani kuanza, Kampuni ya Scania Tanzania Limited imeonyesha nia ya kuuza mabasi yatakayofanya kazi katika mradi huo.
Kwa mara ya kwanza leo Septemba 19, 2024 kampuni hiyo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram imeonyesha aina ya mabasi hayo aina ya Scania Marcopolo.
“Tuna habari ya kusisimua kitu kizuri kinakuja hivi karibuni! Jiandaeni kuona basi hili zuri lililoundwa mahususi kwa ajili ya Tanzania. Tuna furaha kuliona likifanya kazi kwenye laini ya BRT hivi karibuni,” imesema sehemu ya taarifa ya Scania.
Juhudi za kupata taarifa zaidi kutoka kwa Kampuni ya Scania kuhusu basi hilo hazikufanikiwa. Mmoja wa wafanyakazi alimtaka mwandishi wa habari kutuma maswali, hata hivyo hayakujibiwa.
Kampuni hiyo imeonyesha basi hilo ikiwa umepita mwezi mmoja tangu Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla kueleza zaidi ya mabasi 200 yanatarajiwa kuanza kufanya kazi kwenye njia ya Mbagala-Gerezani ifikapo Desemba, 2024.
Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart), Dk Athuman Kihamia, alilieleza gazeti dada The Citizen kwamba Serikali haina mkataba na kampuni hiyo kuhusu mabasi yaendayo haraka.
“Huko nyuma Serikali iliwahi kuwa na mazungumzo na kampuni hiyo kwamba walete mabasi ili Serikali inunue kwa ajili ya mradi wa BRT, lakini mazungumzo hayo hayakuendelea baada ya sera ya BRT kutoka,” amesema.
Amesema sera ya BRT inahitaji sekta binafsi na umma kununua mabasi, wakati Serikali kupitia Dart, itakuwa inasimamia miundombinu.
Dk Kihamia amesema wakala kwa sasa uko kwenye mchakato wa zabuni kutafuta mtoa huduma, na mpango unakwenda kwa kasi nzuri.
Amesema wazabuni watatu wa nje na ndani ya nchi wameonyesha nia ya kushiriki katika zabuni hiyo.
“Pale mshindi atakapobainishwa, tutatangaza na mikataba itakamilishwa. Basi ambalo linaonekana kwenye mitandao ya kijamii ni mfano unaonyeshwa ili mfanyabiashara yeyote anayevutiwa aendelee na ununuzi, tangu mwaka jana lilionyeshwa kwa Serikali iweze kuona aina, lakini kwa sasa hatuna mazungumzo hayo,” amesema.
Ripoti zilizopo zinaonyesha BRT awamu ya kwanza kutoka Kimara-Kivukoni-Gerezani-Morocco bado inahitaji mabasi 170 ili kufanya kazi kwa ufanisi, mabasi 500 yanahitajika kuanza kufanya kazi kwa BRT awamu ya pili kwenye njia ya Mbagala.
Katika siku za karibuni, wamiliki wa mabasi walisema wana nia ya kuwekeza katika mradi wa BRT endapo maboresho yangefanyika katika ukusanyaji wa nauli na mikataba ya uendeshaji.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Joseph Priscus ameliambia The Citizen wiki iliyopita kwamba mazungumzo na Dart yalifanyika mwaka 2022, ambayo waendeshaji mabasi walipendekeza kununua mabasi ili kufanya kazi ndani ya miundombinu ya BRT lakini bado hawajapata mrejesho.
Mwanzoni mwa Septemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Mohamed Mchengerwa aliwataka Dart na Udart kushirikiana katika kuunganisha wamiliki wa mabasi kwenye mfumo wa BRT, ili kuboresha huduma za usafiri wa abiria badala ya kungojea wawekezaji wa kigeni.